Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania ( NSSF) Dr. Ramadhan Dau akizitaja changamoto
za mfuko huo katika hafla ya ufunguzi wa mkutano wa tatu wa wadau wa Mfuko huo
Mjini Arusha.
Waziri wa Kazi na Ajira wa
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanznia Mh. Gaudensia Kabaka akitoa tathmini
iliyofikiwa na Tanzania ya vigezo saba kati ya Tisa vya shirika la Kazi Duniani
(ILO) kuhusu mafao ya Jamii kwenye Mkutano wa NSSF Mjini
Arusha.
Balozi Seif Ali Iddi akitoa
Tuzo kwa baadhi ya wakuu wa Taasisi zilizofanya vizuri katika kuwasilisha
michango ya mafao ya wafanyakazi wao katika mifuko ya hifadhi ya
Jamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif akipokea zawadi maalum kutoka kwa Waziri wa Kazi na Ajira
wa SMT Mh. Gaudensia Kabaka kutokana na juhudi zake za kuwa karibu na mfuko
huo.
Baadhi ya wageni na
washiriki wa Mkutano wa tatu wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF) wakijivinjari wakati wimbo maarufu wa kitambaa cheupe ulipoimbwa katika
halfa ya ufunguzi wa Mkutano huo Mjini Arusha.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wakiwa pamoja na
wenyeji wao wakitoka kwenye Hoteli ya Mount Meru Arusha baada ya kufungua
Mkutano wa tatu wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF
)(Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ).
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Mifuko ya Pencheni Nchini kuwekeza
katika sekta ya Kilimo pamoja na Viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa kwa
lengo la kuongeza ajira hasa kwa vijana ili kuondoa ukali wa maisha na kupunguza
umaskini.
Wito huo ameutoa wakati
akifungua Mkutano wa Tatu wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
Tanzania (NSSF) unaofanyika Mjini Arusha.
Balozi Seif amesema
haifurahishi kwa Taifa hili kubarikiwa kuwa na rasilmali nyingi lakini matokeo
yake malighafi ya mazao mengi yanayotokana na rasilmali hizo, husafirishwa nje
ya Nchi hali ambayo inasababisha Serikali kupata mapato
madogo.
Amesema pamoja na kazi
nzuri ya uwekezaji katika kilimo inayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya
Jamii Tanzania, lakini bado Mifuko mingine ya Pensheni ina wajibu wa kufanya
jitihada za kuzuia usafirishaji huo na badala yake wanayasarifu hapa nchini ili
mbali ya kuongeza thamani lakini pia kutoa ajira kwa wananchi walio
wengi.
Balozo Seif amesisitiza
kuwa Ikiwa Nchi ya India imeweza kupiga marufuku kusafirisha mali ghafi kama
pamba ipo haja na sisi Tanzania kufanya jitihada za makusudi kabisa ya kuzuia
kusafirisha mazao yetu kwa namna hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar ameelezea faraja yake kutokana na mikakati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi
ya Jamii ( NSSF) ya kuwekeza kwenye Viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, ambao
utatoa fursa zaidi kwa wakulima kupata soko la uhakika wa mazao
yao.
Balozi Seif ametoa mfano
wa uwekezaji huu wa NSSF ambao umetoa fursa nzuri kwa wakulima wadogo wadogo
wa miwa Mkoani Kagera kuvuna Tani 40,000 za miwa, ambazo zina thamani ya
shilingi Bilioni 1.6 hali iliyoimarisha kipato cha jamii iliyo karibu na Kiwanda
cha Sukari Mkoani humo.
Akizungumzia umuhimu wa
utafiti na elimu ya kuongeza idadi ya wanachama, Balozi Seif amesema ipo haja
kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufanya utafiti katika sekta isiyo rasmi ambayo
mchango wake katika Uchumi wa Taifa ni mkubwa.
Amesema sheria ya
marekebisho ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii nambari 5 ya mwaka 2012, bado
hayajasaidia kupanua wigo wa wanachama bali kinachoonekana hivi sasa ni kwa
Mifuko hiyo ikishindana kwa kubadilishana wanachama wale
wale.
Akimkaribisha mgeni rasmi
Balozi Seif, Waziri wa Kazi na Ajira wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania Mh.Gaudensia Kabaka alisema Tanzania imefikia vigezo saba kati ya Tisa
vilivyoainishwa na Shirika La Kazi Duniani (ILO) katika Mkataba nambari 102
kuhusu mafao ya Jamii.
Waziri Gaudensia alivitaja
baadhi ya vigezo hivyo kuwa ni pamoja na Uzee, Kifo, Ugonjwa, Ukosefu wa Ajira
na Uzazi ambavyo vimekuwa vikitekelezwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na ile ya
Pencheni.
Hata hivyo Waziri wa Kazi
na Ajira Mh. Gaudensia Kabaka alieleza kwamba bado kipo kilio kikubwa kwa
wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na ile ya pencheni ambacho ni ufinyu wa
kukidhi mahitaji ya mafao.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania Dr. Ramadhan Dau alisema bado zipo
baadhi ya changamoto zinazozorotesha utekelezaji wa majukumu ya mfuko
huo.
Dr. Ramadhan Dau aliitaja
moja ya changamoto hiyo kuwa ni ucheleweshaji wa ukusanyaji wa michango ya
wanachama ambapo mpango maalum uko tayari kutumika wa makusanyo ya michango hiyo
kwa kutumia njia ya M. Pesa.
Ujumbe wa mwaka huu wa
Mkutano huo wa Tatu wa Wadau wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania
(NSSF) ni ‘Hifadhi ya Jamii Tanzania iko njia
panda’.
Post a Comment