Kwenye jamii yetu kuna
mjadala wa gesi. Kila ninapoufuatilia mjadala huu naiona hulka ya baadhi ya
viongozi wetu inavyodhihiri; kuwa wanachanganya siasa na gesi. Kuna hatari
ninayoiona ya nchi kulipuka. Ni wanasiasa walioelekeza mjadala wa gesi ubebe
sura ya kimaeneo na kikabila. Na nahofia si muda mrefu tusasikia dini nayo
ikichanganywa na gesi. Hapa kuna tatizo kubwa. Kinachokosekana ni ufahamu wa
jambo zima kuhusu rasilimali zetu za nchi na nani wa
kumnufaisha.
Tumefika mahali
Watanzania tumekuwa kama wale watu wanaogombania bakuli za supu kwa ng’ombe
ambaye hajachinjwa, na pengine hajatolewa hata zizini. Fikiri kama ng’ombe
atakata kamba au kutoroka zizini.
Tumefika mahali baadhi
ya wanasiasa kwa kauli zao, wanawafanya Watanzania waamini kuwa neema ya gesi
kwao itapatikana kesho au kesho kutwa. Si kweli. Kimsingi manufaa ya gesi hii,
kama itasimamiwa vema, ni kwa watoto na wajukuu zetu. Hii si gesi yetu, ni ya
vizazi vijavyo. Ujinga ni kutaka kuitumia gesi ya vizazi vijavyo kama karata
kwenye siasa zetu za sasa za reja reja- retail politics. Ndio hii hatari
ninayoisema ya kuchanganya gesi na siasa.
Ni dhahiri, kuwa muda
wetu wa kuishi humu duniani ni mfupi sana. Tofauti na wanyama, binadamu katika
maisha yetu ya duniani, tuna kawaida ya kufikiria hiba ya kuacha nyuma yetu, kwa
familia zetu na kwa jamii tunayoishi.
Fikiri mtoto uliyemzaa
akikuuliza; “ Mama/ Baba, ukiondoka hapa duniani ungependa tukukumbuke kwa
yepi?
Hilo ni swali gumu kwa
yeyote anayeulizwa. Majibu ya swali hili yanatusaidia kuelewa umakini wa
anayejibu. Swali hili linahusu hiba ya mtu anayoiacha nyuma yake. Hiba ambayo
angependa akumbukwe kwa kuhusishwa nayo, ni urithi. Wazungu wanaita
“Legacy”.
Huko nyuma nimepata
kutoa mifano kadhaa ya viongozi walioacha hiba nyuma yao, hiba njema na mbaya;
kule Burkina Faso alitokea kiongozi kijana na mwanamapinduzi. Aliacha hiba njema
ya kuenziwa ndani ya nchi yake, Afrika na duniani, aliitwa Kapteni Thomas
Sankara.
Mwanamapinduzi huyu
alikuja kuawa kwa kupigwa risasi na wapinga mapinduzi na maendeleo ya Burkina
Faso. Sankara alipata kukaririwa akisema;
“Ningependa kuacha nyuma
yangu, imani ya kuwa, kama tunaimarisha kiwango fulani cha uangalifu na
oganaizesheni, basi, tunastahili ushindi. Kamwe huwezi kuleta mabadiliko ya
kimsingi bila ya kuwa na kiwango fulani cha uwendawazimu.
Hali hii inatokana na
kutoshinikizwa na taratibu zilizozoeleka, kuwa na ujasiri wa
kuzipa mgongo kanuni za
kizamani, ujasiri wa kuanzisha mustakabali.
Ni wendawazimu wa jana
waliotuwezesha kuyafanya tuyafanyao leo.
Ninataka kuwa mmoja wa
wendawazimu hao.” ( Hayati, Kapteni Thomas Sankara)
Ndugu
zangu,
Mara kadhaa nimemnukuu
Mwandishi mahiri Frantz Fanon aliyepata
kusema; ”Kila kizazi
kina jukumu lake. Kina lazima ya kutoka kwenye hali ya ugiza na kulitafuta
jukumu lake; kulikamilisha au kulisaliti”-
(Frantz Fanon.) Ni sisi
wenyewe ndio wenye kuandika historia yetu kwa kupitia
matendo yetu, na zaidi
kupitia harakati zetu za mapambano dhidi ya maovu ya aina zote
.
Kamwe hatuwezi
kulikamilisha jukumu la kizazi chetu, jukumu la kujikomboa
kiuchumi
kama tutaonyesha hofu ya
kupambana na maovu katika jamii.
Tuwe tayari kujitoa
muhanga. Kila mzalendo wa nchi hii apambane mahali alipo kwa
kutumia silaha iliyo
karibu naye. Apambane kwa ajili ya Tanzania kama taifa. Ni jukumu la kizazi
chetu
Katika mapambano haya,
tusikubali matokeo mengine bali ni ushindi wa jumla. Na huko nyuma niliwahi
kutoa mfano wa Ken-Saro Wiwa wa Nigeria. Ni mfano wa vijana wengi wa bara hili,
vijana waliolitafuta jukumu la kizazi chao, wakalitekeleza,
hawakulisaliti.
Kijana huyu alikuwa ni
mwanaharakati wa haki za kimazingira. Aliwahamasisha watu wa
kabila la Ogoni,
kuandamana na kupinga kampuni ya mafuta ya Shell BP ya Uingereza kupewa eneo
kubwa la ardhi ya Ogoni ili waachimbe mafuta. Fedha zilizotokana na mafuta hayo
ziliishia mifukoni mwa wateule wachache kule Lagos.
Watu wa Ogoni walibaki
na ufukara wao na huku mazingira yao yakiharibiwa vibaya. Zaidi ya miaka kumi na
sita iliyopita, Ken-Saro Wiwa na wenzake 17 walinyongwa na utawala wa kijeshi wa
Nigeria.
Saro Wiwa alijitoa
mhanga. Dunia ikafahamu madhira ya watu wa Ogoni. Mabadiliko
yakatokea. Saro-Wiwa na
wenzake walikufa kwa ajili ya kizazi cha leo na
kesho cha Kabila la
Ogoni na Wanaigeria kwa ujumla.
Ni heri kufa na kuacha
fikra zinazoishi kuliko kuishi bila kufikiri.
Nahitimisha.
Post a Comment