Bodi ya Utalii Tanzania  inapenda kuwaarifu wananchi na umma  kwa ujumla kuwa Tanzania  itakuwa ni miongoni mwa nchi ambazo angalau moja ya vivutio vyake kitaingia katika orodha ya Maajabu Saba ya Asili Barani Afrika baada ya kukamilika kwa  upigaji wa kura katika shindano la kutafuta Maajabu Saba ya AsiliBarani Afrika Desemba 31, 2012 na Tanzania kuwa miongoni mwa washindi.
Kampeni ya kutafuta Maajabu Saba ya Asili  ya Bara la Afrika  ilikuwa iikiendeshwa na Taasisi ya  Seven Natural Wonders    yenye makao yake makuu nchini Marekani tangu mwaka 2008 ambapo upigaji wa kura ulihusisha Taasisi za Kimataifa ikiwemo taasisi ya uhifadhi asili wa Mazingira (IUNC) na wataalamu wengine duniani ambao walipiga kura kwa kuzingatia zaidi umuhimu wa asili, upekee na uzuri wa kivutio husika.
Taasisi hiyo ya Seven Natural Wonders imewasiliana na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, Dr. Aloyce Nzuki na kumfahamisha kuhusu matokeo ya awali  na kumthibitishia kuwa Tanzania ni kati ya nchi zilizoshinda na kwamba vivutio vyake zaidi ya kimoja vitakuwa miongoni mwa Maajabu hayo Saba ya Asili Barani Afrika. Tanzania itakuwa mwenyeji wa sherehe za tukio la utangazaji wa vivutio vilivyoshinda katika shindano hili na kwamba itakuwa ni fursa kwa Watanzania na Afrika kwa ujumla kufurahia tukio hilo na Maajbu yatakayoshinda.
Sherehe za utangazaji wa washindi zitafanyika jijini Arusha katika Hotel ya Mt Meru Februari 11, 2013 ambapo watu mashuhuri kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika, na wandishi kutoka vyombo vya habari vya Kimataifa na ndani ya nchi wataalikwa kushiriki katika sherehe hizo na kushuhudia utangazaji wa vivutio vya Tanzania na vingine vya Afrika kuwa Maajabu Saba ya Asili Barani Afrika.
Bodi ya Utalii Tanzania inapenda kuwashukuru watu wote ndani na nje ya Tanzania walioshiriki katika kupigia kura vivutio vya Tanzania. Vivutio vya Tanzania vilivyokuwa katika shindano hili ni  Mlima Kilimnajaro, Bonde la Ngorongoro, na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mwendeshaji
Bodi ya Utalii Tanzania
Jengo la IPS ghorofa ya tatu
Mtaa wa Samora/Azikiwe
S.L.P 2485 D’slaam, Tanzania