Bwalya |
KALUSHA
BWALYA:
SAHAU kuhusu
Zambia iliyochukua Kombe a Challenge mwaka 2006, wakati huo imekwishajitoa
katika nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati
(CECAFA) na kuingia nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA).
Zambia
iliyotikisa katika soka ya Afrika Mashariki na kati ni ile iliyokuwa ikiitwa KK
Eleven kuanzia miaka ya 1970 hadi 1990 mwanzoni, kabla ya ajali ya ndege iliyoua
nyota wa kikosi hicho pwani ya Gabon mwaka 1993.
Kalusha
Bwalya alikuwa katika orodha ya wachezaji waliotakiwa kuingia kwenye ndege
iliyopata ajali, lakini bahati nzuri kwake alisema atatokea kwenye klabu yake
moja kwa moja Ulaya kwenda Tunisia, hivyo akanusurika.
Katika
historia yake ya ushiriki wa Challenge, KK Eleven ilibeba taji hilo mwaka 1984
na 1991 ambao, Kalusha Bwalya aliungana na Majid Musisi katika ufungaji bora,
kila mmoja akifunga mabao yake matatu.
Challenge ya
mwisho kwa Bwalya ilikuwa mwaka 1992 mjini Mwanza, alipoiongoza Zambia hadi Nusu
Fainali ilipotolewa na Uganda kwa penalti 4-2, Uwanja wa CCM Kirumba kufuatia
sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
Huwezi
kuizungumzia historia ya Challenge bila ya kumtaja Bwalya, aliyezaliwa Agosti
16, mwaka 1963 mjini Mufulira, kwani enzi zake alikuwa mkali haswa.
Huyo ni
mchezaji aliyeichezea Zambia mechi nyingi zaidi na kuifungia mabao mengi zaidi
pia kuliko mchezaji yoyote hadi sasa. Ndiye mchezaji babu kubwa zaidi kuwahi
kutokea katika ardhi ya Zambia. Unamzungumzia Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka
1988, ambaye mwaka 1996 aliingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka
Bora wa Dunia, ambayo ilichukuliwa na Mwafrika mwenzake, George
Weah.
Omondi Philip |
UGANDA ndio
mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Challenge, wakiwa wamebeba Kombe hilo
mara 12 (1973, 1976,
1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003, 2008, 2009 na
2011).
Wapo
wachezaji wawili ambao huwezi kuwatenganisha na mafanikio ya The Cranes katika
Challenge. Akina nani hao?
Wote hawa
wamekwishatangulia mbale ya haki hivi sasa, Philip Omondi na Majjid
Musisi.
Phillip
Omondi aliyezaliwa mwaka 1957 na kufariki dunia Aprili 21, mwaka 1999 huyu
alikuwa mtu hatari sana enzi zake na waliobahatika kumuona wanaweza kukiri juu
ya hilo.
Omondi
aliyechezea klabu ya Kampala City Council FC kuanzia mwaka 1973 hadi 1979,
alipotimkia Sharjah ya Falme za Kiarabu (UAE) alikuwa shukaa wa Uganda hadi
kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Omondi
aliichezea The Cranes katika fainali za Afrika miaka ya 1974, 1976 na za 1978,
ambazo pamoja na kuifikisha Cranes fainali, pia aliibuka mfungaji
bora.
Kwenye
Challenge, Omondi aliisaidia mno Uganda kutwaa mataji ya mwaka 1973 na
1977.
Katika
fainali za mwaka 1978, mkali wa mabao wa zamani wa Uganda, Phillip Omondi
aliungana na Opoku Afriyie na Segun Odegbami katika ufungaji bora, kila mmoja
akipachika nyavuni mabao matatu. Leo Omondi hayupo duniani, lakini huwezi
kuzungumzia historia ya Challenge bila kumtaja yeye.
Musisi |
MAJID
MUSISI:
NI kweli,
Philipo Omondi alikuwa noma enzi zake, lakini unaweza kusema nini kuhusu Majid
Musisi Mukiibi?
Mshambuliaji
huyo aliyezaliwa Septemba 15, mwaka 1967 kabla ya kufariki dunia Decemba 13,
mwaka 2005 vyombo vya habari Uganda vimechekecha vikaamua kuweka bayana, huyo
ndiye mchezaji bora zaidi kihistoria kuwahi kutokea nchini humo.
Musisi,
ambaye ni mchezaji wa kwanza wa Uganda kucheza soka ya kulipwa Ulaya, alikuwa
ana majina mawili maarufu ya utani enzi zake, ambayo ni Tyson na Magic. Tyson
kwa sababu alikuwa mkorofi na Magic ni kwamba soka yake iliitwa ya
miujiza.
Huyo
aliisaidia The Cranes kutwaa Kombe la Challenge katika miaka ya 1989 na 1990.
Mfumo wa maisha ya kuendekeza pombe, ulimfanya afananishwe na magwiji wa soka
duniani akina George Best, Eric Cantona au Paul Gascoigne ‘Gazza’.
Musisi
alikuwa ana utajiri miguuni mwake na mabeki kwa pamoja na makipa walikuwa
wanamheshimu sana mtu huyo. Alikuwa hashindwi kufanya jambo anapoamua kufanya
kwa juhudi zake zote.
