NaBaltazar
Nduwayezu,EANA
Zaidi ya watu 1,000 kutoka
Afrika Mashariki na sehemu nyingine duniani wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa
wa siku tatu wa Nishati ya Petroli na Maonyesho utakaofanyika mjini Arusha, kati
ya Februari 6 na 8, 2013.
‘’Lengo kuu la Mkutano na
Maonyesho ni kukuza uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi kwa kuionyesha
dunia rasilimali ya nishati hiyo iliyopo katika kanda na kubadilishana taarifa
juu ya hali ya uendelezaji wa sekta hiyo katika kila nchi mwanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC),’’ Dk. Nyamajeje Weggoro,Mkurugenzi wa Tija na Sekta
ya Jamii wa EAC aliwaambia waandishi wa habari hapa juzi.
Aliongeza kwamba mkutano
huo utatoa mada mbalimbali za kiufundi zinazoonyesha maendeleo ya sekta ya
mafuta ya petrol na gesi katika EAC na duniani kwa ujumla wake.
‘’Hii ni nafasi ya kipekee
kwa Afrika Mashariki kuonyesha ugunduzi wa hivi karibuni wa uwepo wa mafuta na
gesi na kuona ni namna gani bora ya kuweza kuchimba rasilimali hiyo katika nchi
wananchama,’’ alisema Dk. Weggoro. Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi na
Rais Jakaya Kikwete.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni
: ‘’Kanda ya Afrika Mashariki,eneo linaloibukia kwa uwekezaji na upatikanaji wa
mafuta na gesi kwa siku za usoni kwa maendeleo endelevu.
‘’Tumechagua kauli mbiu
hiyo kwa sababu upo ugunduzi mkubwa wa mafuta na gesi katika miaka miwili
iliyopita Magharibu mwa Uganda na katika maeneo mengine,ugunduzi wa gesi Kusini
mwa Tanzania na ukanda wa Pwani, ugunduzi mkubwa wa mafuta Kaskazini mwa Kenya
na gesi pia ukanda wa Pwani wa Kenya,’’ alieleza Dk. Weggoro na kuongeza ‘’hali
hii imeifanya kanda hii kuwa na mvuto wa aina yake kwa wawekezaji kutoka duniani
kote.’’
Wajumbe waliothibitisha
kushiriki katika mkutano huo ni pamoja na viongozi wa biashara katika sekta ya
nishati,mawaziri wa shughuli za EAC, mawaziri wanaoshughulikia nishati, fedha
na mipango toka nchi tano za EAC na sekta nyingine muhimu, wawakilishi toka
sekta binafsi, bodi mbalimbali za kitaaluma, vyuo vikuu na kampuni kubwa za
uchimbaji petroli na gesi.
Mkutano huo wa Afrika
Mashariki wa Nishati ya Petroli unaofanyika kila baada ya miaka miwili
ulizinduliwa rasmi mwaka 2003 na unafanyika kwa mzunguko miongoni mwa nchi
wanachama
Post a Comment