Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Arusha wakiwa katika kazi zao za kila siku
……………………………………………………………..
NA GLADNESS MUSHI WA FULLSHANGWE-HANANG
JAMII nchini imeaswa kutumia ipasavyo fursa zilizopo na zinazotolewa na Serikali au mashirika mengine ya ndani na nje ya nchi hususani shirika la kazi duniani (ILO) kwa kuwa wabunifu na kujituma ili waweze kujiendeleza kimaisha.
Hayo yameelezwa juzi mjini Kateshi wilayani Hanang’ mkoani Manyara na Ofisa Maendeleo ya mifugo na uvuvi wa wilaya hiyo Dk Tom Maeda,kwenye uzinduzi wa mpango wa ukuzaji wa ujasiriamali kwa vijana wenye kauli mbiu moto wa nyika. Katika uzinduzi huo ulioandaliwa na asasi ya Disabled and Orphans Hope Centre (Dohoce) ya wilayani Hanang’ kupitia shirika la kazi duniani (ILO) Dk Maeda alisema huu ni wakati wa wajasiriamali nchini kuchangamikia fursa zilizopo.
Alisema wilaya hiyo ni sehemu ya jumuiya ya watanzania wenye kuwajibika kutekeleza malengo ya milennia na dira ya Taifa ya mwaka 2025 na mkakati wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini (Mkukuta) namba mbili.
Naye,Mratibu wa Dohoce,Kianga Mdundo alisema takwimu zilizotolewa na Waziri wa kazi na ajira Dk Makongoro Mahanga,zinaonyesha kuwa watanzania walioajiriwa kwenye sekta rasmi ni asilimia 30,ajira Serikali asilimia tano,sekta zisizo rasmi asilimia 35 na wasio na ajira asilimia 30.
Mdundo alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya mahesabu ya mashirika ya umma,Zitto Kabwe alisema wahitimu wa vyuo vyote nchini kwa mwaka ni 650,000 na wanaopata ajira ni 40,000 na 610,000 waliobaki wanakosa ajira.
Kwa upande wake,mwezeshaji wa mafunzo hayo Julius Slaa alisema kada zilizopatiwa mafunzo hayo na kupatiwa cheti ni mafundi wa ushonaji,seremala, magari,pikipiki,waashi,mamalishe,wakulima,wafugaji na wasindikaji vyakula.



Post a Comment