MKE
wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda amesema kila mtu hana budi kumshukuru Mungu kwa
kumfikisha salama wakati wa sikukuu ya Noeli kwani kuna wengine ambao
walitamanikuiona siku hii lakini wameshindwa.
Ametoa kauli hiyo leo
mchana (Jumanne, Desemba 25, 2012) wakati wa ibada ya Krismasi iliyofanyika
katika kigango cha Kibaoni kata ya Kibaoni wilayani Mlele, mkoani
Katavi.
“Tunapaswa kumshukuru Mungu
kwa kutuwezesha kufika sikukuu hii, mpaka leo ni mapenzi yake hakuna binadamu
ambaye ana amri na maisha yake. Tutakumbuka hata mwaka jana tulikuwa na Askofu
wetu wa Jimbo la Mpanda lakini leo hii hatunaye, hivyo sote tunapaswa kumshukuru
Mungu kwa kutupa uhai,” alisema.
Alisema katika kuadhimisha
sikukuu hii watu hawana budi kuwa na kiasi, wasinywe sana hadi kusababisha
magomvi. Aliwasihi wazazi wawe karibu na familia zao, na wawajibike
kwao.
”Tumuombe Mungu atupe
neema, yale tuliyokosea mwaka 2012 tuyaache, tujiandae kuingia mwaka 2013 na
yale mazuri tuliyoyaona mwaka 2012,” alisema.
Naye Padre John Giji wa
Shirika la Wamisionari wa Mt. Thomas ambaye aliongoza ibada hiyo, aliwataka
waumini wa kigango hicho kuwajali wenye shida na siyo kujiingiza katika matendo
mabaya wakati wa sikukuu.
“Kuishi kwetu kuanzia leo
lazima kuwe na mabadiliko, ni lazima tuwajali wenzetu katika shida zao kwani kwa
kufanya hivyo, tutakuwa na mabadiliko ya kiroho na hivyo kuweza kukua kiimani,”
alisema Padre John ambaye pia ni Paroko wa Usevya.
“Wako watu wanasherehekea
Krismasi kwa matendo mabaya kama vile uzinzi na ujambazi. Huo siyo ukristu
tunaotegemewa kuwa nao katika familia takatifu ya Mungu. Tukifanya kazi kwa
bidii, hatuwezi kuwa na tamaa ya vitu vya wengine,”
alionya.
“Leo ni sikukuu, tufurahi
kwa amani bila jazba za kidunia. Tusherehekee kwa upendo na amani, ”
alisisitiza.
Post a Comment