Na Akili Philipo
"…Kwa hiyo jambo mojawapo lililo ndani ya Serikali ni
kukataa makuu ya Nchi bila ya kuwepo maisha bora kwa raia wake, na pia kukataa
kutafuta utajiri wa kuchezea. Ndiyo kuikubali imani kwamba kuna vitu vingine
vingi vyenye maana zaidi maishani kuliko kujaza utajiri, na kama kutafuta
utajiri kunakwenda kinyume cha vitu kama heshima ya binadamu, au usawa wa hali
ya maisha, basi jambo litakarofikiriwa kwanza litakuwa heshima na usawa wa
binadamu. Maana katika nchi ya Tanzania, Serikali imeanza kutimiza shabaha ya
utaratibu wote wa maisha, uchumi na siasa, lazima iwe binadamu; yaani raia,
raia wote, wa nchi hii. Kuongeza mali ni jambo zuri, na ni wajibu wetu kuongeza
mali. Lakini faida ya mali hiyo itatoweka wakati itakapokoma kuwatumikia watu
na kuanza kutumikiwa na watu. Katika hali yetu ya sasa ya uchumi, jambo hili
linaweza likaonekana kama jambo la vitabuni tu; lakini kwa kweli ni jambo kubwa
sana. Kwa sababu tunasema kwamba kuna baadhi ya vitendo ambavyo tutakataa kufanya
au kuvikubali, kila mtu binafsi au Taifa zima, hata kama matokeo ya vitendo
hivyo vingeleta maongezeko ya uchumi. Kwa mfano, hata kama ni kweli kwamba
yangepatikana maongezeko makubwa sana ya hesabu ya utajiri wa nchi na mapato ya
watu wetu walio wengi, kama nchi ya nje, au mabepari wangelima mashamba
makubwa, wangeleta, au kuanzisha makampuni au kujenga viwanda vikubwa na
vidogo, n.k. (na mimi nina shaka na ukweli huo), bado tungekataa mapendekezo
hayo. Tungeyakataa kwa sababu ya matokeo yake kwa uhuru wetu, na kwa sababu
idadi kubwa ya watu wetu watapata ujira mdogo sana, watakuwa vibarua wa nchi nyingine au wa mtu mwingine. Katika hali hiyo
riziki na maisha yote ya watu wa Tanzania yatakuwa mikononi mwa nchi nyingine
au watu wachache. Lo lote katika haya mawili halitafanana na uamuzi wetu wa
kuulinda uhuru wa Tanzania, na uhuru na usawa wa raia wake wote. Lakini hayo
maana yake si kusema kwamba tumekubali hali tulio nayo hivi sasa; hata kidogo.
Serikali inataka watu wafanye juhudi kubwa kuinua hali ya maisha yao. Tunasema
kwamba mambo yaliyozichukua nchi kubwa miaka mia nyingi kutimiza, sisi
tutachukua miaka michache tu. Tunachojitahidi kufanya ni kufanya mapinduzi ya
haraka ya maisha yetu na uchumi wetu. Hili si jambo lisilowezekana kwa
binadamu. Imechukua miaka mamia ya milioni kwa maisha ya ulimwengu kubadilika
kutoka katika hali ya vidudu kufikia hali ya juu ya maisha yaani binadamu.
