Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

BALOZI FOUM AFARIKI DUNIA.

BURIANI BALOZI MOHAMMED ALI FOUM, GWIJI LA DIPLOMASIA NA MZALENDO WA KITANZANIA. 

Mwanzoni mwa Mwezi huu Tanzania ilipata pigo zito mno lislopata mithilika, aliyekuwa Balozi wetu wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa Mzee Mohammed Ali Foum aliiaga Dunia Jijini Cairo Nchini Misri.

Balozi Foum (Juni 4, 1936 - Februari Mosi, 2013) ni Mzalendo wa kupigiwa mfano wa Tanzania ambaye aliitumikia Nchi hii, Afrika na Dunia kwa Ujumla kwa Moyo wake wote na Utumishi wa Kutukuka.

Aliteuliwa na Rais Nyerere kuwa Balozi wetu wa kudumu katika Umoja wa Mataifa Mwaka 1984 na akajitambulisha Rasmi kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Javier Perez de Cuellar Tarehe Septemba 14, 1984 kama anavyoonekana Pichani katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York Nchini Marekani.

Ufuatao ni Wasifu Mfupi wa Mema mengi yaliyotendwa na Balozi Mohammed Ali Foum hapa Duniani ambao nimeuhariri kidogo kutoka kwenye Wasifu wa awali ulioandikwa na Mwandishi Nguli na Gwiji, Bwana Amhed Rajab. Wasifu husika ulikuwa ni sehemu ya Tanzia ya Kifo chake ambao ulichapishwa katika Gazeti la 'Raia Mwema' tolea namba 281 la Mwezi huu.
 
MOHAMMED ALI FOUM: MZALENDO WA KINZANZIBARI NA MSIRI WA NYERERE.

KOMREDI WA KWELI.

Mohammed Ali Foum aliyefariki dunia jijini Cairo Ijumaa usiku, atakumbukwa kama mwanamapinduzi na shujaa aliyepigania "Uhuru wa Zanzibar" na kuchangia mengi katikaM juhudi za kulikomboa Bara la Afrika. Wengi waliokuwa wakimfahamu juu juu, hawakuutambua mchango wake uliokuwa adhimu katika harakati za ukombozi wa Afrika. Hayo si ya ajabu kwa kuwa Foum hakuwa mtu wa kujionyesha na akipendelea kuuficha umahiri wake hasa katika nyanja ya diplomasia.

Nikimfahamu tangu kufungua kwangu macho kwani sote tulizaliwa Vuga, Mji Mkongwe, Unguja. Alikuwa ni mmoja miongoni mwa kaka zetu wa Vuga waliowashajiisha wadogo zao mtaani wawe na moyo wa kuwa pamoja. Mwenzake mmoja katika hili, alikuwa Salim Hakim, ambaye sasa ni mmoja wa mabalozi wanaosifika wa Omani. Baadaye wote wawili walikuwa mabalozi katika Umoja wa Matifa, Foum akiiwakilisha Tanzania na Hakim akiiwakilisha Omani.

Katika miaka ya hivi karihuni wakawa tena pamoja wakiishughulikia Somalia. Foum alikuwa Mwakilishi wa Muungano wa Afrika, na Hakim alikuwa Mwakilishi wa Umoja wa Kiarabu (Arab League). Lakini huko utotoni waliwatia ari watoto wa Vuga waunde timu ya soka ya Young Brothers. Nakumbuka hao wawili na wenzao wa rika lao, walikuwa na tabia ya kuitana kwa kupiga mbinja au mluzi, kama wasemavyo Bara.

Tangu utotoni, Foum alikuwa si mtu wa kukaa nyuma, Daima akipenda kushirikiana na wenzake mtaani na pia skuli. Ingawa hakuwa pocho Foum aliamua kukatiza masomo yake ya sekondari na kuanza kufanya kazi katika Ofisi ya Leba ambako pia akifanya kazi Ahmed Diria Hassan. Baadaye Diria naye atakuja kuwa mmoja wa mabalozi madhubuti wa Tanzania.

Foum alianza kuzivaa siasa alipojiunga na chama cha Hizbu, yaani Zanzibar Nationalist Party (ZNP). Chama hicho kilimpeleka Cuba kwenda kufungua ile iliyokuwa ikiitwa Ofisi ya Zanzibar. Huko alikuwa pamoja na Kanali Ali Mahfoudh na Komredi Salim Ahmed Salim ambao alijiunga nao kwa muda mfupi. Nyumba yao mjini Havana, ambayo pia ilikuwa ni ofisi yao, ilikuwa katika eneo la Vedado ambako wakiishi Wacuba wa tabaka la kati. Sehemu moja ya nyumba hiyo ilikuwa ofisi ya chama cha ANC cha Afrika ya Kusini.

SOGELEA UKOMBOZI.

