Na Charles Charles
“Wakati mjadala wa nani anafaa kuwa Rais wa Serikali ya
Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unashika kasi kila kona
ndani na nje ya nchi, jina la Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Dk. Willibrod Slaa limeng’ara”, liliandika gazeti moja la kila siku
nchini, Jumatano wiki hii na kuendelea:
“…Kwa mujibu wa kura za maoni zilizoendeshwa na mtandao
maarufu duniani wa Jamii Forums kwa kuuliza: “Nani ungependa agombee urais mwaka
2015 kwa tiketi ya Chadema na CCM”, majina manne yalipambanishwa, mawili kutoka
CCM na mawili Chadema”.
Mchanganuo wa kura hizo ambazo hata hivyo hazihusiani
chochote na uchaguzi wowote wa rais ila kama za
maoni ya ndani ya vyama hivyo vyenyewe, zoezi ambalo pia lilijaa ushabiki
binafsi kwa watu waliohusishwa zilimpa ‘ushindi’ Dk. Slaa dhidi ya Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ingawa mchezo huo si lolote wala chochote kisiasa
kwa yeyote kati yao.
“Jumla ya wapiga kura 1,188 walishiriki kuwapigia kura
wagombea wa Chadema”, inasema habari hiyo na kuongeza: “Dk. Slaa alipigiwa kura
1,007, sawa na asilimia 84.76 wakati Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini aliibuka
na kura 181, sawa na asilimia 15”.
Mbali na hao, wengine ‘waliopambanishwa’ lakini kutoka
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli mkoani
Arusha, Edward Lowassa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Benard Membe.
Katika hadithi hiyo ya kitoto, jumla ya kura
walizopigiwa zimetajwa kuwa 375 na Lowassa kupewa 164 zilizotajwa kuwa ni
asilimia 43.73, kisha Membe akaishia 67 ambazo ni sawa na asilimia 17.87
tu.
“Matokeo ya jumla yanaonyesha kuwa Dk. Slaa aliibuka na
ushindi mkubwa wa kura 1,007 kwa kupigiwa kura nyingi zaidi kuliko majina ya
washiriki wengine waliopendekezwa na kuingia katika mnyukano huo. Mshindi wa
pili ni Zitto mwenye kura 181, wa tatu Lowassa mwenye kura 164 na Membe anashika
nafasi ya nne kwa kura 67”, inabainishwa.
Nimeanza makala yangu kwa kusema hii ni hadithi ya
kuchekesha kutokana na malengo ya makusudi ambayo ni
mawili.
Ni juhudi za makusudi zilizopangwa na kutekelezwa na
kikosi cha wapambe wanaotarajia mkakati wao utasaidia kumjenga katika chama
chake, na pili wanaamini kuwa njia hiyohiyo itamaliza kabisa ndoto zote
alizonazo Zitto na pia kumsambaratisha hata mwenyewe
kisiasa.
Wapambe hao wa padri huyo wa zamani wanadhani kwa
kufanya hivyo atapata umaarufu nje na ndani ya chama chake, jambo ambalo mtu
yeyote asiyekuwa na mtindio wa ubongo haliwezi kumuingia kichwani ila kama ni
mtoto wa chekechea.
Ni mchezo uliotengenezwa kipuuzi kwa ajili ya watu
wapuuzi wanaoweza wakaaminishwa upuuzi na siyo wenye akili timamu hata
kama ni washamba wa kufikiri. Hakuna anayeweza
kurubuniwa kwa ujinga uliotengenezwa maalum ili kumfariji babu huyo wa watu. Ni
juhudi zinazofanywa pia ili kumfariji baada ya kusambaratishwa vibaya katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kutamka kwamba hayatambui
matokeo.
Ni juhudi zinazofanywa kwa makusudi ili kumpunguzia
hasira ambapo alifikia mpaka hatua ya kutishia kuwa Tanzania isingeweza
kutawalika “mpaka kieleweke”, lakini pia ni harakati za kutaka kumfariji kwa
sababu bado ‘amechanganyikiwa’ kichwani, halafu wapambe wake wanafahamu kwamba
uwezo wake wa kutathmini au kuchanganua mambo ni mdogo sana.
Ndiyo maana kwa mfano huwezi kuzichanganya kura za urais
wa Madagascar na Cameron au
za Kenya na Msumbiji. Haiwezekani kura
za maoni za kutafuta mgombea urais, ubunge ama udiwani za ndani ya CCM
zichanganywe na kura kama hizo za Chadema kwa
sababu hakuna uhusiano wowote uliopo kati yake.
Gazeti hilo lenyewe
limeeleza kuwa Dk. Slaa alipambanishwa na Zitto katika chama chao, halafu
Lowassa naye alikutanishwa na Membe kama wana
CCM. Katika hali hiyo na hata vinginevyo, haiwezekani kuja kuyachanganya pamoja
matokeo ya kura zao maana hayana uhusiano wowote na katika hali
zote.
Mbali na kutaka kumdanganya kwa sababu wanafahamu kuwa
uwezo wake wa kuchanganua mambo ni mdogo, wapo waliolenga kumtisha Zitto kwa
imani kwamba atahofia kushindwa katika mbio hizo na kuamua kuachana
nazo.
Walilenga kumtisha kwamba endapo ameungwa mkono na watu
181 tu kati ya 1,188 walioshiriki zoezi hilo huku Dk. Slaa akikubaliwa na 1,007
katika hesabu hiyo, mwaka 2015 anaotaka kugombea urais ataishia kuaibika, hivyo
ili asitumbukie kwenye aibu hiyo inabidi apime mwenyewe, atathmini na
kujitoa.
