Baada ya mauaji ya kinyama ya watu 27 wakiwemo watoto 20 wenye umri wa kati ya miaka 6 na 7 katika jimbo la Connecticut . Rais wa Marekani Barack Obama, amesema kuna haja ya kuweka kando siasa ili kuchukuwa kile alichosema “hatua madhubuti za kukomesha maafa zaidi kama hayo.” Lakini Obama hakwenda mbali zaidi kutowa wito wa kutaka kuwepo kwa sheria kali zaidi za kudhibiti silaha.
Mauaji hayo yameamsha upya mjadala juu ya udhibiti wa silaha katika nchi ambapo utamaduni wa kumiliki silaha umeshamiri na kuna ushawishi mkuwa wa kupigia debe umilikaji wa silaha, jambo ambalo limewakatisha tamaa wanasiasa wengi kufanya jitihada zozote zile kubwa za kushughulikia tatizo la kumiliki silaha kwa urahisi.
Meya wa mji wa New York Michael Bloomberg ambaye anaongoza muungano wa mameya katika suala la sera ya silaha amesema hapo Ijumaa kwamba Rais Obama wa chama cha Demokrat anapaswa kuchukuwa hatua licha ya upinzani kutoka chama cha Republikan ambacho kinalidhibiti Baraza la Wawakilishi la bunge la Marekani. Bloomberg amesema katika taarifa ” Tumeyasikia madoido ya kusema kabla.Hatukushuhudia uongozi sio kutoka Ikulu wala kutoka bungeni. Jambo hilo halina budi kukomeshwa leo hii.”
Maafisa wa polisi waliwakuta watoto 18 wenye umri kati ya miaka 6-7 na watu wazima saba akiwemo muuaji wakiwa tayari wamekufa huko shuleni na watoto wawili walifia hospitali kutokana na kujeruhiwa vibaya. Obama amesema wengi waliokufa walikuwa ni watoto wadogo ambao walikuwa na maisha marefu yakiwasubiri na kwamba kila mzazi nchini Marekani moyo wake umeemewa na huzuni.
Obama ilibidi ajitahidi kudhibiti hisia zake na kufuta machozi yaliokuwa yakimtoka wakati alipoliambia taifa kupitia televisheni akiwa Ikulu hapo Ijumaa kwamba ” Nyoyo zetu zimevunjika.” Zaidi ya watu 1,000 hapo Ijumaa wamekesha kucha katika Kanisa la Kikatoliki la St. Rose lilioko maili chache kutoka eneo la mauaji kufanya ibada ya maombi.