Lakini mimba inapita katika hatua zake zote mnamo miezi tisa tu. Kuongezeka kwa uchumi wa Taifa letu
kunaweza kukaharakishwa, na bado kukabaki kuwa ni kwetu. Itachukua zaidi ya
miezi tisa, lakini wananchi wakitumia raslimali zao, ardhi yao kwa kutumia
ujuzi uliopo wa karne hii, tuna hakika ya kupunguza sana muda ambao nchi kama
Uingereza au Marekani zimechukua kufikia hali yao ya sasa. Wananchi wa Tanzania
wenyewe tu ndio wanaoweza kuwa na dhati ya kutosha kuijenga Tanzania, kwa faida
ya Watanzania; na ni Watanzania tu ndio wanaoweza kusema faida hizo ni zipi,
kwa hiyo hatuna budi kujitegemea sisi na amali yetu wenyewe katika kuleta
maendeleo. Amali hizo ni ardhi, na watu, fikira zetu zielekezwe katika vitu
tulivyo navyo, au vinavyoweza kupatikana, kwa gharama ndogo, na ambavyo
vinaweza kutumiwa na wananchi. Tukiendelea kwa njia hii tunaweza kuepuka
kuharibu utaratibu na kuepuka shida za binadamu. Wakati huo huo tunaweza
tukajenga viwanda na huduma katika vijiji, ambako ndiko watu wengi waliko, na
hivyo tukasaidia kuendeleza uchumi vijijini. Kwa njia hiyo watu wengi zaidi
wanaweza kupata maongezeko ya mapato yao, badala ya kukazania kuongeza uchumi
uliomo mikononi mwa watu wachache. Fedha tulizo nazo lazima zitumiwe kuleta
faida kubwa, katika kununua mbolea, vitu muhimu kwa maendeleo, kuwakopesha watu
wanunue ng’ombe wazuri, kuboresha, kuzalisha amali; katika kuunda utaratibu
bora zaidi wa uchumi, na vitu vingine kama hivyo. Mambo hayo yataleta
maongezeko makubwa katika pato la mwananchi. Wala maneno haya maana yake siyo
kwamba hakutakuwa tena na maendeleo ya mijini, au kwamba sasa hatutajenga
viwanda vipya. Watu wengi wanapoishi pamoja, huduma Fulani huwa za lazima kwa
sababu ya afya na usalama wa watu. Tutakuwa wajinga tukisahau miji, ambayo
ndiyo inayotoa huduma za kusaidia vijiji vinavyoizunguka. Viwanda
vinavyoifaidia nchi nzima lazima vijengwe katika sehemu zinazofaa. Lakini hata
wakati tunapojenga viwanda vinavyoifaidia taifa zima, hatuna budi kufikiria
kama ni lazima kwetu kutumia mitambo ya kisasa. Hatuna budi kufikiria kama
mitambo ya aina ya zamani, inayohitaji wafanya kazi wengi zaidi, wasiohitajiwa
kuwa na ufundi mkubwa, haiwezi kutufaa kutimiza haja yetu, na vile vile gharama
yake tukaimudu. Lakini ziko njia mbili ambazo kwazo wito wetu wa kujitegemea
umeeleweka vibaya, au watu wamekataa kuuelewa makusudi. Kujitegemea maana yake
siyo kujitenga ama katika mambo ya uchumi, ama katika mambo ya siasa. Maana
yake ni kwamba tutajitegemea wenyewe, hatuwategemei watu wengine. Lakini kusema
hivyo si sawa na kusema kwamba hatutafanya biashara na watu wengine, au kwamba
hatutashirikiana nao, kama ushirikiano huo unatuletea faida. Ni dhahiri kwamba
tutafanya hivyo; lazima tutaendelea kuuza bidhaa zetu za kutosha katika nchi za
nje kutuwezesha kulipia vifaa tunavyovipata. Mpaka sasa hivyo ndivyo Tanzania
inavyofanya; na kwa kweli, kwa miaka mingi sana thamani ya bidhaa tulizouza
imekuwa ni kubwa zaidi kuliko ile ya vitu tulivyo nunua kutoka nchi za nje.
Lazima vitu tunavyonunua viendelee kuwa vile ambavyo ni muhimu kwa maendeleo
yetu, muhimu kwa maendeleo na maisha ya watu wetu wote, na ambavyo sisi wenyewe
hatuwezi kuvitengeneza. Mpaka sasa tumekuwa tukinunua kutoka nchi za nje vitu
vingi ambavyo tungeweza kuvipata mumu humu nchini kwa juhudi kidogo tu. Vitu
hivyo ni kama chakula au vitu vya anasa vinavyowafanya watu wetu wachache
watamani mambo ambayo hawataridhika nayo kamwe. Yaani kujitegemea
hakutatupunguzia biashara yetu na mataifa mengine ulimwenguni. Mambo mengine
kuhusu kujitegemea ambayo ni muhimu kuelewa ni kwamba Tanzania haikusema kwamba
haitaki msaada kutoka katika nchi za nje kwa kazi zake za mendeleo. Tutaendelea
