Mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa, Christopher Sanya, alitoa kauli hiyo mjini hapa alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na msimamo wa chama kuhusu matukio hayo.
Sanya alisema chama kimeshtushwa na matukio ya mauaji mfululizo na kusema licha ya kuua watu lakini pia yanazidi kuupa sifa mbaya mkoa wa Mara.
Alisema chama hicho hakiwezi kuvumilia watu wakichinjwa na kuporwa mali zao wakati waliopewa dhamana ya kulinda raia wapo na kwamba ni wajibu wao kusimamia na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani.
Aliwataka wananchi wa mkoa huo kutokuwa na hofu, kwani mauaji hayo hayafanyiki mkoani Mara pekee bali hata mikoa mingine na kwamba chama kimeshaliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linakomesha mauaji hayo.
Takriban mwezi mmoja sasa wananchi wa mkoa wa Mara wamekuwa wakiishi kwa hofu baada ya kutokea mauaji ya mara kwa mara ambapo wauaji wamekuwa wakiondoka na viungo mbalimbali kama vile vichwa.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment