Na Rajab Ramah,
Nairobi
Wakati Kenya ilipoadhimisha miaka 49 ya uhuru
wiki iliyopita, raia waliokusanyika kwenye mitaa ya Nairobi kusherehekea
walisema taifa hilo halijafikia kiwango chake kamilifu cha maendeleo na liko
mbali sana kuweza kutimiza matarajio yao.
Wacheza ngoma za
kijadi wa Kenya wakicheza huku wakipita mbele ya jukwaa la rais katika Uwanja wa
Taifa wa Nyayo jijini Nairobi tarehe 12 Disemba wakati wa sherehe za Siku ya
Jamhuri (Simon Maina/AFP).
Rais Mwai Kibaki wa Kenya, ambaye aliongoza
sherehe za siku ya uhuru tarehe 12 Disemba, inayofahamika pia kama Siku ya
Jamhuri, alisema kwamba ndani ya kipindi chake cha miaka 10 madarakani, ameweka
misingi imara ya kuigeuza Kenya kuwa wa uchumi wa tabaka ya kati.
Katika hotuba yake kwenye Uwanja wa Taifa wa
Nyayo, Kibaki alisema nchi hiyo imeimarisha kiwango cha elimu, miundombinu,
maendeleo, afya, maji na usafi.
"Tulianzisha elimu ya msingi ya bure na ya
lazima. Programu hii imepata mafanikio makubwa, ambapo karibuni watoto wetu
milioni 10 wanafaidika nayo," alisema. "Tulishawishika kwamba kuimarisha
mitandao ya usafiri kwa njia za barabara, reli na angani, na pia utanuzi wa
sekta za nishati na mawasiliano, kutawezesha usafirishaji wa bidhaa na watu nchi
nzima na kwenye eneo letu."
Pamoja na hayo, Mary Wangari mwenye umri wa
miaka 50, mfanyabiashara wa mtaani kwenye soko la Muthurwa la Nairobi, alisema
miaka mingi baada ya Kenya kupata uhuru wake kutoka Uingereza, bado umasikini,
ujinga na maradhi yanaendelea kuitafuna nchi.
Hata kama kumekuwa na maendeleo fulani, alisema
mengi zaidi yangeliweza kufikiwa. "Bado tunakabiliwa na matatizo yale yale
ambayo tulidhamiria kuyashinda wakati wa kuzaliwa kwa nchi hii," aliiambia
Sabahi. "Kwangu hakuna kilichofikiwa kustahiki hongera zangu."
Wakati nchi ikiandama kuelekea maadhimisho ya
miaka 50, Wangari alisema serikali yapaswa kujenga masoko zaidi na kuunda
programu za kuiinua uchumi, kama vile mikopo na misaada ya fedha kwa biashara
mpya.
Alisema kutoa mikopo kwa biashara zinazoanza
sasa kutawahamasisha vijana kuwa wajasiriamali. "Tabia iliyopo ni kwamba vijana
wanakwenda skuli na baada ya kumaliza masomo yao wanangojea kazi za kuajiriwa na
serikali kwa sababu wamezoeshwa hivyo," alisema. "Wale wanaotaka kujiajiri
wenyewe na kuanzisha biashara zao, wanakosa mtaji wa kuanzia. Utamaduni wa
kusubiri ajira unapaswa kubadilika sasa. Vijana wanapaswa kushajiishwa kuunda
ajira zao wenyewe."
Mwanaharakati wa haki za kiraia Fredrick
Odhiambo alisema bei za juu za vyakula na kupanda kwa gharama za maisha ni
changamoto zinazolikabili taifa, na lazima zishughulikiwe vyema ili kuimarisha
hali za maisha za watu.
"Pengo baina ya masikini na matajiri
limeongezeka," Odhiambo aliiambia Sabahi. "Umasikini umetufanya kuwategemea
wengine. Huu si uhuru tunaouhitaji. Tunataka ushughulikiwe kupitia uundaji wa
nafasi zaidi za ajira."
Alisema kungelikuwa na usawa kwenye utumiaji wa
rasilimali za taifa na uundaji wa ajira nchi nzima, ili watu kwenye maeneo wawe
na fursa za kuyaboresha maisha yao.
Ndolo Benji, mwanaharakati na mwanachama wa
Baraza la Katiba na Elimu, alisema katiba mpya na mageuzi yanayohusishwa nayo
yameanza kuiweka nchi kwenye zama za uwajibikaji, uwazi na utawala bora.
Alisema kuyalinda mafanikio yaliyopatikana na
kujenga mustakabali wa maendeleo yanayoahidiwa na mageuzi ya kikatiba, taifa
lazima lishughulikie ukosefu wa usalama nchini Kenya. "Kwa maendeleo kupatikana,
tunahitajika kupigania amani, hasa wakati wa uchaguzi mkuu wa hapo tarehe 4
Machi," Benji aliiambia Sabahi. "Hili linaweza kufanikiwa ikiwa tutapambana na
mzuka wa ukabila na siasa za kugawana ambazo huiingiza nchi kwenye machafuko
kila mwaka wa uchaguzi."
Hatua muhimu lazima zichukuliwe dhidi ya
ufisadi wa serikali, alisema, ambao umepelekea kupotea kwa fedha za walipakodi
ambazo zingetumiwa katika miradi ya maendeleo.
Chanzo: sabahionline.com
Chanzo: sabahionline.com
Post a Comment