Ndivyo pia walivyolenga dhidi ya CCM kutaka ionekane
kwamba imechuja huku Chadema yao ikimeremeta katika kipindi hiki cha mpito
kuelekea mwaka 2015. Pamoja na hayo na hata vinginevyo, hesabu inayochezwa ni
kama ngoma ya kitoto ambayo siku zote
haikeshi.
Kama nilivyobainisha tokea mapema huo ni ujinga wa
kufikiri kwa sababu hakuna asiyejua kwamba katika uchangiaji unaofanyika katika
mitandao kama Jamii Forums, mtu mmoja anaweza
kujiita majina hata 20, 50, 80 au zaidi yake. Inategemea na jinsi anavyopata
nafasi ya kuchangia chochote, na pia kuna wengine wanaodhani kuwa njia hiyo ni
bira zaidi kisiasa kama Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa Taifa wa Chadema, John Mnyika.
Kwa mfano hata Dk. Slaa mwenyewe pia anaweza kujiita
Athumani, Saidi, Yohana, Richie, Danford, Khadija, Hilda, Rhoda, Fatuma, Lucy na
kadhalika. Anaweza kujipachika kila aina ya majina ili hatimaye ajipigie kura,
kazi amabyo pia inaweza ikafanywa na wapambe wake ama kwa makubaliano naye
maalum au kwa kujipendekeza wenyewe.
Ndiyo maana tunadanganywa pia kuwa eti mtandao huo ni
“maarufu duniani” kote wakati hakuna ukweli. Hauna umaarufu hata Afrika
Mashariki pekee mbali ya Afrika Mashariki na Kati, Afrika iliyopo kusini mwa
Jangwa la Sahara ama Afrika peke
yake.
Hausomwi hata na watu 3,000 peke yao angalau kwa siku moja
ama wiki nzima isipokuwa kikundi ambacho kwa kawaida ni kilekile, tena
kilichokusanya kwa kiwango kikubwa zaidi wanachama au wafuasi wa
Chadema.
Ni ulimbukeni unaofanana kama ulevi wa pombe ambao kwa
mfano wanywaji wa bia aina ya Tusker, Ndovu au Serengeti huwa ni walewale kwa
kila siku na mtu mmoja anaweza kumaliza chupa tano, 10 au hata sanduku moja peke
yake na kuonekane kuwa ni wengi.
Mtu mmoja ama pengine na mpenzi wake wanaweza
wakajifungia mahali wakaanza kuagiza bia mojamoja, mbili au tatu wakishinda
mpaka jioni wanaweza kumaliza hata sanduku zima na kadhalika. Hapo huwezi kusema
kuwa eti wanywaji wa pombe wanaongezeka kwa kasi ama kila kunapokucha wakati
ukweli ni walewale.
Hivyo ndivyo inavyokuwa pia katika mitandao yote ya
kijamii ambako mtu mmoja anaweza ‘akaingia’ hata kutwa nzima na hasa anapokuwa
na kazi ndogo tu ya kuandika majina kama “DK.
SLAA, ZITTO, LOWASSA” au “MEMBE”.
Anaweza akafanya hivyo kuanzia asubuhi mpaka usiku wa
manane ili ‘kumbeba’ mtu wake au kwa kujipigia kura mwenyewe akibadili majina
kuanzia Mayasa, Teophil, Mkunza, Petro, Esther, Augusta, Madaraka na kadhalika
ili isionekane kuwa ni yuleyule isipokuwa jopo la watu.
Huo ndio mchezo uliofanyika ili kumbeba Dk. Slaa kwa
imani kuwa atashinda urais mwaka 2015 na kwenda Ikulu kwa daraja la Chadema
yake.
Mtu yeyote anayebisha haya aende akazunguke katika mitaa
yote mijini na vijijini, kisha aulize kuwa ni watu wangapi ‘wanaingia’ katika
mitandao kama ya twitter, Jamii Forums, facebook na mengineyo ili
aone.
Hata intaneti wanakoshinda hadi watu wasiojua namna gani
ya kutumia twitter au facebook nako utakuta wanaokwenda hawazidi hata 40 kwa
siku moja. Kule wanakokwenda wengi ni zile zinazokuwa karibu zaidi na vyuo
vikuu.
Zinapata watu wengi ambao siku zote huwa wanafunzi wa
shahada mbalimbali kwa ajili ya kujitafutia ‘material’, na pili ni zile
zinazokuwa jirani na ofisi za vilabu vya waandishi wa habari hususan
mikoani.
Wapiga kura walio wengi mijini na vijijini hawajawahi
hata kusikia neno “intaneti” na hata mitandao iwe ya twitter, facebook, jamii
forums wala mwingine wowote. Hawajui chochote kuhusu mambo hayo yote na ndiyo
maana ni ajabu kuitegemea kwa namna yoyote ile kupata ushindi wa urais maana
haihusiki nao.
Haiwezi kumfanya Dk. Slaa kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania iwe
mwaka 2015, 2020, 2025 wala mbele ya safari isipokuwa kama ni serikali ya
maigizo kama michezo ya fukuto, radi, ngweso na
kadhalika.
Katika hali hiyo na hata vinginevyo, wote walioshiriki
‘kumrusha roho’ babu huyo wa watu sina ugomvi nao wowote ila ninaomba
wauzingatie ushauri wangu huu: waache kumpachika urais wala ushindi wa kupitia
mtandao huo wa Jamii Forums kwani hautakuwepo daima.
Waache kabisa kufanya hivyo kwa sababu wanampandikizia
imani na ndoto za alinacha. Wanamtafutia maradhi yakiwemo sugu pindi akigombea
tena nafasi hiyo na kushindwa maana hataamini masikioni wala
machoni.
Mungu Ibariki Tanzania!
Post a Comment