
Msimamo huo wa serikali ulitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Membe alikiri kuwa serikali haikuwa makini katika kusimamia uchunguzi, badala yake ilikuwa mstari wa mbele kutoa usajili bila kubaini adhari za mbele.
Membe alifafanua kuwa, kampuni ya uwakala iliyosajili meli hizo, Philtex ya nchini Dubai, ndiyo iliingia mkataba na Mamlaka ya Usafirishaji Bandarini Zanzibar (ZMA), kama meli za kigeni.
Alisema kuwa baada ya serikali kubaini mchezo huo mchafu, ilichukua hatua ya kufuta usajili wa meli hizo mara moja, sambamba na uwakala wa kampuni hiyo ili usiendelee kusajili meli kwa mgongo wa Serikali ya Zanzibar.
“Wakati serikali ikijua suala hili limemalizika, Oktoba 19 mwaka huu, nilipokea barua kutoka Ubalozi wa Marekani, ikiituhumu Tanzania kushindwa kuzifutia usajili meli 36, mbali na hilo ikaongeza kuwa zimesajiliwa meli nyingine 17 ambazo zinadaiwa kufutiwa usajili wake nchini Tuvalu kitu ambacho hakina ukweli.
“Kutokana na tuhuma hizo, tumeziomba nchi marafiki ikiwemo Marekani kutusaidia kuchunguza tatizo hilo ili kubaini Philtex ni kina nani, baina yake na kampuni tanzu, mtandao pamoja na ofisi yenye jina hilo Dubai, na ina mkataba gani na uandikishaji wa meli kwa jina la Tanzania,” alisema.
Membe aliongeza kuwa, tuhuma zilizotolewa awamu ya pili kuhusu meli 17 ambazo zinasadikiwa kupeperusha bendera ya Tanzania tofauti na zilizofutiwa usajili, serikali itafuta kimaandishi mkataba wao na kampuni hiyo ili isifanye mawasiliano yoyote yanayohusu usajili wa meli.
“Hili la pili likithibitika wazi, mosi si kwamba tutazifuta usajili meli tena, bali tutaitoa kampuni hiyo moja kwa moja kuingia upya mkataba na nyingine ambayo itakubali masharti ya nchi na si vinginevyo,” alisisitiza.
Waziri Membe alisema serikali itakuwa makini kufanya utafiti pindi maombi ya wawekezaji yatakapowasilishwa eneo husika, halafu usajili utafuata baadaye ili kuondoa msigano baina yao.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment