Saed Kubenea - Mapendekezo ya Katiba Mpya
13/01/2013
Nani anataka nini katika katiba mpya?
Haya ni maoni yaliyowasilishwa na Saed Kubenea wa MwanaHALISI;
gazeti lililofungiwa na serikali kwa muda usiojulikana tangu 30 Julai 2012.
JUZI (10 Januari 2013) wenye vyombo vya habari na asasi nyingine za
habari waliwasilisha kwa Tume ya Katiba Mpya, mapendekezo ya asasi zao na hata
kuongeza maoni binafsi kama mwenyekiti wa mkutano wa Katiba, Prof. Mwesiga
Baregu alivyoruhusu.
Saed Kubenea, Mkurugenzi Mtendaji wa Hali
Halisi Publishers Limited (HHPL), wachapishaji wa magazeti ya MwanaHALISI na
MISETO, aliwasilisha maoni yake. Ndimara Tegambwage ameyasoma na kuyafanya moja
ya mambo muhimu aliyoona yenye thamani. Anatushirikisha:
Mapendekezo:
Katiba Mpya (Na Saed Kubenea)
1. Kuhusu vyombo vya
Habari
KATIBA itamke kuwa vyombo vya kutunga sheria (Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania; Baraza la Wawakilishi, Bunge la Tanganyika au Bunge la
Shirikisho; na vyovyote vile vitakavyokuwepo) visitunge:
a) Sheria
inayopingana (inayokinzana), inayokwaza au kuingilia uhuru wa kuwa na maoni
(kufikiri)
b) Sheria inayopingana, inayokwaza au kuingilia uhuru wa kujieleza
(kutoa kauli)
c) Sheria inayopingana, inayokwaza au kuingilia uhuru wa
habari (kupata habari zozote zinazohusu jamii zilizoko mikononi mwa
serikali)
d) Sheria inayopingana, inayokwaza au kuingilia uhuru wa vyombo vya
habari (kazi za utafutaji, ukusanyaji na usambazaji wa habari inayofanywa na
waandishi wa habari na watangazaji)
e) Sheria inayopingana, inayokwaza au
kuingilia uhuru wa kujumuika kwa amani (mikutano/maandamano ambavyo kihalisi ni
njia za wanajamii kuwasiliana au kupeleka ujumbe kwa wahusika)
2.
Kuhusu Mamlaka ya DPP
Katiba itamke kuwa:
a) Mkurugenzi wa
Mashitaka (DPP) ateuliwe na chombo huru cha uteuzi (siyo rais wa nchi) na
athibitishwe na Bunge
b) DPP awajibike kwa Bunge (Chombo cha kutunga sheria)
3. Mapendekezo Mengine
1. Katiba itamke kuwa ARDHI ni mali
ya Watanzania. Isiwekwe chini ya rais bali iwe chini ya wananchi wa Tanzania.
Serikali itakuwa tu na mamlaka ya kutwaa ardhi kwa ajili ya manufaa ya umma
ambayo yameainishwa kama vile ujenzi wa miundombinu, utunzaji wa mazingira na
uboreshaji makazi. Serikali isiwe na uwezo wa kutwaa ardhi kwa ajili ya
uwekezaji wa mtu binafsi au kampuni kama inavyoelezwa sasa na Sheria ya Ardhi ya
Mwaka 1999.
2. Katiba itamke kuwa kila kijiji kitakuwa na serikali ya
kijiji ambayo itaongoza kijiji hicho pamoja na uwezo wa kutunga sheria ndogo na
kuzipitisha chini ya usimamizi wa mkutano mkuu wa kijiji. Serikali za vijiji
ndizo zitakuwa na mamlaka ya kusimamia na kulinda haki za wananchi juu ya
umiliki wao wa ardhi ya kijiji na kupanga mipango ya matumizi ya ardhi. Zitakuwa
na uwezo wa kutoza kodi na kuendesha miradi ya maendeleo vijijini.
3.
Katiba itamke kuwa rasilimali za madini, mafuta, gesi na maliasili, ni mali ya
Watanzania na ni lazima zitumike na kuvunwa kwa manufaa ya Watanzania. Serikali
haitasaini mikataba bila kibali cha bunge; bali itakuwa na uwezo wa kutoa leseni
za utumiwaji wake. Utoaji huo wa leseni lazima pia uwe wa wazi na ambao
utaidhinishwa na Bunge.
4. Katiba itamke kwamba migogoro yote ya
uwekezaji sharti isuluhishwe kwa mujibu wa sheria za Tanzania na Mahakama za
Tanzania. Hili ni takwa la Kanuni ya makubaliano ya Calvo na vilevile Azimio Na.
1803 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Mwaka 1962 na Azimio Na. 3281 la 1974
la Baraza hilo juu ya Haki na Wajibu wa Mataifa juu ya Maliasili.
5.
Katiba itamke kuwa rais atachaguliwa kwa kupigiwa kura na kupata zaidi ya
asilimia 50 ya kura za watu wanaotakiwa kupiga kura. Yeye na serikali yake ni
lazima awajibike kwa bunge na kila uteuzi anaofanya kwa nafasi za juu za
uongozi, sharti uidhinishwe na bunge baada ya Bunge kuhojiana nao.
6. Katiba
itamke kuwa Bunge lina madaraka na haki ya kumfuta kazi rais kwa kutowajibika au
kwa kutumia madaraka yake vibaya.
7. Katiba itamke kuwa rais hatakuwa na
haki au uwezo wa kulivunja bunge kwa sababu yoyote ile.
8. Katiba itamke
kuwa rais hatakuwa na kinga dhidi ya mashitaka yoyote yale akiwa madarakani na
baada ya kutoka madarakani. Mtu yeyote anaweza kufungua kesi dhidi yake binafsi
au ofisi yake.
9. Katiba itamke kuwa uteuzi wa majaji wa mahakama kuu na
mahakama ya rufaa ufanywe na chombo huru (badala ya rais) na ufuate umahiri na
uelewa wa sheria pamoja na uadilifu wa kimaadili na kisheria.
10. Katiba
itamke kuwa mhimili wa Mahakama, ukiongozwa na Jaji Mkuu, ndio usimamie na
kuwasilisha bajeti yake bungeni (badala ya serikali kama ilivyo
sasa).
11. Katiba itamke kuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na
viongozi wengine wakuu wa tume, wateuliwe na chombo huru cha uteuzi baada ya
wanaotaka nafasi hiyo kuomba na kufanyiwa usaili. Aidha, maamuzi ya tume, kwa
nafasi yoyote ile ya wagombea, yaweze kupingwa na mtu yeyote
mahakamani.
12. Katiba itamke kuwa kukosa uadilifu au kutumia madaraka
vibaya, kama itakavyothibitishwa na chombo husika, ni kosa la jinai.
13.
Katiba itamke kuwa wote wanaojipatia utajiri kwa kuhujumu uchumi au watu
wanaojitajirisha kwa kutumia madaraka yao ya umma, lazima washitakiwe kwa kosa
la uhaini na mali zao zote, ikiwa ni pamoja na zile za walionufaika kutokana na
kosa hilo, zitaifishwe.
14. Cheo cha Makamu wa Rais kiondolewe. Kibaki
cha Waziri Mkuu.
15. Katiba itamke kuwa wakuu wa mikoa, wilaya (kama ni
lazima kuendelea kuwa nao) wapatikane kwa kupigiwa akura ili w3aweze kuwajibika
vema katika maeneo yao. Mameya wa miji na majiji nao wachaguliwe na wananchi
moja kwa moja badala ya kuchaguliwa na madiwani.
16. Katiba itamke haki
ya kuishi katika mazingira safi na salama lazima.
17. Katiba itamke
kuwapo haki ya kufungua kesi za kutetea katiba, haki za binadamu na utawala wa
sheria bila gharama zozote zile.
18. Katiba itamke kuwa elimu na afya ni
haki kwa Watanzania wote.
19. Katiba itamke haki ya
starehe.
Mwisho.
on Sunday, January 13, 2013
Post a Comment