Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete akitoa hotuba ya kuukaribisha
mwaka mpya wa 2013, kwa Wananchi, Jana Jumatatu, tarehe 31 Desemba, 2012, Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Utangulizi
Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu;
Ni furaha na faraja kubwa kuifikia siku hii
adhimu ya kuuaga mwaka wa 2012 na kuukaribisha mwaka 2013. Ni jambo la bahati
ambayo hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia
uzima na kutuwezesha kuumaliza mwaka huu salama. Wapo ndugu, jamaa na marafiki
zetu wengi ambao wangependa kuiona siku hii lakini hawakujaaliwa. Wametangulia
mbele ya haki. Tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema.
Amin. Nasi tumuombe Mola wetu atujaalie fanaka tele katika mwaka ujao.
Mapitio ya
Mwaka 2012
Ndugu wananchi;
Mwaka tunaoumaliza leo ulikuwa wenye mambo
mengi mazuri na mafanikio makubwa, lakini, pia, ulikuwa na changamoto zake.
Baadhi zilikuwa ngumu na zipo zilizokuwa za kusikitisha na kuhuzunisha.
Ajali za barabarani na majini ziliendelea
kupoteza maisha ya watu wengi na kusababisha majeraha na ulemavu kwa maelfu.
Ajali mbaya kuliko zote kutokea, mwaka huu, ilikuwa ile ya meli ya MV Skagit
iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012 ambapo watu 144 walipoteza maisha. Ajali za
barabarani zilizosababisha vifo nazo ziliongezeka kutoka 3,012 mwaka 2011 hadi
kufikia 3,144 na kusababisha
vifo vya ndugu zetu 3,714.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia ajali ya MV Skagit ambayo ilitokea
miezi 11 baada ya ile ya MV Spice Islander, Serikali zetu mbili zimekuwa
zikishirikiana kwa karibu kuhusu masuala ya usafiri wa majini kati ya Tanzania
Bara na Zanzibar. Kwa ajili hiyo SUMATRA na Zanzibar Maritime Authority
zinafanya kazi kwa karibu zaidi na kanuni za usafirishaji wa abiria na mizigo na
za usajili na ubora wa meli zimewianishwa. Ni matumaini yetu kuwa hatua hizo
zitasaidia kumaliza ajali zinazotokana na makosa ya wanadamu.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa ajali za barabarani tuliendelea
na tutaendelea kuwahimiza madereva kuheshimu Sheria za Usalama Barabarani,
waepuke uzembe na hasa ulevi wakati wa kuendesha. Tutaendelea kuwakumbusha
wenye magari kuhakikisha kuwa uzima wa magari yao unakuwa wa kiwango cha juu.
Hali kadhalika, tumewataka Polisi waongeze ukali na kuwabana ipasavyo madereva
na wamiliki wa magari ili watekeleze wajibu wao na wasipofanya hivyo
wawajibishwe inavyostahili.
Hali ya Usalama
Ndugu wananchi;
Tunaumaliza mwaka huu nchi yetu ikiwa shwari,
salama na tulivu. Tuombe Mungu hali hii iendelee mwaka 2013 na idumu milele.
Mipaka ya nchi yetu ipo salama na uhusiano na majirani na nchi zote duniani ni
mzuri. Tunaendelea kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka kati ya nchi yetu na
Malawi katika Ziwa Nyasa kwa njia ya mazungumzo. Suala hilo limewasilishwa kwa
pamoja na Serikali zote mbili kwa Mheshimiwa Joaquim Chissano, Mwenyekiti wa
Umoja wa Viongozi Wastaafu wa Afrika kwa ajili kuzisaidia nchi zetu kupata
ufumbuzi. Matumaini yetu ni kuwa viongozi hao watalishughulikia suala hili
mapema iwezekanavyo.
Ushirikiano wa Kanda
Ndugu Wananchi;
Ushirikiano wetu wa kikanda katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
unaendelea vizuri. Mwaka huu nchi yetu imepewa heshima kubwa ya kuwa Mwenyekiti
wa Chombo cha SADC kinachoshughulikia masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
Jukumu hilo ni zito na hasa katika kipindi
hiki ambapo kuna changamoto za kisiasa na kiusalama katika nchi za Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na Zimbabwe. Nchi yetu inatarajiwa kuongoza
juhudi za kupata ufumbuzi wa migogoro hiyo migumu. Ndiyo maana tulifanya
Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi za SADC hapa Dar es Salaam tarehe 7 na 8
Desemba, 2012. Mwaka ujao, kwa kushirikiana na wenzetu, tutaendeleza juhudi
zetu. Ni matumaini yangu kuwa tukipata ushirikiano wa viongozi na wananchi wa
nchi husika na jumuiya ya kimataifa tutapata ufumbuzi tunaotaka.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
tumeendelea kushuhudia Jumuiya hiyo na harakati za utangamano zikizidi kustawi.
Jengo la Makao Makuu ya Jumuiya limekamilika na kuzinduliwa rasmi tarehe 28
Novemba, 2012. Siku hiyo hiyo kule Athi River, Kenya, barabara ya kutoka Arusha
hadi Athi River ilizinduliwa. Barabara hii ni moja ya miradi kadhaa
inayotekelezwa kwa pamoja na nchi wanachama wa Jumuiya wa Afrika Mashariki.
Mchakato wa utangamano wa kiuchumi wa Afrika
Mashariki unaendelea kwa kasi. Tanzania ikiwa sehemu kamili ya mchakato huo,
lazima tuhakikishe kuwa tunakwenda nao sambamba. Tusikubali kuachwa nyuma wala
kuwa chanzo cha kuuchelewesha mchakato huo bila ya sababu za msingi. Utangamano
una maslahi kwa nchi yetu na manufaa yake ni makubwa. Kwa mfano, mauzo yetu
katika soka la Afrika Mashariki yameongezeka sana kutoka dola za Kimarekani
milioni 58.6 mwaka 2000 hadi kufikia dola za Kimarekani milioni 409 mwaka
2011.
Jumuiya imekuwa kichocheo muhimu cha kukuza
uzalishaji, ajira na uchumi hapa nchini. Kwa ukubwa wa nchi yetu na rasilimali
tulizonazo tuna matumaini makubwa ya kunufaika zaidi siku za usoni. Naweza
kuthubutu hata kusema kuwa Tanzania inaweza kunufaika zaidi kuliko nchi nyingine
wanachama wa Jumuiya hiyo. Kinachotakiwa ni sisi kujipanga vizuri kwa sera na
mipango ili tuzitumie fursa tulizonazo kwa maslahi ya uchumi na maendeleo ya
nchi yetu na watu wake. Tuache woga, tujiamini.
Matishio ya
Usalama
Ndugu Wananchi;
Licha ya kumaliza mwaka nchi ikiwa shwari na
yenye amani na utulivu, yalikuwepo matukio yaliyotishia usalama wetu. Bahati
mbaya na kwa masikitiko makubwa matukio hayo yalisababishwa na baadhi ya
viongozi wa dini na siasa na wafuasi wao. Kwa kweli kwa mara ya kwanza nchi
yetu ilifikishwa kwenye hatari ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa Watanzania au
hata mapigano ya raia kwa misingi ya dini zao. Bahati nzuri hilo halikutokea na
Mungu aliepushe lisitokee kamwe.
Nimeshalisemea jambo hili siku za nyuma na
napenda kurudia tena leo kuwasihi Watanzania wenzangu kupima athari za kauli
zetu na matendo yetu kwa mustakabali wa jamii yetu, nchi yetu na watu wake.
Viongozi wa dini, waumini na viongozi wa siasa na wafuasi wao wanao wajibu
maalum wa kuhakikisha kuwa Watanzania wanaendelea kuishi kwa upendo, amani na
ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zao, makabila yao, rangi zao au maeneo
watokako. Hiyo ndiyo sifa ya nchi yetu tunayoijua sote ambayo ni njema na watu
wengi wanataka kuja kujifunza kwetu na wale wenye shida wanatamani wawe kama
sisi. Hii ni tunu muhimu ya taifa ambayo tusikubali kuipoteza kwa maslahi
binafsi ya watu wachache.
Ndugu Wananchi;
Wakati wo wote, lazima tutambue umuhimu wa
kuvumiliana na kuheshimiana kwa tofauti zetu za kidini, rangi, kabila, tutokako
na ufuasi wa vyama vya siasa. Lazima pia tuhakikishe kuwa tunaheshimu sheria
na taratibu zinazotawala mikutano na maandamano. Tukiyazingatia hayo nchi yetu
itakuwa haina tishio lo lote kwa amani na usalama wake. Yasipozingatiwa
tunaiweka nchi yetu hatarini. Sisi katika Serikali tutakuwa hatuna la kufanya
bali kutimiza wajibu wetu wa kulinda usalama wa raia na nchi yetu. Wahusika
watachukuliwa hatua na vyombo vya usalama na kisheria kwa mujibu wa sheria za
nchi. Tulifanya hivyo mwaka huu na hatutakuwa na ajizi kufanya hivyo siku yo
yote kama hapana budi.
Uhalifu
Unapungua
Ndugu Wananchi;
Inatia moyo kuona kuwa mwaka huu makosa ya
jinai yalipungua na kufikia 66,255 yakilinganishwa na makosa 69,678 ya mwaka
jana au 94,390 ya mwaka juzi. Hii inathibitisha kuimarika kwa kazi nzuri
inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana na wananchi na vyombo vingine vya
usalama. Pamoja na hayo lazima tuongeze juhudi za kupambana na uhalifu kwani
bado matukio ni mengi mno na upungufu bado ni mdogo. Tutaendeleza kazi
tuifanyayo sasa ya kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa rasilimali watu, zana na
vitendea kazi husika.
Uhalifu wa
Kimtandao
Ndugu Wananchi;
Tutaongeza nguvu katika kupambana na uhalifu
unaoendeshwa na mitandao ya uhalifu ndani na nje ya nchi. Mitandao hiyo hasa
imekuwa inajihusisha na biashara ya kusafirisha wanadamu, biashara ya dawa za
kulevya na biashara ya nyara za Serikali.
Mapambano dhidi ya uhalifu wa kimtandao
yametuwezesha kukamata wahamiaji haramu 4,765 na tayari 1,611 wamerudishwa kwao.
Kwa upande wa dawa za kulevya watuhumiwa 6,929 walikamatwa mwaka huu
ukilinganisha na 209 mwaka 2011. Kilo 55,285 za dawa za kulevya zilikamatwa
mwaka huu ukilinganisha na kilo 17,752.4 mwaka jana. Kwa upande wa nyara za
Serikali, zilizokamatwa ni 1,416 na kati ya hizo 736 ni meno ya tembo.
Watuhumiwa 1,037 walikamatwa na kesi 746 zipo Mahakamani katika hatua
mbalimbali.
Ndugu Wananchi;
Taarifa hizi zinathibitisha kuimarika kwa
jitihada za kupambana na uhalifu wa kimtandao. Tutaimarisha zaidi jitihada zetu
mwaka 2013 ili tupate mafanikio zaidi. Tutaviongezea uwezo wa rasilimali watu,
zana, vifaa na fedha za uendeshaji vyombo vyetu vya usalama vinavyoongoza
mapambano haya.
Tutaimarisha na kuendeleza ushirikiano baina ya
nchi yetu na nchi jirani na nyinginezo duniani. Hii itasaidia kutuongezea uwezo
wa kupambana na mitandao ya uhalifu ndani ya nchi, kikanda na kimataifa. Pia
tutazipitia upya sheria za kupambana na makosa haya kwa nia ya
kuziboresha.
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013, tutapanua na kuimarisha
huduma ya matibabu kwa watu walioathirika na dawa za kulevya kote nchini.
Tutakamilisha ujenzi wa kituo cha Dodoma na kujenga kingine kipya Dar es
Salaam. Natoa wito kwa wale wote walioathirika au watu wenye watoto au rafiki
au jamaa walioathirika waende hospitali kupatiwa matibabu kwani matibabu hayo ni
bure.
Hali ya
Uchumi
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2012, tunaoumaliza leo, uchumi wa
nchi yetu uliendelea kukua na kuimarika licha ya kuwepo kwa changamoto za
upatikanaji wa umeme, kupanda kwa bei za mafuta na chakula duniani na uhaba wa
mvua katika maeneo mengi nchini uliosababisha kupungua kwa uzalishaji na kupanda
kwa bei za vyakula nchini. Pia, licha ya kuendelea kwa msukosuko wa uchumi wa
dunia na hasa katika Bara la Ulaya ambako ni soko kuu la bidhaa zetu na watalii.
Mategemeo yetu ni kuwa, mwaka huu, uchumi wetu utakua kwa asilimia 6.8 na
mwakani (2013) utakua kwa asilimia 7.0 ukilinganisha na asilimia 6.4 mwaka
2011.
Kwa jumla, ukilinganisha na makadirio ya IMF ya
kiwango cha ukuaji wa uchumi wa dunia kuwa asilimia 3.3 mwaka huu, ni dhahiri
kuwa uchumi wetu unakua kwa kasi nzuri na kuifanya Tanzania iendelee kuwa
miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.
Hali hii ya uchumi wetu ina maana kubwa mbili.
Kwanza, kwamba uchumi wetu umejenga uhimilivu dhidi ya misukosuko ya uchumi wa
dunia. Na pili, kwamba shughuli za uzalishaji na huduma zinazidi kukua na mauzo
ya bidhaa ndani na nje ya nchi yameongezeka. Kuongezeka kwa mauzo ya nje
kumefanya akiba yetu ya fedha za kigeni kufikia dola za Marekani bilioni 3.9
mwezi Novemba, 2012 kiasi ambacho kinatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa
miezi minne.
Ndugu Wananchi;
Makusanyo ya mapato ya Serikali yatokanayo na
kodi yalifikia shilingi bilioni 580.3 mwezi Oktoba, 2012 ikilinganishwa na
shilingi bilioni 479.3 mwezi Oktoba 2011. Matarajio yetu ni kufanya vizuri
zaidi mwaka 2013 kwa mapato yatokanayo na kodi na yale yasiyotokana na kodi
ambayo bado ni chini ya lengo.
Ndugu Wananchi;
Mfumuko wa bei kuwa juu ni changamoto ambayo
tunaendelea kuikabili ili kuleta utulivu uliokamilifu kwa uchumi wetu na
kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wa Tanzania. Serikali imechukua hatua
kadhaa kudhibiti hali hiyo na mafanikio ya kututia moyo yameanza kuonekana. Kwa
mfano, mfumuko wa bei umepungua kutoka asilimia 19.8 mwezi Desemba 2011 hadi
asilimia 12.1 mwezi Novemba, 2012. Kiwango hicho bado ni cha juu na
hakikubaliki. Tutaendelea kuchukua hatua zaidi ili tuweze kufikia lengo letu la
mfumuko wa bei kuwa chini ya asilimia 10 ifikapo mwezi Juni, 2013.
Miongoni mwa mambo tuliyopanga kufanya ili
kupunguza mfumuko wa bei ni kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme na kudhibiti
mwenendo wa bei ya mafuta. Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza gharama za
uzalishaji na uchukuzi wa bidhaa. Aidha, tutaendelea kutekeleza mipango na
mikakati ya kukuza na kuboresha kilimo nchini kwa lengo la kujihakikishia
usalama wa chakula, kukuza pato la taifa na kupunguza umaskini hasa miongoni mwa
wakulima.
Utekelezaji wa
Miradi ya Maendeleo
Ndugu wananchi;
Mwaka huu tunaoumaliza leo ulikuwa na mafanikio
ya kutia moyo kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya kuendeleza miundombinu
nchini. Tumeshuhudia miradi ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, reli,
bandari, umeme na maji ikikamilika, au kuanzwa au utekelezaji wake ukiwa
unaendelea. Hakika lengo la kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara kwa
barabara za lami siyo ndoto tena bali ni jambo la uhakika na litatimia muda si
mrefu ujao.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa reli, mwaka huu tumeendelea
kukarabati reli ya kati na kurejesha usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam
kwenda Mwanza na Kigoma. Mwaka ujao (2013) tutaendeleza kazi ya ukarabati wa
reli hiyo muhimu na kuzidi kuboresha huduma. Tumekamilisha ujenzi wa viwanja
vya ndege vya Mpanda na Songwe na tunaendelea kuboresha viwanja vya Tabora,
Kigoma, Bukoba, Mafia, Mwanza na Zanzibar. Tumeendelea kujenga na kupanua
miundombinu ya maji nchini na kuboresha upatikanaji wa maji salama kwa
Watanzania. Kwa mwaka huu usambazaji wa maji salama umefikia asilimia 87 kwa
watu wa mijini na asilimia 61.5 vijijini. Tutaendeleza kazi hiyo mwaka
2013.
Msongamano wa
Magari Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Katika Jiji la Dar es Salaam tumeendelea na
tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza msongamano wa magari unaozidi
kuongezeka. Barabara mpya zimejengwa na zinaendelea kujengwa ndani na kuzunguka
Jiji. Barabara kadhaa zimepanuliwa na nyingine zitaendelea kupanuliwa. Ujenzi
wa miundombinu (barabara na vituo) ya mabasi yaendayo haraka umeanza. Mwaka
2013 ujenzi wa barabara za juu ya nyingine katika makutano ya TAZARA utaanza na
matayarisho ya kufanya hivyo kwa makutano ya Ubungo yatakamilishwa.
Tumetimiza ahadi yetu ya kutumia treni
kusafirisha abiria katika jiji la Dar es Salaam. Usafirishaji umeanza na
unaendelea kati ya Stesheni na Ubungo na kutoka Stesheni ya TAZARA hadi Pugu –
Mwakanga. Mwaka ujao tutaendelea kuimarisha usafiri huo kwa kuongeza treni na
idadi ya safari. Tayari Mshauri Mwelekezi ameshateuliwa kufanya upembuzi
yakinifu na kushauri kuhusu kupanua huduma hiyo mpaka ifike Tegeta, Bunju,
Kimara, Luguruni, Kibaha, Mbagala-Rangi Tatu na Kongowe. Ushauri huo pia
utahusu kuwa na huduma bora ya usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam kwa
maana ya aina ya njia, vichwa vya treni na mabehewa. Tuliamua kuanza na reli na
treni iliyopo, lakini nia yetu ni kufanya vile hasa inavyotakiwa iwe kwa usafiri
wa treni mijini.
Umeme
Ndugu Wananchi;
Mwaka tunaoumaliza leo haukuwa rahisi kwa
upande wa upatikanaji wa umeme. Mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kidatu, Kihansi,
Mtera, Pangani na Nyumba ya Mungu yameendelea kutokuwa na maji ya kutosha kwa
sababu ya uhaba wa mvua. Hivyo basi taifa limelazimika kutegemea umeme wa
kukodi unaozalishwa kwa kutumia mafuta. Umeme huo umekuwa wa gharama kubwa na
hivyo kuwa mzigo mkubwa kwa TANESCO na taifa. Serikali imeendelea kushirikiana
na TANESCO na kuisaidia kubeba mzigo huo. Tutaendelea kufanya hivyo mwaka ujao
na mpaka tutakapofikia hatua ya kutokuwa na ulazima wa kutumia umeme wa
kukodi.
Ndugu Wananchi;
Mtakumbuka kuwa tulipopata tatizo la ukame na
upungufu wa umeme mwaka 2006/2007, Serikali yetu iliazimia kuongeza uzalishaji
wa umeme kutokana na vyanzo vingine vikiwemo gesi asili, makaa ya mawe, upepo na
jua. Nafurahi kusema kuwa, tangu wakati ule Serikali imeiwezesha TANESCO
kujenga vituo vitatu vinavyozalisha MW 245 kwa kutumia gesi.
Hatukuweza kuongeza zaidi uzalishaji wa umeme
kwa kutumia gesi kwa sababu ya kiasi cha gesi kinacholetwa Dar es Salaam kutoka
Songo Songo kuwa kidogo. Ndiyo maana tukaamua kujenga bomba jipya kubwa la
kusafirisha gesi kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam.
Ndugu Wananchi;
Kwa nia ya kutaka kuhakikisha kuwa kutakuwa na
gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi pale inapohitajika, ikaamuliwa
bomba hilo liendelezwe mpaka visima vya gesi vya Mtwara. Ujenzi wa bomba hilo
umeanza mwezi Novemba, 2012 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18. Gesi
itakayopatikana ina uwezo wa kuzalisha MW 3,000 za umeme. Tayari mipango
inaendelea ya kujenga mitambo ya kuzalisha MW 900 pale Kinyerezi ili mara gesi
itakapofika umeme uzalishwe. Hatua hiyo itatuwezesha kuung’oa mzizi wa fitina
wa mgao wa umeme na mzigo wa kununua umeme ulio ghali.
Utafutaji wa
Gesi
Ndugu Wananchi;
Tangu
mwaka 2010 gesi nyingi imegundulika baharini na nchi kavu katika Mikoa ya
Mtwara, Lindi na Pwani. Utafutaji bado unaendelea na tuna matumaini kuwa gesi
nyingi zaidi huenda ikagundulika. Hivi sasa Serikali inaandaa sera na sheria
mpya ya gesi ili kuboresha zinazotumika wakati huu. Nia yetu ni kutaka
kuhakikisha kuwa rasilimali hii adhimu inasimamiwa vizuri kwa manufaa ya nchi
yetu na watu wake pamoja na kulinda maslahi ya wawekezaji.
Napenda kutumia nafasi hii kuwahakikishia ndugu
zetu wa kule gesi ilipogunduliwa au popote itakapogundulika, kuwa watanufaika
sawia na katu hawatasahaulika. Rai yao ya kutaka na wao wanufaike inakubalika
na Serikali inajiandaa hivyo. Viongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa mfano,
wanajua maelekezo niliyotoa kuhusu kuiandaa miji ya Mtwara na Lindi kupokea
uchumi wa gesi.
Lakini, sharti la kutaka gesi isisafirishwe
kwenda kokote na kwamba kila kitu kifanyike kwao halikubaliki. Rasilimali
inayopatikana po pote katika nchi hii ni mali ya taifa zima na hutumika kwa
manufaa ya taifa. Katu siyo mali ya watu wa pale ilipogundulika au pale
shughuli hizo zinapofanyika. Jumla ya makusanyo ya mapato yatokayo sehemu zote
za nchi yetu na kutokana na vyanzo mbalimbali ndiyo yanayotumika kuhudumia watu
wote po pote walipo.
Ndugu Wananchi;
Huu ni msingi mzuri, ni sera nzuri na ni jambo
jema la tunu, tulilorithi kwa waasisi wa Taifa letu, ambalo hatuna budi kulienzi
na kulidumisha. Nawasihi wanasiasa wenzangu tusiwaelekeze kwenye mambo mabaya
wananchi tunaodai kuwapenda. Kutafuta umaarufu kwa agenda zinazopandikiza chuki
kwa watu na kuligawa au kulibomoa taifa, ni upungufu mkubwa wa uongozi na
uzalendo. Tuache siasa za ubarakara na kuwapa watu matumaini yasiyotekelezeka.
Nawaomba wananchi msiwasikilize, si watu wanaowatakia mema na wala hawaitakii
mema nchi yetu.
Elimu
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio katika utekelezaji
wa sera yetu ya kupanua fursa ya elimu kwa Watanzania katika ngazi zote. Mwaka
huu vijana wetu wengi zaidi walijiunga na elimu ya msingi, sekondari, ufundi na
elimu ya juu. Hivi sasa tunaelekeza juhudi zetu zaidi katika kuongeza ubora wa
elimu. Kwa ajili hiyo, tumechukua hatua za makusudi za kupanua mafunzo na
ajira za walimu wa shule za msingi na sekondari. Kwa mfano, mwaka huu walimu
24,621 wapya waliajiriwa kati yao 11,379 wa shule za msingi na 13,242 wa shule
za sekondari. Januari, 2013 tunategemea kuajiri walimu 28,746 kati yao 14,606
wa shule za msingi na 14,060 watakuwa wa shule za sekondari.
Kwa sababu hiyo, uwiano wa mwalimu kwa
wanafunzi umeendelea kuwa mzuri. Hivi sasa kwa shule za msingi uwiano umefikia
1:46 ukilinganisha na 1:56 mwaka 2005. Uwiano unaostahili ni 1:40. Kwa upande wa
sekondari uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi hivi sasa ni 1:29 ukilinganisha na
1:20 unaostahili. Kutokana na upanuzi wa vyuo vya kufundisha walimu nchini,
bila ya shaka baada ya miaka mitatu hivi upungufu wa walimu wa shule za msingi
na sekondari haitakuwa kilio tena.
Ndugu Wananchi;
Upatikanaji wa vitabu nao unazidi kuwa bora.
Hivi sasa uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi ni 1:3 kwa shule ya msingi na
sekondari 1:3 ukilinganisha na 1:5 kwa shule za msingi na sekondari 1:4 mwaka
2009. Hata hivyo, tutaendelea kuongeza mgao wa fedha katika bajeti ya elimu ili
kuongeza upatikanaji wa vitabu na vifaa vingine vya kusomea na kufundishia.
Tunataka katika muda mfupi ujao uwiano uwe 1:1.
Kwa upande wa maabara za sayansi, tarehe 4
Novemba, 2012, nilipokuwa kwenye ziara ya Mkoa wa Singida, nilitoa agizo la
kutaka ndani ya miaka miwili, kuanzia mwaka 2013, kila shule ya sekondari ya
kata nchini iwe na majengo ya maabara yaliyokamilika. Yawe pia yanatumika kwa
maana ya vifaa na mahitaji muhimu. Nimewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya
kuhakikisha kuwa agizo hili linatekelezwa kwa ukamilifu. Kuanzia sasa, katika
ziara zitakazofanywa Mikoani na mimi, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu tutapenda
kupata taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wake.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa ufundishaji imedhihirika kwamba
mkakati maalum unahitajika kuboresha ufundishaji wa masomo ya hisabati,
kiingereza na sayansi katika shule za msingi na sekondari. Matokeo ya mitihani
ya darasa la saba na kidato cha nne kwa miaka mingi sasa yanathibitisha haja
hii. Sasa wakati umefika kwa suala hili kulipa uzito unaostahili. Tutafanya
hivyo kuanzia mwaka 2013.
Afya
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2012 ulikuwa na mafanikio mengi ya kutia
moyo kwa upande wa sekta ya afya nchini pamoja na kuwepo kwa changamoto
mbalimbali. Kazi ya kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi watu kwa maana
ya kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali mpya na kuimarisha zilizopo
iliendelea kutekelezwa kwa mafanikio kote nchini.
Hali kadhalika, uwezo wetu wa ndani wa
uchunguzi na tiba ya magonjwa makubwa umezidi kuimarika mwaka huu. Upatikanaji
wa dawa, vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba umeendelea kuboreshwa. Aidha,
mafunzo na ajira za madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa afya vimeendelea
kuongezwa. Kituo cha Tiba ya Maradhi ya Moyo kimekamilika katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili na mwaka ujao (2013) shughuli za upasuaji na nyinginezo
husika kutibu maradhi ya moyo zitakuwa zimeboreshwa sana. Upanuzi mkubwa wa
Hospitali ya Saratani ya Ocean Road umekamilika. Kwa ajili hiyo, huduma
zitakuwa bora zaidi na msongamano wa wagonjwa hospitalini hapo utakuwa
umemalizika. Ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma
unaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika mwaka 2014. Hospitali hiyo
itatumika kufundishia wanafunzi wa udaktari na uuguzi.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu pia, tumekamilisha matayarisho ya
kuanza ujenzi wa hospitali kubwa na ya kisasa kabisa kule Mlonganzila, Dar es
Salaam. Ujenzi utaanza Februari 2013 na kukamilika Februari, 2015. Hospitali
hii pia itakuwa ya kufundishia wakati Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
cha Muhimbili kitakapohamishia sehemu kubwa ya shughuli zake huko Mloganzila.
Mchakato wa ujenzi wa Chuo hicho nao unakaribia kuanza. Kuwepo kwa hospitali
hizi kutaongeza sana uwezo wetu wa ndani wa uchunguzi na tiba. Sasa naweza
kuthubutu kusema kuwa safari ya kupunguza wagonjwa tunawaopeleka nje tumeianza
kwa dhati.
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio katika mapambano
dhidi ya magonjwa makubwa yanayosababisha vifo vingi kama vile UKIMWI, Kifua
Kikuu na Malaria. Maambukizi na vifo vinazidi kupungua. Pia vifo vya kina
mama na watoto vinaendelea kupungua.
Kwa mujibu wa taarifa za mwaka huu za Shirika
la Afya Duniani, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano hapa Tanzania
vimepungua kutoka vifo 81 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2009 hadi
kufika vifo 65.2 mwaka 2011 na vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo
51 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2009 na kufikia vifo 45 mwaka
2011. Mafanikio haya yanaiweka Tanzania katika orodha ya nchi 10 zinazofanya
vizuri duniani katika kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka
mitano.
Ndugu Wananchi;
Hatuna budi kufahamu kuwa haya ni matokeo ya
kufanya vizuri kwenye chanjo kwa watoto ambayo imefikia wastani wa asilimia 90.
Pia imechangiwa na mafanikio yetu katika kupunguza maambukizi ya malaria na
UKIMWI kwa watoto. Naamini tutapata mafanikio makubwa zaidi kuanzia mwaka 2013
tutakapoanza chanjo dhidi ya kichomi (pneumonia) na ugonjwa wa kuharisha kwa
watoto chini ya umri wa miaka mitano. Aidha, tukiendelea kutekeleza kwa dhati
mpango wa kila mtoto kulala kwenye chandarua kilichotiwa dawa na ule Mpango
Kabambe wa Kuzuia Maambukizi ya Mama Kwenda kwa Mtoto niliouzindua kule Lindi
tarehe 1 Desemba, 2012, mambo yatakuwa vizuri zaidi.
Sensa ya Watu
na Makazi
Ndugu wananchi;
Leo
asubuhi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja nilitangaza matokea ya Sensa ya Watu na
Makazi iliyofanyika mwezi Agosti, mwaka 2012. Matokeo haya yanaonyesha kwamba
idadi ya watu nchini Tanzania ni milioni 44,929,002 kati yao watu milioni
43,625,434 wanaishi Tanzania Bara na milioni 1,303,568 wanaishi Zanzibar.
Ukilinganisha na Sensa ya mwaka 2002 tulipokuwa na watu milioni 34.4, hili ni
ongezeko la watu milioni 10.5 au wastani wa asilimia 2.6 kwa mwaka.
Matokeo haya yana maana kubwa kwa Serikali na
kwa kila mmoja wetu. Kwa kasi hii ya ongezeko la watu ifikapo mwaka 2016
Tanzania itakuwa na watu milioni 51.6. Hii ni idadi kubwa sana ya watu
inayoleta changamoto kwa Serikali na jamii. Hatuna budi kutambua maana ya idadi
hiyo ya watu na kujipanga vyema kukidhi mahitaji yao na hasa kuhakikisha kuwa
maskini hawaongezeki na huduma zinatosheleza mahitaji na zina ubora wa juu.
Kazi hiyo lazima ianze sasa na ionekane katika Mipango ya Maendeleo.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, sisi wananchi, taarifa hii
inamlazimu kila mmoja wetu atambue kuwa kwa kasi hii, siku za usoni nchi yetu
itakuwa na watu wengi, hivyo ushindani kwa rasilimali utakuwa mkubwa.
Watakaofanikiwa wakati huo ni wale wenye familia ndogo au zile ambazo zimepanga
uzazi. Tukipanga uzazi tunajipa nafasi ya kutunza na kulea vizuri watoto wetu
na kuwapatia mahitaji yao muhimu ya maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kurudia kuwashukuru
wananchi wenzangu wote kwa ushirikiano wenu uliowezesha zoezi zima kufanikiwa
kiasi hiki. Aidha, nawashukuru kwa dhati viongozi, watendaji wakuu na maofisa
wote waliopanga, kuratibu, kusimamia na kutekeleza zoezi la kuhesabu watu.
Natoa shukrani maalum kwa Kamati ya Kitaifa ya Sensa, Kamati za Sensa za Mikoa
na Wilaya, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Jamhuri ya Muungano na Afisi ya Mtakwimu
Mkuu wa Zanzibar na makarani wote wa sensa. Penye nia pana njia. Tumeweza
kushinda changamoto zote na kuwapatia Watanzania nyenzo muhimu ya kupanga
mipango ya maendeleo yao.
Vitambulisho
vya Taifa
Ndugu wananchi;
Mwaka huu tumeanza zoezi la kusajili watu na
makazi kwa ajili ya kuandaa kutoa Vitambulisho vya Taifa kuanzia mwaka 2013.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ilifanya zoezi la majaribio katika mkoa wa Dar
es Salaam na wilaya ya Kilombero ambalo lilifanikiwa. Hivi sasa wanaendelea na
zoezi hilo Zanzibar. Maandalizi kwa ajili ya kutekeleza zoezi la kutoa
vitambulisho nchi nzima kuanzia mwaka 2013 yanakwenda vizuri. Napenda kuwasihi
wananchi wenzangu wakati utakapofika kutoa ushirikiano unaostahili kwa maafisa
watakaohusika na kukusanya taarifa na kutoa vitambulisho ili zoezi lifanikiwe
ipasavyo. Nawaomba muitumie vizuri fursa hii ya kujisajili na kupata
vitambulisho.
Mchakato wa
Katiba Mpya
Ndugu wananchi;
Mtakumbuka kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
nililiyoiunda tarehe 1 Mei, 2012 ilianza kazi yake rasmi tarehe 29 Juni, 2012 na
inaendelea vyema. Mpaka sasa Tume imekamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya
maoni ya mtu mmoja mmoja katika Mikoa yote nchini. Napenda kuchukua nafasi hii
kuwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni. Zoezi linalofuata ni
la kukusanya maoni ya makundi maalumu kuanzia mwezi Januari, 2013. Natoa wito
kwa makundi hayo nayo kushiriki vizuri kwenye hatua hii muhimu. Baada ya hatua
hiyo kukamilika, Tume itaandaa Rasimu ya Katiba ambayo wanategemea itakuwa
tayari mwezi Mei, 2013.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume, rasimu hiyo
itawasilishwa kwenye Vikao vya Mabaraza ya Katiba vitakavyofanyika kati ya mwezi
Juni na Agosti, 2013. Tume itatangaza muundo na namna ya kuwapata Wajumbe wa
Mabaraza hayo na utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili na kutoa maoni juu ya
Rasimu ya Katiba wakati huo ukiwadia.
Baada ya kukamilika kwa Vikao vya Mabaraza ya
Katiba, Tume itakamilisha Rasimu ya Katiba ambayo itachapishwa kwenye Gazeti la
Serikali kama yalivyo matakwa ya Sheria. Aidha, itachapishwa katika magazeti ya
kawaida kwa wananchi kusoma. Mwezi Novemba, 2013 rasimu hiyo itawasilishwa
kwenye Bunge Maalum kujadiliwa na kupitishwa. Baada ya Bunge Maalum kupitisha
Rasimu ya Katiba, Rasimu hiyo itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho
kupitia kura ya maoni.
Ndugu Wananchi;
Matarajio yetu ni kwamba kama kila kitu
kitakwenda kama inavyotarajiwa nchi yetu itakuwa na Katiba Mpya iliyotokana na
maoni na matakwa ya wananchi ifikapo mwaka 2014. Mwaka huo Muungano wetu
utakuwa unatimiza miaka 50 hivyo hiyo itakuwa zawadi ya tunu kubwa.
Tukifanikiwa kupata Katiba mpya wakati huo, tutafanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015 kwa kutumia Katiba hiyo. Inshallah, Mwenyezi Mungu atajaalia baraka zake,
nia yetu njema itatimia. Pamoja na hayo, natoa wito kwenu wananchi wenzangu
kushiriki kwa ukamilifu katika hatua zote za mchakato ili tuweze kujenga muafaka
kuhusu Katiba tunayoitaka.
Marekebisho ya
Sheria
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa
Februari, 2012, nilieleza kwamba katika mazungumzo baina ya Serikali na vyama
vya siasa na wadau wengine juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
tulikubaliana tushughulikie marekebisho ya Sheria hiyo hatua kwa hatua.
Tulikubaliana kuanza na mambo yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya
Wananchi ili Tume iundwe na ianze kazi. Baada ya hapo tuangalie vipengele
vinavyohusu Bunge Maalum na Kura ya Maoni.
Tulifanya hivyo kuhusu Tume ya Katiba na sasa
tunajiandaa kuanza mazungumzo kuhusu ngwe iliyobaki yaani, Bunge Maalum na Kura
ya Maoni. Kama mazungumzo yatakamilika mapema kunako Januari, 2013 mapendekezo
hayo yatafikishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano katika kikao cha Februari
kwa uamuzi. Vinginevyo itakuwa katika Bunge la Aprili, 2013
Ndugu Wananchi;
Kuhusu Kura ya Maoni, Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba inaelekeza kuwa Kura ya Maoni itatungiwa Sheria yake maalum. Ni
matumaini yangu kuwa matayarisho yake yataanza mapema iwezekanavyo. Nawasihi
wananchi wenzangu, viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kijamii tuwe
watulivu, tuendelee kushirikiana katika mchakato huu wa Katiba mpaka tulifikishe
jahazi ufukweni salama kwa mustakabali mwema wa nchi yetu na watu wake.
Mfumo wa
Dijitali
Ndugu wananchi;
Bila ya shaka mtakumbuka taarifa za Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Mawasiliano kwamba kuanzia tarehe
1 Januari, 2013 nchi yetu itahamia katika mfumo wa mawasiliano unaotumia
teknolojia ya dijitali (au kidijiti kwa tafsiri ya BAKITA) badala ya huu wa sasa
wa analojia. Uamuzi huu unakuja kufuatia uamuzi wa kimataifa kwamba nchi zote
duniani ziwe zimeingia kwenye mfumo huu ifikapo mwaka 2015. Pia unazingatia
uamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa nchi zetu kuanza safari hiyo tarehe 1
Januari, 2013.
Hapa nchini zoezi hili litafanyika kwa awamu.
Litaanza katika mikoa saba ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya,
Kilimanjaro, Mwanza na Tanga na mingine itafuata kwa mujibu wa ratiba
itakayopangwa.
Ndugu Wananchi;
Teknolojia ya dijitali katika mfumo wa
mawasiliano hufanya picha za televisheni kuwa nzuri na hazina chenga chenga.
Mawasiliano ya simu yatakuwa mazuri zaidi. Vile vile, itakuwa rahisi kupata
huduma za televisheni kwenye simu za mkononi na huduma ya intaneti kwenye
televisheni.
Ndugu Wananchi;
Ili kuweza kutumia teknolojia hii, kila
televisheni inatakiwa iwe na kifaa kiitwacho king’amuzi. Vifaa hivi vipo kwa
wingi madukani na wengine tayari wanavyo. Naomba niwatoe hofu kwamba kwa kuingia
katika mfumo huu siyo lazima kununua televisheni mpya. Televisheni yo yote yenye
vitundu vitatu vya rangi za njano, nyeupe na nyekundu itaweza kufanya kazi
kwenye mfumo wa dijitali. Hata wale ambao hawana televisheni za namna hiyo
wanaweza kununua kifaa cha kuunganishia king’amuzi na mambo yakawa mazuri.
Uhusiano wa
Kimataifa
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2012, uhusiano wetu na washirika
wetu wa maendeleo ulikuwa mzuri na uliendelea kuimarika. Wote wanaridhika na
kusifu kazi nzuri inayofanywa na Serikali yetu na ndiyo maana wanaendelea
kushirikiana nasi na kutoa misaada ya maendeleo. Aidha, wameonesha nia thabiti
ya kuendelea kushirikiana nasi na kutusaidia katika harakati zetu za kujiletea
maendeleo.
Napenda kutumia nafasi hii kwa niaba yenu nyote
kutoa shukrani za dhati kwa washirika wetu wa maendeleo kwa mchango mkubwa
wanaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi yetu. Nawahakikishia kuwa tunathamini
sana ushirikiano wao na misaada yao na tutafanya kila tuwezalo kudumisha
ushirikiano baina yetu.
Mkutano wa
Smart Parntership
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu nchi yetu ilipata bahati ya kuwa
mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kikanda na kimataifa. Mikutano hiyo ni pamoja
na Mkutano Mkuu wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Mkutano wa
Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mkutano Mkuu wa Shirika la
Kimataifa la Chanjo (GAVI) na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC.
Bahati nzuri mwaka 2013 Tanzania itakuwa
mwenyeji wa mikutano mingine ukiwemo ule wa Global 2013 Smart Partnership
Dialogue utakaofanyika Dar es Salaam kuanzia tarehe 24 – 28 Mei, 2013. Huu ni
mkutano unaohusisha nchi nyingi duniani na kutoka takriban mabara yote. Mkutano
huu hukutanisha na kushirikisha viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Nchi na
Serikali, viongozi wa sekta binafsi wakiwemo wa makampuni makubwa ya kimataifa,
wasomi na wawakilishi wa asasi za kiraia na watu binafsi.
Kwa kawaida katika mkutano kama huu huwepo
agenda maalum, aghalabu kuhusu masuala ya uchumi, biashara na maendeleo.
Mkutano wa mwaka 2013 utazungumzia “Matumizi ya Sayansi na Teknolojia kwa Ajili
ya Maendeleo ya Afrika” (Leveraging Science and Technology for Africa’s
Development). Kwa kweli ni kipaumbele muafaka kabisa, ndiyo maana na sisi
tumefarijika kuukaribisha.
Ndugu Wananchi;
Kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu wa
watu zaidi ya 500 mashuhuri, ni heshima kubwa kwa nchi yetu. Ni nafasi nzuri ya
kuitangaza Tanzania na fursa zake za uwekezaji, biashara na utalii. Pia, ni
nafasi nzuri kwa wafanyabiashara wetu kutangaza shughuli zao na fursa za
biashara na uwekezaji wanazotaka kushirikisha wafanyabiashara wa nje. Naomba
tuitumie vyema fursa hiyo adimu kwa manufaa ya taifa na ya waanyabiashara wetu.
Tuwaonyeshe wageni wetu upendo na ukarimu kama ilivyo sifa yetu Watanzania ili
waondoke na kumbukumbu nzuri za nchi yetu na watamani kurudi tena kutembea au
kuwekeza.
Hitimisho
Ndugu wananchi;
Tunatarajia
kuwa mwaka 2013 utakuwa mwaka wa mafanikio makubwa zaidi katika nyanja zote
kuzidi mwaka 2012. Mambo yaliyokwama mwaka 2012 yatakwamuliwa. Ajira
zitaongezeka kwa uwekezaji vitega uchumi kuongezeka na kuwajengea uwezo
wajasiriamali wazalendo, ili waweze kujiajiri wenyewe na kuajiri wengine. Kwa
ajili hiyo, Mifuko ya kusaidia wajasiriamali wadogo, wanawake na vijana
itafufuliwa na kutengewa fedha nyingi katika bajeti ya Serikali.
Mwaka 2013 ni mwaka wa matumaini, hivyo kila
mmoja wetu anatakiwa kujituma na kutimiza wajibu wake. Maisha bora yatakuja kwa
kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake ipasavyo. Kama kila mtu atafanya kazi kwa
bidii na maarifa, na, kama kila mmoja wetu atajivunia matokeo ya kazi yake na
siyo uhodari wa maneno yake ya uchambuzi wa hali. Kila mtu achukie uvivu na
tabia ya kulalamika pasipo kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Mimi
na wenzangu Serikalini tunawaahidi ushirikiano wa hali ya juu na kwamba
tutawatumikia kwa moyo wetu wote, kwa nguvu zetu zote na kwa maarifa yetu yote.
Tunataka kukidhi matarajio na imani ya wananchi kwa Serikali yao. Tutaendelea
kuimarisha utendaji kazi Serikalini na kuhimiza uwajibikaji katika ngazi zote za
uongozi. Tutaendeleza mapambano dhidi ya rushwa bila ajizi na watumishi wasio
waaminifu, wazembe, wabadhirifu wa mali ya umma watawajibishwa ipasavyo.
Wananchi pia wanao wajibu wa kuwa raia wema na wazalendo wa kweli kwa nchi yao.
Kila mmoja wetu ajiulize ataifanyia nini jamii yake na nchi yake badala ya
kuuliza itamfanyia nini.
Ndugu zangu,Watanzania Wenzangu;
Nawatakieni
nyote heri na fanaka tele katika mwaka mpya wa 2013. Tusherehekee pamoja kwa
amani na utulivu.
Mungu Ibariki
Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania!
Asanteni
sana kwa kunisikiliza.
Post a Comment