Jengo la Dakhalia ya Chuo cha Kilimo Kizimbani
likionekana katika mandhari nzuri na ya kupendeza.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi akipanda mti kama kumbukumbu mara baada ya kuizinduai dakhalia ya Chuo cha
Kilimo Kizimbani Wilaya ya Magharibi.
Makamu wa Pili wa Raiswa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akizindua Dahalia ya chuo cha Kilimo kizimbani ikiwa ni shamra shamra za
maadhimisho ya kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Mkurugenzi wa Chuo cha Kilimo Kizimbani Nd. Mohd
Khamis Rashid akimpatia Balozi Seif zawadi ya ndizi bora aina ya Mkono
Mmoja iliyolimwa kitaalamu chuoni hapo.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema vijana pamoja na wanafunzi wa Zanzibar
wana fursa nzuri ya kupata elimu ya juu
hapa hapa nchini kutokana na kuongezeka
kwa vyuo vikuu ili kupunguza gharama zisizo za
lazima.
Alisema utafiti wa
Kitaalamu umebainisha kwamba mwanafunzi anayepata digirii ya kwanza mfano Nchini
Uingereza analazimika kulipiwa zaidi ya shilingi milionio 57,000,000/- fedha
ambazo zinaweza kugharamia wanafunzi kadhaa hapa nchini wakati kiwango na ubora
wa elimu kinafanana.
Balozi Seif alieleza hayo
wakati akiizindua Dakhalia mpya ya chuo cha Kilimo Kizimbani ikiwa ni shamra
shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 49 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya
mwaka 1964.
“ Tumefikia wakati Zanzibar
hakuna sababu kwa
elimu ya diploma na digirii ya kwanza kufuatwa tena nchi za
nje hasa tabia iliyojengeka kwa vijana kwenda Ulaya kwani tayari tumeshakuwa na
vyuo vikuu vinavyotosheleza mahitaji”. Alifafanua Balozi
Seif.
Aliutaka uongozi wa Chuo
cha Kilimo Kizimbani kuongeza juhudi za kutoa Taaluma ili Taifa likidhi mahitaji
ya Wataalamu wa Kilimo ambao hivi msasa wapo 141 wakati mahitaji ni Wataalamu
287 kukiwa na upungufu wa Wataalamu 146.
Balozi Seif alifahamisha
kwamba ujenzi wa dakhalia uliofanywa na chuo cha kilimo ni mabadiliko makubwa
yatakayoiwezesha Zanzibar kuwa na wataalamu wake na kuacha mfumo wa kutegemea
watalaamu wa kigeni ambao wanaibebesha mzigo
Serikali.
“ Nafurahi kuona chuo cha
Kilimo Kizimbani kimezaa dakhalia ikiwa ni ishara ya mabadiliko na mapinduzi
katika sekta ya kilimo ambayo ni tegemezi kwa Uchumi wa Taifa”. Alifafanua
Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uhakika wa Chakula na
Lishe Zanzibar.
“ Mapinduzi ya Kilimo ni vyema yakaenda
sambamba na mabadiliko ya chuo cha Kizimbani”. Aliendelea kusisitiza Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
Amewaomba wanafunzi wa
chuo hicho kujizatiti katika mafunzo yao kwa vile Serikali kupitia Wizara ya
Kilimo imeshawaandalia mazingira bora ya kujipatia Elimu wanafunzi
hao.
Alikumbusha kwamba taratibu
za chuo lazima zifuatwe na wanafunzi hao katika dhana ya kudumisha nidhamu ya
hali ya juu itakayokijengea sifa
nzuri chuo hicho kitaifa na Kimataifa.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya
Kilimo na Maliasili Nd. Afan Othman Maalim alisema katika kukijengea uwezo zaidi
wa kitaaluma chuo cha Kilimo Kizimbani Wizara ya
Kilimo tayari inawaandaa Walimu kumi kupata mafunzo ya ajuu kwa ajili ya
kukiwezesha chuo hicho kutoa elimu ya Digirii ya
kwanza.
Nd. Afan alisema hatua hiyo
imelenga kuondosha tatizo la uhaba wa mabwana na mabibi shamba uliopo ambao
unachangia kudumaza juhudi za wakulima katika uzalishaji wa
Kilimo.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara
ya Kilimo alifahamisha kwamba mpango huo utakwenda sambamba na juhudi za
serikali kupitia wizara hiyo na kwa msaada wa Serikali ya Norway kwa
kujenga dakhalia nyengine kubwa na ya kisasa muda ufupi
ujao.
Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa
dakhalia hiyo pamoja na mikakati ya baadaye ya Chuo Mkurugenzi wa chuo cha
Kilimo Kizimbani Nd. Mohd Khamis Rashid alisema ujenzi wa dakhalia hiyo yenye
vyumba saba na kuhudumia wanafunzi 42 umekuja kutokana na changamoto
iliyojitokeza ya ongezeko kubwa la idadi ya Vijana wanaotaka kujiunga na chuo
hicho.
Alisema mbali ya wanafunzi
wa chuo hicho lakini pia dakhalia hiyo itatumiwa na wakulima wa mafunzo na
muda mfupi kipindi ambacho wanafunzi wa chuo hicho watakuwa
likizoni.
Mapema Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kuangalia maonyesho ya kazi mbali mbali
zinazofanywa na wanafunzi hao likiwemo zaidi suala la utafiti wa ardhi, mazao ya
kilimo na mifugo.
Walimu wa chuo cha Kilimo
Kizimbani wakiongozwa na mwalimu wa mazao katika chuo hicho Bwana Foum Ali Garu
alimueleza Balozi Seif juhudi zinazochukuliwa na chuo hicho katika kuwajengea
uwezo wa kitaalamu wanafunzi hao katika kufanya utafiti kwa
vitendo.
Dakhalia hiyo ya chuo cha
Kilimo Kizimbani imegharimu jumla ya
shilingi Milioni 399,000,000/- na kugharamiwa na Mfuko wa Kimataifa wa
kuendeleza Kilimo { IFAD }.
Othman Khamis
Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar
6/1/2013.





Post a Comment