Waziri wa
habari utamaduni utalii na michezo Said Ali Mbarou akizungumza na waandishi wa
habari juu ya kulifanyia matengenezo jengo la Beit El Ajab lililoanguka moja ya
sehemu zake.
Waziri wa Habari
Utamaduni Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk amesema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba maharibiko ya kuanguka sehemu
ya jengo la Makumbusho ya Taifa Beit El Ajab yanarekebishwa na matengenezo ya
jumla ya jengo hilo na majengo yote ya kihistoria yanasimamiwa
ipasavyo.
Akizungumza na waandishi
wa habari katika makumbusho ya Mnazimmoja, Waziri Mbarouk amesema kutokana na
heshima na hadhi ya jengo la Beit El Ajab kwa historia ya Zanzibar, kuanguka kwa
jengo hilo kumeathiri shughuli za utalii kwani ni miongoni mwa vivutio vikuu vya
Utalii ZANZIBAR.
“Asilimia 70 ya wageni
wanaotembelea sehemu za kihistoria huwa wanafika makumbusho ya Beit El Ajab’’,
alisema Waziri Said Ali Mbarouk.
Amesema uamuzi wa
kuyahifadhi maeneo ya Historia ikiwemo jengo la Beit El Ajab utaendelea kupewa
umuhimu mkubwa kwani ni sehemu ya urithi wa Utamaduni wa Zanzibar na yanahitaji
kudumu kwa miaka mingi zaidi.
“Jengo hili lililojengwa
mwaka 1883 na Mfalme Barghash bin Said ni moja kati ya majengo yenye hadhi kubwa
kihistoria, kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa Zanzibar” alisisitiza Waziri
Mbarouk.
Amesema umaarufu wa
jengo la Beit El Ajab unatokana na kuwa ni la kwanza Zanzibar kuwekewa huduma za
kijamii kama vile umeme, simu, lifti na maji ya mfereji kabla ya huduma hizo
hazijaanzishwa kwenye nchi nyingi za Afrika Mashariki.
Ameongeza kuwa kutokana
na maharibiko yaliyotokea Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe
inachukua hatua ya kuiarifu UNESCO kuhusu tukio hilo na kuomba msaada wa
kitaalamu na fedha kulinusuru.
Aidha amesema Idara ya
Makumbusho na Mambo ya kale inafanya mawasiliano na watalaalamu wa majengo ya
kale ili kupata tathmini ya hali ya jengo hilo na Kasri ya Kifalme na aina ya
matengenezo ya kudumu na gharama zinazohitajika.
Jengo la Makumbusho kuu
ya Jumba la Ajab lilianguka usiku wa Jumamosi iliyopita wakati likiendelea
kufanyiwa matengenezo na MACEMP na limewahi kutumika kwa sherehe na shughuli za
utawala wakati wa ufalme, Makumbusho ya Chama cha ASP, Chuo cha Itikadi ya Chama
na kuanzia mwaka 2002 likapewa hadhi ya kuwa makumbusho inayohusu Utamaduni wa
Mswahili na Historia ya Zanzibar.
IMETOLEWA NA
IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR


Post a Comment