Foum na wenzake waliwasili Havana si muda mrefu baada ya Fidel Castro na Che Guevara kuuteka mji huo katika Mapinduzi yaliyomwondoa Fulgencio Batista madarakani. Tayari wakati huo Foum alikuwa amekwishaanza kuzikumbatia siasa za mrengo wa kushoto. Huko Cuba pia alikuwa akihudhuria mafunzo ya kijeshi yaliyokuwa yameandaliwa mahsusi kwa vijana Wakikomred kutoka Zanzibar, waliokuwa wakifunzwa namna ya kupindua Serikali.

Baadaye vijana hao pamoja na kina Foum, Ali Mahfoudh na Salim Ahmed walijiunga na chama cha Umma Party cha Abdulrahman Babu na kushiriki katika Mapinduzi ya 1964. Waandishi wa habari kutoka nje waliofika Zanzibar baada ya Mapinduzi na kuandika kwamba walikuwako Wacuba huko, walikuwa kwa hakika wakiwazungumza kina Foum na makomred wenzake waliorejea kutoka Cuba na waliokuwa wakizungumza Kispanyola.

Mwaka 1963 walipokuwa bado Havana, Foum na Ali Mahfoudh waliandika kijitabu kilichoitwa: ‘Forge Ahead To Emancipation’ (Songelea Ukombozi) kilichozungumzia vuguvugu la Zanzibar la kuupinga ubeberu.

Historia ya Umma Party, inaonyesha kwamba Ali Sultan Issa, Foum, Mahfoudh na Salim Rashid ndio waliokuwa wakimshadidia zaidi Babu wakiache mkono chama cha ZNP.

UGWIJI KATIKA DIPLOMASIA, UFASAHA WA MANENO KATIKA KURAI NA UAMINIFU KATIKA KUTUNZA SIRI.

Katika miezi ya mwanzo ya Mapinduzi, Foum alikuwa pamoja na Mahfoudh kwenye kambi ya kijeshi na baada ya kuundwa Muungano, akateuliwa awe mshauri (counselor) katika Ubalozi wa Tanzania, New York. Hapo ndipo Foum alipoanza kazi zake za kidiplomasia na kuanza kung’ara katika shughuli hizo. Rais Julius Nyerere alimteua awe Balozi wa Tanzania India, Italia na pia katika Umoja wa Mataifa. Foum aliwahi pia kuwa waziri mdogo wa mambo ya nje.

Nyerere akimuamini sana, na Foum alikuwa ni msiri wake mkubwa, na hasa kuhusu shughuli za kimataifa. Mara nyingi Mwalimu Nyerere alikuwa akimtuma kuonana na viongozi wa nchi nyingine alipokuwa ana mambo nyeti yaliomfanya awasiliane na viongozi hao. Yeye mwenyewe Foum, alikuwa na uhusiano na wanaharakati mbalimbali wa kimataifa.

MAFUNGAMANO NA MALCOLM X PAMOJA NA WAPIGANIA HAKI, USAWA NA UTU WENGINE.

Miaka michache iliyopita nilimpelekea baruapepe Amiri Baraka, Mshairi, Mwandishi na Mwanaharakati wa Kimarekani mwenye asili ya Kiafrika na nikamuuliza lini alikutana mwanzo na Babu. Baraka (ambaye zamani akijulikana kwa jina la LeRoi Jones) alinijibu: “Nilikutana naye Astoria Hotel, New York, mwaka 1964 wakati uleule nilipokutana mwanzo na Malcolm X”.

Wakati huo, Foum tayari alikuwa New York na alikuwa Mtanzania wa mwanzo kujuana na Malcom X na halafu akamjulisha kwa Babu aliyekuwa akidhuhuria kikao cha Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Gamba la albamu moja ya hotuba za Malcolm X lina picha ya Foum na Babu wakiwa pamoja naye Malcolm X. Ninajua kwamba Babu aliwahi kuiona albamu hiyo na gamba lake, lakini Foum hakuwahi kuiona.

Miaka miwili iliyopita tukiwa pamoja Nairobi alinishikiia nimtafutie gamba la albamu hilo. Moja ya masikitiko yangu ni kwamba sikujaaliwa kumtimizia haja yake. Usuhuba wa Foum na Malcolm X ulikuwa mkubwa kiasi cha kuwafanya wawe wanatembeleana majumbani mwao. Mwengine aliyekuwa akimtembelea Foum nyumbani kwake New York alikuwa mwanamapinduzi wa Cuba Che Guevara. Kwa ujasiri wake na licha ya kujuwa kwamba akiandamwa na majasusi wa CIA wa Marekani Foum alikuwa akifuatana bila ya kificho na Malcolm X pamoja na Che.

FOUM, KIASHIRIA CHA UTU, HESHIMA NA SERA ILIYOTUKUKA YA MAMBO YA NJE YA TANZANIA.

Kwa hilo na pia kwa harakati zake za kupinga ukoloni na ubeberu Foum alikuwa heshi kuwakera Wamarekani. Aliwakera sana kwa msimamo wake imara wakati mijadala ya vikao vya Kamati ya 24 ya kuufyeka ukoloni duniani. Foum aliteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika kamati hiyo.

Mfano wa jinsi Wamarekani walivyokuwa wakimuona kuwa ni mkorofi ni telegramu moja kutoka ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa iliyopelekwa kwenye wizara ya mambo ya nje ya Marekani. Telegramu hiyo iliandikwa Novemba 26, 1968, wakati Marekani ilipokuwa ikizingatia kujitoa kutoka kwenye Kamati ya 24.

Ilisema hivi: “Maazimio kama hayo yanatungwa hasa na Waafrika wenye siasa kali — kama Foum (Tanzania) wakisaidiwa na Masovieti na Waarabu wenye siasa kali kama Syria na Iraq”. Diplomasia kama ilikuwa katika damu yake na inaonyesha alimrithisha mdogo Abdillahi ambaye mwaka jana tu alistaafu akiwa balozi mdogo wa Sweden mjini Addis Ababa.

WATU WEMA HAWACHOKI KUWATUMIKIA WENZAO.

Yeye mwenyewe Foum aliendelea na shughuli za kidiplomasia hata baada ya kustaafu serikalini. Novemba 22, 2002, Amara Essy, Mwenyekiti wa muda wa wakati huo wa Muungano wa Afrika (AU), alimteua awe mjumbe wake maalum nchini Somalia. Foum alijipatia sifa kwa uchapaji kazi wake na kwa jitihada zake wakati wa Mkutano wa Somalia wa Kuleta Suluhu ya Kitaifa uliofanywa nchini Kenya toka Oktoba 2002 hadi Oktoba 2004.

Alikuwa mbioni pia wakati wa jitihada nyingine zilizochukuliwa baadaye na jumuiya ya kimataifa kujaribu kustawisha amani na kuleta suluhu nchini Somalia. Aliuacha wadhifa wa kuwa Mwakilishi Maalum wa Muungano wa Afrika kwa Somalia mnamo 2007 na mahala pake pakashikwa na Nicolas Bwakira kutoka Burundi.

Baadaye kama miaka miwili hivi iliyopita alichukuliwa kwa muda na Augustine Mahiga, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Somalia, awe mshauri wake. Aliiacha kazi hiyo mwaka jana akishughulika na biashara. Ujuzi wake wa siasa za Somalia na majungu ya wanasiasa Wakisomali ulikuwa wa kupigiwa mfano. Binafsi nilifaidika nao nilipokuja kuishi Nairobi na kusimamia mradi mmoja wa shirika la UNDP la Umoja wa Mataifa kuhusu kielelezo cha katiba mpya ya Somalia.

Alinishauri na kunielekeza wapi pa kupiga hodi ili kazi zangu kuhusu Somalia zifanikiwe. Wakati mwingine akinishauri hata bila kuomba ushauri wake. Huo ni mfano wa sifa nyingine aliyokuwa nayo — ya ukarimu na kutokuwa na uchoyo.

WEMA HAWADUMU ULIMWENGUNI, MOLA AMLAZE PEMA MCHAMUNGU MOHAMMED ALI FOUM.

Hizo zote ni sifa za mcha Mungu, na Foum alikuwa mtu wa aina hiyo kama marehemu baba yake, Inspekta Ali Foum.

Safari moja nikiwa Jeddah, Saudi Arabia, mfanyakazi mmoja katika Ubalozi mdogo wa Tanzania aliniambia kwa masikitiko: “Sijui Foum mzima kwa sababu haipiti mwezi hutokea hapa kuja kufanya umra Makkah. Mwezi huu sijamuona”.

Ama mimi sitomuona tena siku za Ijumaa katika Msikiti wa Hurlingham hapa Nairobi. 

"Hakika sisi ni Miliki ya Mungu, na Hakika kwake tutarejea", Mola amlaze Pema Mja Mwema huyu.
BURIANI BALOZI MOHAMMED ALI FOUM, GWIJI LA DIPLOMASIA NA MZALENDO WA KITANZANIA.

Mwanzoni mwa Mwezi huu Tanzania ilipata pigo zito mno lislopata mithilika, aliyekuwa Balozi wetu wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa Mzee Mohammed Ali Foum aliiaga Dunia Jijini Cairo Nchini Misri.

Balozi Foum (Juni 4, 1936 - Februari Mosi, 2013) ni Mzalendo wa kupigiwa mfano wa Tanzania ambaye aliitumikia Nchi hii, A
frika na Dunia kwa Ujumla kwa Moyo wake wote na Utumishi wa Kutukuka.

"Hakika sisi ni Miliki ya Mungu, na Hakika kwake tutarejea", Mola amlaze Pema Mja Mwema huyu
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top