Baada ya baadhi ya
vyombo vya habari kuandika tarehe 3 Desemba 2012 kauli yangu kuwa usafiri wa
treni katika jiji la Dar es salaam kwamba kwa sasa unaingiza hasara ya wastani
wa shilingi milioni 10 kwa siku tano, wanahabari mbalimbali kupitia simu na
baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii wametaka nitoe ufafanuzi kuhusu
madai hayo.
Ieleweke kwamba nilitoa
kauli hiyo wakati nikijibu swali la mwananchi kwenye mkutano wa hadhara tarehe 1
Desemba 2012 katika mtaa wa Saranga Jimboni Ubungo ambaye alihoji kuhusu ufanisi
wa usafiri wa treni jijini Dar es salaam na hatua nyingine ambazo Serikali
inapaswa kuchukua kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es salaam; hivyo
katika hotuba yangu nilizungumza masuala mengi na kueleza mapendekezo niliyotoa
kwa nyakati mbalimbali ya kuboresha mfumo mzima wa usafiri.
Nilieleza kwamba naunga
mkono usafiri wa treni kuwepo jijini Dar es salaam na kwamba katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2010 ilikuwa ni moja ya masuala niliyoahidi wananchi kwamba
nitayafuatilia, na wakati huo wa kampeni wapo walionipinga ikiwemo kwa
kuzungumza katika mikutano yao ya kampeni na hata katika radio.
Kazi ya mbunge ni
kuwawakilisha wananchi katika kuishauri, kuisimamia serikali na kutunga sheria
hivyo kwa msingi huo mara baada ya kuchaguliwa nilihoji bungeni kutaka hatua za
haraka za kuanzishwa kwa usafiri huo na hatimaye Wizara ya Uchukuzi (wakati huo
ikiwa chini ya Waziri Omar Nundu) mwaka 2011 ikajibu kuwa itatumia sehemu ya
fedha kwenye bajeti kuanza matengenezo kwa ajili ya usafiri huo
kuanza.
Kwa hiyo nilisisitiza
kwenye mkutano wa hadhara usafiri huu kuanza mwaka huu 2012 ni matokeo ya kazi
ambayo ilishaanza mwaka 2011, na nikawaeleza wananchi kwamba natambua mchango wa
Waziri wa sasa Dk. Harrison Mwakyembe katika kuongeza msukumo; hata hivyo
niliwaeleza wananchi kwamba kama mbunge bado siridhiki na maandalizi
yaliyofanyika na kwamba iwapo mapendekezo yangezingatiwa kwa wakati usafiri huo
ungekuwa na mfumo na utaratibu bora kuliko ilivyo sasa.
Hivyo, nikaeleza kwamba
nitaendelea kuwawakilisha wananchi katika kuishauri, kuisimamia serikali na
kutunga sheria ili kasoro zilizopo za miundombinu na mfumo wa uendeshaji ziweze
kuondolewa na nikatoa mfano kwamba usafiri huo kwa sasa unaingiza hasara ya
wastani wa shilingi milioni 10 kwa siku tano hali ambayo inaweza kurekebishwa
ili kuhakikisha kwamba usafiri huo unakuwa endelevu badala ya kukwama baadaye
kutoka na mzigo wa hasara.
Nitoe ufafanuzi wa
nyongeza kwamba natambua kuwa uchambuzi wa gharama (wakati mwingine ikiwa ni
hasara) na faida (cost benefit analysis) hutumia vigezo tofauti kisiasa,
kiuchumi na kijamii na mtazamo wangu wa muda mrefu ambao unaweza kuthibitishwa
kwenye michango yangu bungeni na kauli zangu nje ya bunge, usafiri wa umma (mass
transport) unapaswa kuwa huduma zaidi ya biashara hivyo suala la kupata hasara
ya kifedha wakati mwingine linaweza lisiwe na uzito likilinganishwa na faida ya
kupunguza kero kwa wananchi.
Pia, natambua kwamba
uwekezaji unaweza ukaanza kwa hasara wakati huduma au biashara haijafikia
kiwango cha kutosha cha watumiaji, wateja au uzalishaji wa kuweza kurudisha
gharama na pengine kupata faida (loss before breakeven point). Hata hivyo, kwa
hasara hii ya wastani wa milioni 10 kila baada ya siku tano, hali ni tofauti kwa
kuwa chanzo chake sio vigezo hivyo hapo juu vya hasara isiyoepukika (ambayo
inaweza kufidiwa kwa serikali kutoa ruzuku kwa sababu za kijamii) wala sio kwa
sababu ya kuwa na idadi ndogo ya watumiaji; bali ni kutokana na kutozingatiwa
kwa baadhi ya masuala ya msingi katika maandalizi kuanzia kwenye ukarabati wa
vichwa cha treni, mabehewa na miundombinu ya reli hali ambayo ni wajibu wa
mbunge kuiweka wazi na kutaka serikali irekebishe ili huduma iweze
kudumu.
