Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi
akizungumza
Baadhi ya wanafunzi wa
Shule ya Sekondari Loyola ya jijini Dar es Salaam wakifuatilia mada mbalimbali
ndani ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Shule ya Sekondari
Loyola.
Baadhi ya wanafunzi wa
Shule ya Sekondari Loyola wakionesha ubunifu wa mavazi katika maadhimisho ya
Siku ya Wanawake Shuleni hapo.
Na Mwandishi wa
Thehabari.com
KAIMU Mkurugenzi Mtendaji
wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi amesema wanawake
wanaweza kuwa viongozi wazuri na mfano wa kuigwa katika maeneo mbalimbali endapo
watajengewa mazingira na kuandaliwa mapema tangu wawapo
shuleni.
Bi. Liundi ambaye pia ni
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya TGNP ametoa changamoto hiyo leo katika
Shule ya Sekondari ya Loyola ya jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi
katika maadhimisho ya siku ya mwanamke shuleni hapo.
Akizungumza na umati wa
wanafunzi wasichana wa shule hiyo na wageni anuai waalikwa, alisema tafiti
nyingi zilizofanywa zinaonesha kuwa wasichana wanapoandaliwa mazingira mazuri ya
elimu wanafanya vizuri ukilinganisha na wavulana.
Aidha aliongeza kuwa kwa
sasa zipo shule zinazochukua wasichana pekee ambazo zimekuwa zikifanya vizuri
zaidi jambo ambalo linaonesha wazi mazingira mazuri yakijengwa jamii hii inaweza
kuinuka na kuwa mfano mzuri.
Alisema kwa sasa vishawishi
na changamoto anuai zilizopo katika shule nyingi ndio kikwazo kwa wanafunzi wa
kike kufanya vizuri, hali ambayo ikifanyiwa kazi kiufasaha mabadiliko
kimafanikio kwa kundi hilo yanaweza kutokea.
Hata hivyo alisema tafsiri
iliyojengeka ya kwamba wanafunzi wa kike wanaogopa masomo ya sayansi si sahihi
kiuhalisia, kwani mazingira ambayo wanafunzi hawa wanakumbana nayo ndio kikwanzo
katika mafanikio yao kimasomo.
“Mfano shule nyingi za kata
ni za kutwa wanafunzi hasa wasichana wanakaa mbali na shule, wanalazimika
kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni…wanakumbana na changamoto nyingi
njiani hivyo wanajikuta wanashindwa kufanya vizuri au kukatishwa kabisa masomo
yao,” alisema Bi. Liundi.
Aliongeza kuwa eneo kama
hili, vyombo husika vikiangalia sheria na sera zinazojenga mazingira mazuri kwa
makundi yote, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika
vizuri wasichana wanaweza kuingia katika ushindani kwa fursa
zilizopo.
Kwa upande wake mwanafunzi
Grace Ntambi wa kidato cha tano wa shule hiyo aliiomba serikali kuendelea kutoa
elimu kwa mikoa ambayo bado inaendeleza mila potofu za kumbagua mtoto wa kike
ikiwa ni pamoja na kuelemea kwenye mfumo dume, ili kuangamiza vitendo
hivyo.
“Na hii ianzie pia katika
ngazi za familia kuna kila sababu ya kuondokana na mila potofu za kwamba mtoto
wa kike hana haki ya kupata elimu kama ilivyo kwa mtoto wa kiume…tuwatie moyo
wasichana kwani wanaweza,” alisema mwanafunzi huyo.
Katika hafla hiyo pia TGNP
ilipata fursa ya kutoa mada mbalimbali za masuala ya wanafunzi kujitambua kwa
hatua anuai ikiwa ni pamoja na kutoa ushuhuda ya kwamba wanawake wanaweza
wakiamua kufanya hivyo kwa kila hatua wanayopiga.
Imeandaliwa na Mtandao wa
Thehabari.com (www.thehabari.com)
Post a Comment