MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo ya bidhaa za mafuta ya petroli nchini ambayo imeongezeka kwa sh 70 kwa lita sawa na asilimia 3.4.
Hatua hiyo ni wazi kuwa itasababisha gharama za nauli kuwa juu, pamoja na usumbufu kwa abiria katika nyakati hizi za kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Anastas Mbalawa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Haruna Masebu, alisema kuwa bei hizo zitaanza kutumika kuanzia leo na kuwataka wamiliki wa vituo vya mafuta kutambua bei kikomo ya bidhaa hizo.
Taarifa hiyo ilitaja bei hizo katika Jiji la Dar es Salaam kwa petroli itakuwa sh 2,119, dizeli sh 1,999 na mafuta ya taa sh 2,023; Arusha petroli sh 2,203, dizeli sh 2,083 na mafuta ya taa sh 2,107 huku Dodoma petroli itauzwa sh 2,146, dizeli sh 2,058 na mafuta ya taa sh 2,082.
Mkoani Iringa petroli itauzwa kwa sh 2,183, dizeli sh 2,063 na mafuta ya taa sh 2,087, huku Morogoro petroli itauzwa kwa sh 2,144, dizeli sh 2,024 na mafuta ya taa sh 2,048 na Bukoba petroli sh 2,334, dizeli sh 2,214 na mafuta ya taa sh 2,238.
Alisema kuwa bei za jumla na rejareja kwa mafuta aina zote ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita la Novemba 7, 2012.
“Katika toleo hili, bei za rejareja kwa dizeli imeongezeka sh 10 kwa lita sawa na asilimia 0.53, bei ya mafuta ya taa imepungua kwa sh 3 kwa lita sawa na asilimia 0.1, huku bei za jumla kwa kulinganisha matoleo haya mawili zimeongezeka petroli kwa sh 69.56 kwa lita sawa na asilimia 3.52; dizeli kwa sh 10.04 kwa lita sawa na asilimia 0.52,” alisema.
Alisema kuwa bei ya mafuta ya taa imepungua kwa sh 3 kwa lita sawa na asilimia 0.15 huku akisema kuwa mabadiliko ya bei hizo yametokana na ongezeko la bei ya mafuta katika soko la dunia na kushuka kidogo kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Mbalawa alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko ambapo EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa hizo.
“Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na fomula mpya iliyopitishwa na mamlaka yetu na kuchapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 454 la Desemba 23, 2011,” alisema.
Aidha, alisema kuwa ni muhimu vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa hizo katika mabango yanayoonekana, huku ikionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
Alisema kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja, na kwamba adhabu itatolewa kwa kituo husika.
chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment