HIFADHI YA SERENGETI YANYAKUA TUZO YA KIMATAIFA YA UTALII
PRESS
RELEASE
HIFADHI
YA TAIFA SERENGETI YATEULIWA MSHINDI WA TUZO YA KIMATAIFA YA
UTALII
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeteuliwa
kuwa mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Utalii, Hoteli na Huduma za Vyakula kwa
mwaka 2013. Uteuzi huu umefanywa na kamati ya uteuzi ya tuzo hizo baada ya
Serengeti kukidhi vigezo vilivyowekwa na waandaaji wa tuzo
hizo.
Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA) litapokea tuzo hiyo itakayotolewa kwa Serengeti katika hafla maalum
itakayofanyika mjini Madrid nchini Hispania tarehe 30.01.2013. Tuzo hizi
huandaliwa na taasisi maarufu duniani inayofahamika kama Global Trade
Leaders’ Clubinayohusisha makampuni yapatayo 7000 duniani. Tuzo hii
ilianzishwa kwa ajili ya kutambua na kuenzi michango inayotolewa na taasisi na
makampuni yanayojihusisha na utalii, hoteli pamoja na huduma za vyakula kama
njia ya kuthamini mchango na kuhamasisha wale wote wanaofanya kazi katika sekta
hii ambayo ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi
husika.
Hafla ya utoaji wa tuzo za
mwaka huu itahudhuriwa na wadau wa shughuli za utalii kutoka nchi zipatazo 40
duniani na zitaambatana na Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii yanayofanyika kila
mwaka mjini Madrid, maarufu kama FITUR ambayo Tanzania ni
mshiriki.
Hifadhi ya Serengeti ni
hifadhi kongwe nchini ambayo ilianzishwa miaka zaidi ya hamsini iliyopita na
ambayo pia ni Eneo la Urithi wa Dunia. Hifadhi hii ni maarufu kwa Nyumbu wahamao
kila mwaka katika mzunguko unaohusisha nchi mbili za Tanzania na Kenya. Mzunguko
huu wa wanyama wahamao unaaminika kuwa ndio pekee uliobakia ulimwenguni
unaohusisha wanyama wakubwa wa ardhini.
Kutolewa kwa tuzo hii
ambayo ni heshima kwa TANAPA na nchi kwa ujumla ni matokeo ya sera nzuri za
uhifadhi zinazosimamiwa na TANAPA katika kuhakikisha kuwa maeneo yaliyotengwa
kisheria kama Hifadhi za Taifa yanaendelea kuhifadhiwa vema kwa ajili ya vizazi
vijavyo lakini pia kuhakikisha kuwa viwango vya huduma za utalii katika hifadhi
zinakuwa za kiwango cha kimataifa ili kuhudumia wageni watokao sehemu mbalimbali
ulimwenguni.
Imetolewa na Pascal
Shelutete
MENEJA
UHUSIANO
HIFADHI ZA TAIFA
TANZANIA
29 Januari,
2013
Post a Comment