Rais Jakaya Mrisho Kikwete (yumo garini kushoto) akikagua sehemu ya kutua na kupaa ndege ya uwanja wa Tabora leo Januari 10, 2013 mara baada ya kuzindua rasmi ujenzi wake
Waziri wa Ujenzi Dkt John Pombe Magufuli (kulia) na
Waziri wa Uchukuzi Dkt Harrison Mwakyembe wakiongea wakati wa sherehe za
uzinduzi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Tabora leo Januari 10,
2013
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na balozi wa
Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe Radhia Msuya mara baada ya kutua katika uwanja
wa ndege wa Kimataikfa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea mkoani
Tabora alikokuwa katika ziara ya kikazi ya siku tano kukagua shughuli za
maendeleo na kuzindua miradi mbalimbali
SERIKALI imetangaza hatua
kubwa na kabambe za kufufua usafiri wa abiria na mizigo, ikiwa ni pamoja na
ununuzi wa mabehewa na injini za treni, katika hatua kubwa za aina yake
kuchukuliwa na Serikali kwa muda mrefu katika kurekebisha usafiri wa treni
nchini.
Waziri wa Uchukuzi,
Mheshimiwa Harrison George Mwakyembe ametangaza hatua hizo leo, Alhamisi,
Januari 10, 2013, wakati alipokuwa anamkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuweka jiwe la msingi kwenye
ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Tabora ikiwa ni tukio la mwisho la ziara
yenye mafanikio makubwa ya siku tano ya Rais Kikwete katika Mkoa wa
Tabora.
Mheshimiwa Mwakyembe
amemwambia Rais Kikwete na mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya
uwekaji jiwe hilo la msingi kwenye Uwanja huo kuwa Wizara yake imeanza
kubadilisha reli nyepesi, iliyochakaa na yenye uzito mdogo kwa Reli ya
Kati.
Amesema kuwa kwa kupitia
mashirika yake ya RAHCO na Shirika la Reli Tanzania (TRL) Serikali itafanya
marekebisho hayo makubwa njia mzima ya Reli ya kati na kuwa mafundi wa mashirika
hayo tayari wamefika Mkoa wa Morogoro.
Waziri Mwakyembe amemwambia
Rais Kikwete kuwa Serikali kupitia Wizara yake na mashirika yake hayo, imeagiza
mabehewa mapya ya mizigo 274, imeagiza mabehewa mapya ya abiria 22, imeagiza
mabehewa mapya ya kubebea kokoto 25 na pia imeagiza mabehewa ya breki (brake
vans) 34 na tayari malipo ya awali yamefanyika.
Katika namna
inayothibitisha dhamira ya Serikali kurekebisha hali ya usafiri wa reli nchini,
Mheshimiwa Mwakyembe pia amewaambia wananchi kuwa Wizara yake pia imeagiza crane
mpya na kubwa ya kubebea mizigo yenye uzito unaofikia kilo
100.
Kuhusu injini za treni,
Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa zabuni kwa ajili ya kutengeneza
upya (re-manufacturing) injini
nane za treni imetolewa ili utengenezaji huo ufanyike, iwe ni ndani ama nje ya
nchi.
Pia Waziri amesema kuwa oda
imetolewa kwa ajili ya utengenezaji wa injini mpya 13 za treni ambazo malipo
yake yatafanyika katika mwaka ujao wa fedha hata kama utengenezaji wa injini
hizo utaanza.
Aidha, Waziri amesema kuwa
Wizara kupitia mashirika yake hayo mawili imeagiza spea za kutosha kuweza
kufanya ukarabati mkubwa wa injini tano kwenye karakana zilizoko hapa
nchini.
“Mheshimiwa
Rais, kwa hesabu nyepesi tu ni kwamba katika kipindi kifupi tutaweza kuwa na
injini kiasi cha 26 ambazo zitarudisha uhai wa usafiri wetu wa reli kwa kiasi
kikubwa sana,” Waziri Mwakyembe amemwambia Rais
Kikwete.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
10 Januari,
2013
Post a Comment