WIZARA ya Mambo ya Ndani ya
Nchi, imeifunga kambi ya Mtabila na kuwaondoa wakimbizi wote kutoka Burundi
baada ya kugoma kufanya hivyo kwa hiari.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya
maridhiano ya pande tatu yaliyofanyika Oktoba 8,mwaka huu huko Geneva ambapo
Serikali ya Tanzania, Burundi na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR)
waliamua kuwaondoa wakimbizi hao ili kuepusha machafuko,ghasia na vurugu ambazo
zingeweza kutokea.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam leo, Waziri mwenye dhamana, Emanuel Nchimbi, alisema
kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada kuonekana raia hao hawaonyeshi nia yeyote ya
kurudi nchini kwao kwa hiari hasa baada ya machafuko kuisha.
Nchimbi alisema katika
machafuko ya mwaka 1993 nchini Burundi kufuatia kuuawa kwa Rais Melkior Ndadaya,
Tanzania ilipokea wakimbizi 550,000 hadi kufikia mwaka 2002 lakini wengine
waliondoka baada ya machafuko kuisha na kubaki 36,000.
Alisema kuwa baada ya mwaka
huu kutangazwa kwa zoezi la kurudi kwa hiari ni wakimbizi 1305 ndio waliokubali
hali iliyosababisha serikali kuamua kuwavua hadhi ya ukimbizi waliosalia kwa
mujibu wa sheria ya wakimbizi ya mwaka 1998.
Alisema kuwa baada ya zoezi
hilo kushindikana waliamua kuwarudisha kwao kwa kutumia urejeaji wa kusimamiwa
na kubaki 2400 katika kambi ya Nyarugusu ambao wanasababu za msingi kuendelea
kubaki nchini wakisubiri suluhisho lingine la kudumu.
Aidha alisema kuwa mpaka sasa
makambi yote tisa ya wakimbizi wa nchi hiyo yamefungwa na kueleza kuwa endapo
kuna wakimbizi waliotoroka na kujichanganya uraiani watakamatwa na sheria
itachukua mkondo wake na watahukumiwa kwa sheria ya mwaka 1998.
Nchimbi alisema kuwa baada ya
kuifunga, kambi hiyo itafanyiwa ukarabati na sehemu ya majengo yake yatatumiwa
na wananchi pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).
Post a Comment