Na Boniface
Wambura
MECHI namba
92 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, iliyochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam na kumalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya
African Lyon, imeingiza Sh. 53,756,000.
Watazamaji
9,408 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh.
5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh.
12,499,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh.
8,200,067.80.
Mgawo
mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya Uwanja sh. 6,355,806.33, tiketi sh.
3,183,890, gharama za mechi sh. 3,813,483.80, Kamati ya Ligi Sh. 3,813,483.80,
Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) Sh. 1,906,741.90 na Chama cha Soka
Dar es Salaam (DRFA) Sh. 1,483,021.48.
Katika mechi
hiyo, hadi mapumziko Simba SC walioweka kambi ya wiki mbili Oman kujiandaa na
mzunguko huu, tayari walikuwa mbele kwa mabao 3-0, yaliyotiwa kimiani na Mrisho
Khalfan Ngassa mawili dakika za 19 na 39 na Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’
dakika ya tatu ya mchezo huo.
Redondo
aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya tatu, akiunganisha krosi nzuri ya
Ngassa kutoka wingi ya kushoto na kufumua shuti akiwa katikati ya msitu wa
mabeki wa Lyon.
Bao hilo
liliwatia chaji Simba SC na kuanza kucheza soka maridadi zaidi, wakionana kwa
pasi za mitindo yote, ndefu, fupi, za juu, chini hadi visigino na haikushangaza
dakika ya 19 walipopata bao la pili.
Ilikuwa ni
kazi nzuri ya Ngassa mwenyewe, ambaye baada ya kupata pasi ya Mwinyi Kazimoto
Mwitula aliitoka ngome ya Lyon kabla ya kumchambnua kipa wa timu hiyo, Abdul
Seif.
Baada ya
kufunga bao hilo, Ngassa alikwenda moja kwa moja kwenye benchi la wachezaji wa
akiba na kukumbatiana na Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ kisha kuwapa mikono
wachezaji kadhaa na kurejea uwanjani.
Lyon
walipoteza nafasi nzuri ya kupata bao dakika ya 31, baada ya Shamte Ally
Kilalile kukosa penalti.
Refa Israel
Mujuni alitoa penalti hiyo baada ya beki Paul Ngalema kumkwatua beki Fred Lewis
aliyepanda kusaidia mashambulizi, hata hivyo mkwaju wa kwanza wa Shamte
ulipanguliwa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja, lakini mwamuzi akaamuru irudiwe
kwa madai kipa huyo alitokea kabla ya mpira kupigwa na safari hiyo mpigaji
akapiga nje kabisa.
Simba
iliongeza kasi ya mashambulizi ikitumia mipira ya pembeni, kulia akiteleza
Chanongo na kushoto Ngassa, timu ikichezeshwa vyema na viungo watatu katikati,
Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Jonas Mkude. Ilikuwa burudani kwa mashabiki wa
Wekundu hao wa Msimbazi, kwa jinsi ambayo timu yao ilitawala mchezo.
Kazi nzuri
ya Chanongo aliyeteleza wingi ya kulia huku akiruka madaluga ya mabeki wa Lyon,
iliipatia Simba bao la tatu baada ya krosi yake nzuri kuunganishwa vyema kimiani
na Ngassa.
Baada ya
kufunga, Ngassa alishangilia kwa aina yake bao hilo, kwanza akitambaa hadi
langoni na kisha kujilaza kwenye nyavu kubwa kama yeye ndio
mpira.
Baada ya
hapo, aliinuka na moja kwa moja kwenda tena kwenye benchi la wachezaji wa akiba
akianza kushangilia na Boban, baadaye wachezaji wengine na kocha Jamhuri Kihwelo
‘Julio’, ambaye alitumia kama sekunde 30 akizungumza naye jambo.
Kipindi cha
pili, Lyon walibadilika na kuwabana Simba SC wasiongeze mabao zaidi, huku wao
wakifanikiwa kupata bao la kufutia machozi, lililofungwa na Bright Ike dakika ya
59, pasi ya Fred Lewis.
Dakika ya 64
Ngassa alipoteza nafasi ya kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja, baada ya
kukosa penalti.
Katika mechi nyingine jana, Mtibwa Sugar ililala 1-0 nyumbani mbele ya Polisi
Morogoro, bao pekee la Muzamil Said dakika ya 76, Coastal Union iliifunga
Mgambo JKT 3-1, Ruvu Shooting iliilaza 1-0 JKT Ruvu, bao pekee la Abdulrahman
Seif dakika ya 90 Azam FC imeshinda 3-1 dhidi ya Kagera Sugar na JKT Oljoro
imeilaza 3-1 Toto Africans.
Ushindi wa
Azam ulitokana na mabao ya Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 20 na Khamis Mcha
dakika za 31 na 66, wakati la Kagera lilifungwa na Paul Ngway dakika ya 82 na
sasa timu hiyo imejiimarisha katika nafasi ya pili kwa kutimzia pointi 27, sasa
ikizidiwa mbili tu Yanga iliyo kileleni.
Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga mabao ya Coastal yalifungwa na Philip Mugenzi dakika ya 18,
Daniel Lyanga dakika ya 78 na Joseph Mahundi dakika ya 81, wakati la Mgambo
lilifungwa na Peter Mwalyanzi dakika ya 89.
Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, mabao ya Oljoro yalifungwa na Hassan Isihaka
dakika ya 15, Paul Nonga dakika ya 51 na 57, wakati la Toto lilifungwa na
Selemani Kibuta dakika ya 73.
Ligi hiyo
itaendelea kesho wakati vinara, Yanga SC watakapomenyana na TZ Prisons kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
credits: Bin Zubeiry
Post a Comment