Umaarufu
wake uliwavutia vijana wengi kucheza soka Uganda na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Jamaa alikuwa anaijua soka.
Nteze John |
NTEZE
JOHN:
WENGINE
wanaweza kujiuliza kwa nini siyo Sunday Manara ama Zamoyoni Mogella, Peter Tino
au Edibily Lunyamila, lakini jibu ni kwamba, wote hao hawafui dafu mbele ya
Nteze John Lungu kwa kufanya vitu vikubwa kwenye Kombe la
Challenge.
Haimaanishi
Nteze alikuwa anawazidi kisoka akina Abdallah Kibadeni, Mogella, Lunyamila, Said
Mwamba Kizota na wengine waliowahi kuwika katika soka ya Tanzania, la hasha- ila
Nteze aling’ara zaidi yao kwenye michuano hiyo.
Huyo ndiye
aliyekuwa shujaa wetu wakati tunachukua taji la pili la michuano hiyo, mwaka
1994 mjini Nairobi, Kenya.
Mabao yake
manne aliyofunga katika Kundi A, kwenye michuano hiyo yaliifanya Tanzania Bara
iongoze kundi hilo kwa pointi tisa ilizokusanya kutoka na kushinda mechi zote za
kundi lake, Nteze akifunga katika kila mechi.
Novemba 29,
Tanzania ikiitandika Somalia mabao 4-0, Nteze alifunga mabao mawili katika
dakika za 11 na 84, mengine yakifungwa na George Masatu dakika ya 67 na Madaraka
Suleiman dakika ya 74.
Siku mbili
baadaye Nteze alifunga bao pekee la ushindi dakika ya 57, Bara ikiwafunga
wenyeji Kenya 1-0, wakati Desemba 3, Bara ikiichapa Djibouti 3-0, Nteze alifunga
la tatu dakika ya 75, baada ya Edward Chumila (sasa marehemu) kufunga dakika ya
pili na Clement Kahabuka dakika ya 30.
Nteze
hakufunga katika mechi mbili zilizofuata, Nusu Fainali dhidi ya Eritrea, bao
pekee la Said Mwamba ‘Kizota’ dakika ya saba likiipa Bara ushindi wa 1-0 na
fainali, ambayo baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 120 dhidi ya Uganda, Bara
ilifanikiwa kutwaa Kombe kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Ilikuwa ni
Desemba 10, wakati mabao ya Stars yalipotiwa kimiani na Juma Amir Maftah dakika
ya 14 na Kizota dakika ya 40 wakati Iddi Batambuze aliifungia Uganda dakika ya
47 kabla ya George Ssemogerere dakika ya 88 kusawazisha.
Nteze
aliibuka pia mfungaji bora wa michuano hiyo kwa mabao yake manne na kutwaa Kiatu
cha Dhahabu.
Oliech |
DENNIS
OLIECH:
WAMETOKEA
wanasoka wengi Kenya ambao waling’ara kwenye Challenge, lakini kama ilivyo kwa
wachezaji wa Tanzania unahitajika utulivu wa hali ya juu, ili kumtaja mmoja
ambaye daima anastahili kukumbukwa katika historia ya michuano hiyo.
Mfungaji wa
bao la tatu na la ushindi katika dakika ya 72 ya fainali ya Kombe la Challenge
Desemba 14, mwaka 2002 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Tanzania Bara ikilala
3-2 na kupoteza matumaini ya kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu.
Nani zaidi
ya Dennis Oliech. Na kwa nini asahaulike mtu huyo siyo tu kwa kuwakomoa wenyeji
na kuwapokonya tonge mdomoni, bali soka yake iliyomuuza Ulaya
baadaye.
Siku hiyo,
Emmanuel Gabriel alitangulia kuifungia Bara dakika ya 28, kabla ya Paul Oyuga
kusawazisha dakika ya 30 na Mecky Mexime kufunga la pili kwa penalti dakika ya
59 na John Barasa kuisawazishia Harambee Stars dakika ya 70 na Oliech kupiga la
ushindi dakika ya 72.
Oliech
alikuwa mfungaji bora katika fainali hizo kutokana na mabao yake matano, akiwa
ana umri wa miaka 17 tu wakati huo.
Oliech
alizaliwa Februari 2, mwaka 1985, baada ya kung’ara kwenye fainali hizo, mwaka
2003 alinunuliwa na Al-Arabi ya Qatar hadi mwaka 2005, aliposaini mkataba wa
miaka minne na FC Nantes ya Ufaransa na kuanza safari yake kuogelea kwenye
bwala la fedha Ulaya na sasa anachezea Auxerre.
Aliiwezesha
Kenya kukata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004
na alicheza vizuri kwenye fainali hizo nchini Tunisia na mwaka huo huo
akatabiriwa kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari baadaye duniani, akiwekwa
katika orodha moja na Wayne Rooney wa Manchester United. Oliech kwa sasa ameipa
kisogo michuano ya Challenge, ingawa bado anaichezea Harambee Stars katika
michuano mikubwa, ila Challenge ndio iliyomtoa.
Post a Comment