SEKRETARIETI ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imejichimbia mkoani Kilimanjaro kwa ajili
ya kutengeneza mpango mkakati wa namna ya kuendesha shughuli zao kwa mwaka
huu.
Itakumbuka kuwa moja ya
maazimio ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni
mwa mwaka jana, iliazimiwa kuwa mwaka 2013 ni wa kutumia nguvu ya umma
kuishinikiza serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kuwajibika kwa
wananachi.
Akizungumza na Tanzania
Daima jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema mpango huo ni
sehemu ya mpango mkubwa wa miaka mitano wa chama hicho ulioanza mwaka 2011 na
kuendelea hadi 2016.
Alifafanua kuwa kulikuwa
na minon’gono kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya wajumbe
wakiwamo wabunge wa chama hicho, hawakualikwa kwenye kikao hicho, jambo alilodai
kuwa ni uzushi.
Dk. Slaa alisema kuwa
wajumbe wasiotokana na sekretarieti walioalikwa ni wale wenye majukumu maalumu
ndani ya chama.
“Sisi tuna wabunge 49 na
katika kikao hiki wabunge waliohudhuria ni sita, ukimuacha Mwenyekiti wetu,
Freeman Mbowe na hawa wabunge wameingia kwa kofia za nafasi zao katika chama,”
alifafanua.
Katibu Mkuu huyo
aliongeza kuwa mkakati wanaoupanga utafika katika ngazi nyingine za chama hicho
kwa uamuzi kabla ya kutekelezwa.
Kwa sasa CHADEMA
imejizatiti kwa kile inachokieleza kuwa ni mikakati maalumu ya kuchukua dola
kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015.
Katika kudhibiti hilo,
chama kimewataka wanachama wake kuacha kupoteza muda kwa kulumbana juu ya nani
awe mgombea urais na badala yake utatengenezwa utaratibu maalumu wa wanachama
kutangaza nia.
Hivi karibuni Mwenyekiti
wa chama hicho, Mbowe, aliweka bayana kuwa hana mpango wa kuwania wadhifa huo wa
urais na badala yake atakuwa na jukumu la kuwafunda wagombea makini
watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi zote za uongozi wa vijiji na
mitaa, udiwani, ubunge na urais.
NA TANZANIA
DAIMA
Post a Comment