kupokea misaada kutoka nchi za nje kwa ajili ya mipango maalum, au kama
inasaidia maendeleo kwa ujumla, basi lazima tupate fedha na wataalamu walio
wengi kutoka katika nchi za nje, kutimiza mipango ambayo itaifanya juhudi yetu
kuwa na maana zaidi: mahali ambapo mpango huo unasaidia kazi zingine za
Tanzania. Hiyo ndiyo sababu iliyofanya Serikali itamke wazi kwamba
tutakaribisha misaada kutoka nchi za nje, kama misaada hiyo ni ya Serikali ama
ni ya watu binafsi, katika kujengea aina nyingi mbali mbali za viwanda, hasa
viwanda vinavyotengeneza vifaa vya kutumia, au kusafisha mazao yetu kabla ya
kuuza. Misaada ya elimu ya aina zote ni aina moja ya misaada mingi yenye
kutufaidia ambayo nchi za nje zinaweza kutoa, mradi tu msaada huo unafanana na
nguvu yetu ya kulipia gharama za kila siku. Lakini jambo lililo muhimu ni
kwamba haifai sisi Watanzania kuwa na mawazo kwamba hakuna cho chote
tunachoweza kufanya mpaka kwanza mtu mwingine ametupatia fedha. Jambo la maana
kwetu ni kiasi tutakachofanikiwa katika kumzuia mtu asimnyonye mwenzake, katika
kueneza mtindo wa kufanya kazi pamoja kwa faida ya wote badala ya kila mtu
kushindania faida yake binafsi; lakini lililo muhimu zaidi ni kuhakikisha
kwamba tunapanua uchumi wetu bila ya kupanua nafasi za mirija ya wanyonyaji. Shabaha
yetu haina budi iwe kupata maendeleo kwa njia ambayo itahakikisha kwamba
tunatumia utaalamu na maarifa yote ya kisasa, lakini bila ya kueneza ubepari.
Maana yake ni kwamba katika Tanzania hatuna budi kulinda na kuimarisha
utaratibu wetu wa demokrasi. Lazima tufikie hali ambapo kila mwananchi
anahusika katika mambo ya Serikali yake ya kijiji, mtaa na wakati huo huo
anapata nafasi ya kushiriki katika mambo ya Serikali ya Taifa lake. Maana yake
ni kwamba lazima turekebishe tofauti kubwa ya mapato tulizozirithi kutopka kwa
wakoloni, na kuhakikisha kwamba kila mtu anapokea pato linalolingana na juhudi
yake katika nchi. Lakini wakati huo huo hatuna budi kuwafikiria wale wenzetu
ambao umri wao au udhaifu wa miili yao unawazuia wasiweze kushiriki katika kazi
za uchumi. Vile vile lazima tueneze nafasi sawa kwa wananchi wote, mpaka kila
mtu aweze kushiriki katika kazi za uchumi katika njia anayoimudu… "
“Hiyo ni Sehemu ya Hotuba ya
Rais wa Kwanza wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere katika Chuo
Kikuu Cha Dar Es Salaam.”
Julius Kambarage Nyerere alikuwa
Kiongozi shupavu, makini, mkweli, muaminifu, muhalisia muadilifu, mjuzi na
Mwalimu wa watu wote wa Tanzania, Afrika na Ulimwengu, alitumia maisha yake
yote kuwatumikia watu wote, aliweza kupambana na dhuluma na ubaguzi miongoni
mwa wanadamu, kwa maana hiyo aliweza kupigania haki, uhuru, umoja, usawa, amani
na maendeleo. Nawaomba Watanzania tujitahidi sana kusikiliza na kupata habari
zake, na pia kujifunza na kusoma nyaraka zake nyingi, ama alizoweza kuandika
yeye mwenyewe binafsi, au zilizoandikwa na watu wengine wengi sana, na
zinazoendelea kuandikwa, kwa hakika tutapata elimu kubwa sana, ufahamu mkubwa,
na manufaa mazuri sana, tutaweza kufanya maamuzi makini kwa wakati muafaka,
tutajikomboa na kuleta mabadiliko makubwa katika uhuru wa kiuchumi, kisiasa na
kijamii na kuleta maendeleo na maisha bora kwa watanzania wote. Ninakuomba na ninakusihi
sana tumlilie kwa maombi Mungu Mwenyenzi, ili atuinulie viongozi wenye uwezo,
tabia, haiba na karama kama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na timu yake ili waweze
kutunusuru na hali hii ya hatari ya migogoro, songombingo, sokomoko na mashaka
makubwa, nchini Tanzania, barani Afrika na Ulimwenguni.
Akili Phillipo
E-Mail:phildeak@hotmail.com
Simu Namba:+255(0)754
262270
Post a Comment