Mahmoud Ahmad,Arusha
MFANYABIASHARA wa madini
aina ya Tanzanite mkoani Arusha,Ngerii Olerumwa anayekadiriwa kuwa na umri wa
zaidi ya miaka 40 amekutwa amekufa katika mazingira ya kutatanisha ndani ya
hoteli ya Premier Palace ambayo timu ya wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano
imeweka kambi hotelini hapo jijini Arusha.
Maiti ya mfanyabiashara
huyo iligundulika majira ya saa 3 ;30 asubuhi jana mara baada ya mhudumu wa
hoteli hiyo kugonga kwa muda mrefu mlango wa chumba alichokuwa amefikia marehemu
huyo bila mafanikio na kisha kubaini alikuwa amefariki dunia.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa
tukio hilo akiwemo meneja wa hoteli hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake
hadharani alisema kwamba marehemu huyo aliwasili hotelini hapo mnamo desemba 3
mwaka huu majira ya saa 1 ;00 jioni na kukodi chumba kimojawapo hotelini
hapo.
Meneja huyo akisimulia
tukio hilo alisema kwamba marehemu aliwasili akiwa peke yake hotelini hapo na
kubainisha kwamba yeye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kukodi chumba hotelini
hapo.
Hatahivyo,alidai kwamba
ilipotimu jana majira ya saa 3 ;30 asubuhi wakati mhudumu wa hoteli hiyo
akigonga mlango wa chumba alichofia marehemu kwa lengo la kufanya usafi mlango
huo haukuweza kufunguliwa kwa wakati hali iliyowapelekea kufanya juhudi za
kuufungua mlango huo kwa lazima.
Alisema kwamba baada ya
kufanikiwa kuufungua mlango huo walijaribu kumwamsha marehemu lakini hakuweza
kuamka hali iliyowapelekea kuliarifu jeshi la polisi kuhusiana na tukio
hilo.
Gazeti hili lilipofika
maeneo ya hoteli hiyo liliwashuhudia askari wa upepelezi kutoka jeshi la polisi
mkoani hapa wakichukua maelezo kwa baadhi ya watumishi wa hoteli hiyo wakiwemo
walinzi wa hoteli hiyo huku baadhi ya wabunge wanaounda timu ya wabunge wa bunge
la jamhuri wakitaharuki kutokana na tukio hilo.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti ndugu wa marehemu ambao walikusanyanya nje ya hoteli hiyo walisema
kwamba wameshtushwa na kifo cha ndugu yao na wanahisi kwamba aliuwawa katika
mazingira ya kutatanisha huku wakilitaka jeshi la polisi kubaini chanzo cha kifo
cha marehemu.
Akihojiwa na waandishi wa
habari kamanda mkuu wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas alikiri
kutokea kwa tukio hilo huku akisisitiza kwamba jeshi lake linachunguza kwa kina
kifo hicho.
Sabas,alisema kwamba mwili
wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ndani ya hospitali
ya mkoa ya Mt,Meru na atatoa taarifa kamili ya tukio hilo kuanzia leo mbele ya
waandishi wa habari.
Post a Comment