Na Mahmoud
Zubeiry wa Bin Zubeiry, Kinshasa
AZAM FC ya
Dar es Salaam, imefungwa mabao 2-0 na Shark FC ya hapa, katika mchezo wake wa
mwisho wa Kundi B, Kombe la Hisani, kwenye Uwanja wa Martyrs jioni
hii.
Mabao ya
washindi, timu inayomilikiwa na mdogo wake rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), Joseph Kabila yalifungwa na Ndibu Kalala dakika ya 23 na Kalala
Kabongo dakika ya 34.
Hata hivyo,
kipigo hicho kimechangiwa kwa kiasi kikubwa na uchezeshaji mbovu wa marefa,
ambao tangu mwanzo walionekana kuwapendelea
wenyeji.
Azam leo
imenyimwa penalti mbili za halali, moja kila kipindi, ya kwanza baada ya shuti
la mshambuliaji Gaudence Mwaikimba kuzuiwa kwa mkono na beki wa Shark na ya pili
kiungo Humphrey Mieno aliangushwa kwenye eneo la hatari, tena ndani ya sita
akiwa amekwishamtoka kipa, lakini zote refa
akapeta.
Washika
vibendera nao walizima mashambulizi kadhaa ya Azam kwa kudai wachezaji walikuwa
wameotea.
Mabao yote
Azam walifungwa wakitoka kushambulia na hayakuwa na mushkeli, makosa ambayo
walirekebisha na hawakuyarudia kipindi cha pili. Kipindi cha kwanza, timu
zilishambuliana kwa zamu, lakini kipindi cha pili Azam walitawala zaidi mchezo
na kama si ‘madudu’ ya refa, matokeo yangeweza
kubadilika.
Kwa matokeo
haya, Shark inaongoza Kundi B kwa pointi zake tatu, ikifuatiwa na Dragons
iliyotoka 1-1 na Azam katika mchezo wa kwanza.
Azam sasa
itaomba Shark iifunge zaidi ya mabao 2-0 Dragons katika mechi ya mwisho ya kundi
hilo Desemba 23, ili ifuzu kuingia Nusu Fainali.
Azam
imecheza mechi zote mbili bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall
na Msaidizi wake, Kali Ongala ambao walibaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari
Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche raia wa Ivory
Coast, kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.
Nusu Fainali
zitachezwa Desemba 25 wakati Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka
mshindi wa tatu. Kundi B, lina timu za DC Motema Pembe, Diables Noirs, FC MK na
Real De Kinshasa.
Kocha wa
makipa, Iddi Abubakar aliyeiongoza timu hiyo katika mechi hizo mbili
alilalamikia uchezeshaji wa marefa, ambao walisindikizwa na Polisi kutoka
uwanjani baada ya mechi, kutokana na kuwakera hata mashabiki wa timu za hapa
waliotaka kuwafanyia fujo.
Kikosi cha
Azam leo kilikuwa; Mwadini Ally, Malika Ndeule/Uhuru Suleiman dk 85, Samih Hajji
Nuhu, Luckson Kakolaki/Omar Mtaki dk 65, David Mwantika, Jabir Aziz, Ibrahim
Mwaipopo/Himid Mao dk80, Humphrey Mieno, Seif Abdallah, Gaudence Mwaikimba na
Waziri Salum/Abdi Kassim ‘Babbi’ dk 65
Post a Comment