Ikumbukwe kwamba kwamba
njia ya treni ya kutoka Ubungo mpaka Stesheni ilikuwa inatumika miaka ya zamani
na kampuni ya saruji, kampuni ya makasha ya chuma na kampuni zingine chache
ikiwa ni njia binafsi (siding) na toka wakati huo iliacha kutumiwa. Nilieleza
tangu mwaka 2010 na 2011 kwamba inapaswa kwanza kuimarishwa ili treni iweze
kwenda mwendo kasi zaidi na kuongeza idadi ya safari na hivyo kubeba abiria
wengi zaidi na kuondoa hasara kutokana na ongezeko la mapato (economies of
scale). Hatua hii ingeenda sambamba na kuweka reli zenye uzito mkubwa zaidi
ambazo zingeweza kubeba vichwa vya treni vyenye nguvu zaidi na mabehewa ya ziada
ambayo ni maalum kwa usafiri wa mjini, haya ni masuala ambayo utekelezaji wake
ungeanza kwa wakati kama nilivyopendekeza usafiri wa treni ungezinduliwa mapema
bila ya kuwa na hasara yoyote. Hali hii inaweza kurekebishwa kwa Wizara ya
Uchukuzi kuingilia kati kwa kushirikiana na TRL na TAZARA na kufanya uwekezaji
unaostahili.
Badala ya kukwepa
mjadala huu kuhusu hasara inayopatikana, ni muhimu mjadala ukaendelea ili
wananchi wakafahamu ukweli na hatimaye Serikali ikawajibika kuingiza katika
bajeti kuagiza treni maalum za usafiri mjini (Diesel Multiple Unit-DMU au Gas
Unit-GU) ziweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na kwamba gharama ndogo; iwapo
Serikali haitaufanyia kazi ushauri huu ieleweke kwamba italazimika kutoa ruzuku
kwa TRL na TAZARA ili kufidia hasara.
Aidha, changamoto
zinazoendelea kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi toka vituo vya treni
zinadhihirisha haja ya mapendekezo niliyotoa mwaka 2010 na 2011 ya Serikali
kuunganisha mifumo ya usafiri wa umma (mass transit) ya reli, mabasi ya kawaida
na mabasi ya haraka ili kuweza kuingiliana na kupunguza gharama za usafiri wa
umma.
Ili wazo hilo liweze
kuratibiwa vizuri, ni muhimu kuwa na chombo kimoja cha usafiri Dar es salaam
mathalani Mamlaka ya Usafiri Dar e salaam (MUDA) badala ya utaratibu wa sasa
ambapo mabasi ya haraka yako chini ya DART, mabasi ya kawaida yako chini ya UDA
(ambayo mpaka sasa iko katika utata na hali tete) huku treni ziko chini ya
TAZARA na TRL/RAHCO na wazo la treni za chini kwa chini nalo likija
litaanzishiwa chombo chake; hali ambayo inaongeza gharama za uendeshaji na
matatizo ya mifumo kutokuingiliana ipasavyo kuanzia wakati wa uwekezaji na
uwekaji wa miundombinu.
Bado, hatua nyingi za
ziada zinahitajika zenye kugusa Wizara zaidi ya moja, mathalani Wizara ya Ujenzi
na Halmashauri za Manispaa zina wajibu wa barabara za pembezoni za kupunguza
msongamano, ndio maana hata baada ya kuanza kwa usafiri wa reli, matatizo ya
foleni yanaendelea tofauti na kauli zilizokuwa zikitolewa awali. Hivyo, kwa
nafasi yangu ya mwakilishi wa wananchi katika kuishauri na kuisimamia serikali
na kutunga sheria nitaendelea kutimiza wajibu huo ndani na nje ya Bunge kwa
manufaa ya wananchi wa Jimbo la Ubungo na Taifa kwa ujumla.
Wenu katika maendeleo ya
nchi na wananchi,
John Mnyika
(Mb)
05/12/2012
Post a Comment