SERIKALI ya Japan imepatia
Tanzania msaada wa shilingi bilioni 28.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
mitatu ya uboreshaji wa usafiri jijini Dar es salaam na kilimo hapa
nchini.
Msaada
huo umesainiwa (leo) jijini Dar es salaam na Balozi wa Japan hapa
nchini Masaki Okada kwa niaba ya Japan na Waziri wa Fedha Dkt. William Mgimwa
kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya
kusaini msaada huo Waziri wa Fedha Dkt . Mgimwa alisema kuwa mradi wa kwanza
utahusisha upanuzi wa barabara ya Kilwa na ile ya Bandari ambapo jumla ya
shilingi bilioni 20 zitatumika katika kukamilisha mradi
huo.
Aliongeza kuwa mradi
mwingine ni ule wa ujenzi wa barabara za juu(flyover) katika makutano ya TAZARA
ambapo jumla ya shilingi bilioni moja (1) na milioni 26 zinatarajiwa kutumika
katika kukamilisha mradi huo.
Dkt. Mgimwa aliongeza kuwa
eneo lingine ambalo litanufaika na msaada kutoka Japan ni kuunga mkono sera ya
Kilimo kwanza ambapo Tanzania imepata shilingi bilioni sita(6) na milioni 92 kwa
ajili ya kuhakikisha kunakuwepo kwa usalama wa chakula cha kutosha katika maeneo
mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuwa upande wa
eneo hilo lengo ni kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wa kipato cha chini
wanaboresha kilimo ambacho kitawahakikisha uhakika wa chakula wakati wote na
hivyo kuondokana na umaskini.
Kwa upande wa Balozi wa
Japan hapa nchini Masaki Okada alisema kuwa wananchi wengi wa Tanzania hasa
wakazi wa Jiji la Dar es salaam wamekuwa wakisubiri kwa hamu barabara za juu ili
kusaidia kupunguza msongamano wakati wa kuja na kutoka katikati ya jiji la Dar
es salaam.
Alisema kuwa utakapo
kamilika mradi huo utasaidia kupunguza tatizo la msongamano na hivyo kupunguza
saa za mwananchi kusafiri kuja na kutoka katikati ya jiji la Dar es
salaam.
Balozi Okada alisema kuwa
hatua hii itakuwa muhimu katika kukuza uchumi kwani wananchi watakuwa na muda wa
kutosha kuzalisha mali kutoka na miundombinu kuruhusu magari kwenda kasi pasipo
kikwazo.
Post a Comment