Timu ya Azam FC kesho Jumanne itamalizia ziara yake ya mechi za kirafiki jijini Nairobi kwa kucheza dhidi ya K.C.B kwenye Uwanja wa City.
Azam FC iko jijini hapa kwa ziara ya maandalizi kwa ajili ya ligi kuu na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, imecheza michezo miwili, imefungwa 2-1 na AFC Leopards na ikashinda mchezo mmoja 1-0 SOFAPAKA.
Ziara hiyo ya siku saba inamalizika leo kwa mchezo huo ambapo kikosi hicho kitarejea jijini Dar es Salaam, siku ya Jumatano tayari kwa mechi za ligi kuu.
Katika ziara hiyo hadi jana jioni wachezaji wote walioko safarini wamecheza katika michezo hiyo miwili akiwepo kipa namba mbili Aishi Salum.
Akizungumzia mchezo wake wa mwisho, kocha Stewart alisema wachezaji wote wako safi kwa mchezo huo kwa kuwa hakuna majeruhi yoyote katika michezo hiyo.
Alisema wakimaliza mashindano hayo watakuwa wamejiimarisha vya kutosha kwa ligi kuu, wachezaji watakuwa imara na kurekebisha makosa yao.
“Mechi na KCB tutacheza tukiwa safi, tumepumzika siku moja, wachezaji wamepata mapumziko, itakuwa mechi nzuri” alisema Stewart.
Mchezo huo utachezwa kwenye kiwanja cha City ambacho ni cha nyasi bandia sawa na kile cha Azam Complex Chamazi.