Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MAKAHABA WAWAGONGANISHA MA-RPC JIJINI DAR ES SALAAM.


 

Mmoja amshangaa mwenzake kuwakamata machangudoa, Asema anawakamata kwa sababu hana elimu ya madanguro, Mwenzake ajibu, huyu ana miezi sita hapa, haya anayatoa wapi ?.

Kamanda wa polisi kanda maalumya Dar es Salaam, Seleman Kova.


MAKAMANDA wawili wa polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wamekwaruzana.

Makamanda hao, Charles Kenyela wa Mkoa wa Kinondoni na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, wamekwaruzana na kurushiana maneno yasiyofaa kuhusu namna ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.

Kutofautiana huko kumeibuka baada ya wiki iliyopita, Kamanda Kenyela kufanya operesheni ya kuwakamata wanawake wanaofanya biashara ya ukahaba, maarufu kama machangudoa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Baada ya Kamanda Kenyela kuendesha operesheni hiyo, Kamanda Kiondo wa Temeke, alinukuliwa na vyombo vya habari jana, akikosoa zoezi hilo na kusema hakuna sheria nchini inayozuia mwanamke kujiuza.

Katika maelezo yake, Kamanda Kiondo alisema, operesheni hiyo ilifanywa kwa kukurupuka na kwamba kamanda huyo hajasomea elimu ya jamii juu ya madanguro.

Kwa mujibu wa Kamanda Kiondo, kama Kamanda Kenyela angekuwa anaielewa vizuri elimu hiyo, kamwe asingedhubutu kuwakamata wanawake hao bali angewapatia elimu na ushauri dhidi ya maradhi wanayoweza kuambukizwa.

Pamoja na hayo, alihoji kuna umuhimu gani wa kuwakamata machangudoa wakati hakuna sheria inayomtaka awafikishe mahakamani badala yake anayetakiwa kushitakiwa ni mtu anayetoa nyumba ili itumike kama danguro.

Naye, Kamanda Kenyela alipozungumza na MTANZANIA jana juu ya kauli za kejeli zilizotolewa na mwenzake huyo, alisema amestushwa na taarifa ya Kamanda Kiondo kwa kuwa amemdhalilisha kupitia vyombo vya habari.

“Yaani mwandishi sipati picha kama Kamanda Kiondo ambaye hana miezi sita kwenye nafasi hiyo tangu ateuliwe, anaweza kunidhalilisha juu ya utendaji wangu wa kazi, kwanza inakuwaje azungumzie mambo ya Kinondoni wakati mimi nipo?

“Kama alijua nimekosea, alipaswa kunipigia simu kwanza tushauriane kabla ya kusema kwenye vyombo vya habari au angenisema kwa wakubwa wetu ambao wangeniita na kunishauri ili nisitishe operesheni hiyo, kama kweli ninakwenda kinyume.

“Amenidhalilisha sana na unajua ni vigumu kwa kamanda kama yule kutoka kwenye himaya yake na kuzungumzia himaya ya kamanda mwingine wakati mhusika yupo.

“Kibaya zaidi anasema eti mimi sina elimu ya jamii juu ya madanguro, lakini binafsi siwezi kuona vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani au usumbufu kwa raia wengine, halafu nikakaa kimya, sitaacha kuchukua hatua.

“Ninachoweza kumwambia Kamanda Kiondo ni kwamba, sina ugomvi naye na pia sitaki malumbano naye, kazi ya kudhibiti uhalifu haihitaji mpango mmoja lazima tutumie njia mbadala kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu ya kulinda raia na mali zao, nafikiri suala hilo linazungumzika tuache litapata suluhisho,” alisema Kamanda Kenyela akionyesha kukerwa na kauli za Kamanda Kiondo.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top