Kwa
dhati ya moyo wangu nimesikitishwa sana na taarifa zilizozagaa kwenye vyombo vya
habari kuhusu kujiuza kwa dada zetu wa UDOM. Wasomi ambao wana Dodoma na
watanzania kwa ujumla walitegemea kujifunza kutoka kwao. Taarifa hizi
zimenichochea kukaa chini na kuandika waraka huu huku nikizingatia ukweli kwamba
UDOM ndipo nilikosomea masomo yangu ya shahada ya kwanza; mbali na matatizo yote
yaliyonikumba katika safari hiyo ya kukamilisha shahada hiyo lakini nalazimika
kusema kitu kwa faida yetu wote.
Ikumbukwa
moja ya mategemeo ya jamii ya wana Dodoma kutoka kwenye chuo cha UDOM kilipo
anzishwa mwaka 2007 ilikuwa ni kujionea jamii staarabu iliyoelimika na yenye
kila sifa ya kuigwa, na pia jamii ya Dodoma ilitegemea watoto wao wangejionea
namna wasomi hawa wanavyoishi kwa kusadifu kwa vitendo elimu, maadili na mila
za nchi yao. Zaidi waliamini mambo hayo yangekuwa chachu ya kuwachochea vijana
wao kuzingatia masomo ili na wao siku moja wafikie elimu hiyo ya Chuo lakini
hali imekuwa tofauti kabisa. Leo jamii hii ya wana Dodoma wanashuhudia wasomi
wanaoshinda mitaani wakiranda randa na nguo za kuogelea na za kulalia kana
kwamba walikotoka hakuna wazazi, wanashuhudia wasomi wanaojiuza kama
njugu.
Ila
kwa hali nyingine naweza sema kuna kitu kilichofichika ndani kwani huwezi
kuniambia mwanchuo ana akili timamu akauze mwili wake kwa shilingi mia tano
(500) za kitanzania ukilinganisha na nauli ya kutoka chuo na kurudi tu ni
shilingi mia sita (600). Hapa nabaki na dukuduku kwani kuna watu wachache
wanataka kukichafua Chuo Kikuu cha Dodoma kwa maslahi yao binafsi. Hao wanabidi
wakemewe. huwezi kuniambia picha ndo kigezo tosha cha kusema huyu ni mwanachuo
wa UDOM kwani hajapatikana na kitambulisha na huwezi kuhukumu wakati huna
kithibitisho na ukilinganisha Dodoma kuna vyuo takribani saba (7) kama vile St.
John, CBE Dodoma, Chuo cha Madini, Chuo cha Mipango n.k kwanini kila kitu waseme
UDOM hapa mimi naweza sema kuna kitu
kilichofichika.
Kiukweli
siwezi hata siku moja kuruhusu kulea au kuipamba tabia hizo hata kama kuna
sababu za msingi ambazo zinaweza zikawa zimesababisha tatizo hili kutokea.
Kinachofanywa na dada zetu hawa ni kitendo ambacho kila mungwana anapaswa
kukikemea kwa nguvu, na zaidi ya yote ni wajibu wetu wote kama vijana kurudia
maadili yetu kama watanzania na kulaani kwa nguvu haya. Kama tutaruhusu tabia
hii ikaota mizizi tutaandaa wasomi wasio waadilifu na wasio jiamini, tutandaa
wasomi wenye shahada za kwenye chupi (nisamehewe kwa hiyo lugha lakini nimekosa
neno linalokidhi ninachomaanisha), tutaandaa wasomi walioathirika hivyo kupoteza
nguvu kazi ya taifa, tutaandaa taifa la wavivu na wasifikiri kwa
ufanisi.
Tukumbuke
kuruhusu tabia hii kubobea ni kuruhusu kuporomoka kwa elimu ambayo ni msingi wa
taifa lolote duniani. Na sidhani kama ni busara kuangalia umauti wa taifa letu
kwa kuruhusu tabia hii kuota mizizi, kwani dhambi hiyo haitaishia chuoni tu,
itaingia makazini na hapatakuwa na kazi zaidi ya uzinzi tu, baada ya hapo
dhambi hii itasambaaa hadi kwa watoto na wajukuu wetu na hatimaye itakuwa ndio
mfumo wetu wa maisha. Lakini mbali na yote niliyoeleza hapo juu ninayo yangu kwa
serikali yangu, vijana hawa wa UDOM ni watoto wenu na wengine wameingia pale
wakiwa hawana hata elimu ya kimaisha au ya kujitegemea, wengine wanakutana na
kila aina ya tabia pale.
Mimi
nilisha kuwa kiongozi wa mikopo UDOM-HSS kwa karibu miaka yote ya masomo yangu
ya shahada ya kwanza, naelewa kiasi sababu na wakati dada zetu hawa wanapojiuza.
Kipindi ambacho dada zetu hawa hujiuza huwa ni pale Bodi ya mikopo
inapochelewesha mikopo ya wanafunzi, hali huwa mbaya kiasi dada zetu hawa ufika
mahali wanalazimika kujidhalilisha ilimradi wapate chochote cha kujikimu. Na
ukizingatia majumbani kwao hawana msaada wowote
wanaoupata.
Mfano
mzuri wa ucheleweshaji wa mikopo kwa wanafunzi wa kozi ya Uhusiano wa Kimataifa
(BA IR) hawajapewa mikopo yao mpaka leo, na wanatakiwa kula, kunywa, kuwasiliana
na kununua vitini vya masomo ili hali familia walizotoka ni masikini wa
kutupwa. Haya yote ni mazingira hatarishi kwa dada zetu hawa. Serikali kama
mzazi nakuomba mliangalie kwa umakini sana suala hili ili tuwaepushie wale
wanajihusisha na tabia hii ya kuuza miili yao kutokana na kuishiwa au kukosa
fedha za kujikimu Muda mwingine unaweza kusema serikali inafanya makusudi
kuwacheleweshea mikopo yao wa sababu wanaonufaika sana na tabia hiyo ya dada
zetu kujiuza ni wabunge wanapokuja kwenye vikao vyao vya
bunge.
Kujiuza
kwa dada zetu hawa ni dhahiri ni matokeo ya mambo kadhaa ambayo serikali haina
budi kuyafuatilia kwa kina na hatimaye kutatua kwa ustawi wa tafa letu la
Tanzania. Hatupaswi kufurahia tabia hii hata kidogo kwani kufanya hivyo kunaweza
liathiri taifa letu kwa ujumla wake siku za usoni.
“Ukiona panafuka moshi ujue kuna moto”
IMEANDALIWA NA
ALEX NICHOLAUS THOMAS MUSHI
Post a Comment