Aliyekuwa
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na baade
kuenguliwa kugombea nafasi hiyo na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi huo, Jamali
Malinzi anazungumza hivi sasa na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
kuhusiana na uamuzi huo na kusema kuwa maamuzi hayo ameyasikia tu kwa vyombo vya
Habari lakini hadi sasa hajapata barua rasmi. Vile vile madai yaliyotolewa hadi
kuenguliwa kwake sio sahihi kwani sifa zote anazo.
---
YAH: KUENGULIWA KWANGU
KUGOMBEA URAIS WA TFF 2013
Ndugu zangu,kupitia vyombo
vyenu vya habari ninaomba niueleze umma wa watanzania,hususani wadau wa mpira wa
miguu,yafuatayo kuhusu kuenguliwa kwangu.
Awali ya yote nieleze
kusikitishwa kwangu na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya rufaa ya TFF ya
kuniengua kugombea urais wa TFF.Sikubaliani na maamuzi haya .
Katika kuniengua kamati ya
rufaa ya uchaguzi ya TFF imetoa sababu mbili (nanukuu magazeti ya jana tarehe
12/02/2013 maana hadi leo sijakabidhiwa barua ya kuenguliwa).
Kukosa uadilifu kwa kupinga
waraka uliotolewa na TFF wa kubadili Katiba ya TFF mwezi Desemba
2012.
Kukosa uzoefu wa miaka
mitano ya uongozi.
Ndugu zangu,kiini cha maamuzi
ya Kamati ya rufaa dhidi yangu ni pingamizi lililowekwa na mtu mmoja anayeitwa
AGAPE FUE.Bwana Agape Fue aliniwekea pingamizi katika kamati ya uchaguzi akidai
mimi nilipinga waraka wa kubadili katiba ya TFF na pia sina uzoefu wa miaka
mitano ya uongozi wa mpira.Kinyume na matakwa ya kamati ya uchaguzi kama
yalivyotangazwa kuwa mtoa pingamizi aje mwenyewe kutetea pingamizi lake ,Bwana
Agape Fue hakutokea mbele ya Kamati ya Bwana Lyatto.Matokeo yake tarehe
31/01/2012 kamati ya uchaguzi ya TFF ilitoa maamuzi ya ya kutupilia mbali
pingamizi hili.
Bwana Agape Fue hakuishia
hapo kwa mara nyingine tarehe 06/02/2013 alikata rufaa kwenye kamati ya rufaa
ya uchaguzi akidai kamati ya uchaguzi haikumtendea haki. Rufaa hii haikuwa na
anwani wala namba ya simu ya Bw.Agape Fue.Rufaa ilisikilizwa tarehe 10/02/2013
na maamuzi ya kukata jina langu yakatangazwa jioni ya tarehe
11/02/2013.
Mpaka leo najiuliza hivi huyu
Bw. Agape Fue ni mwanaume au ni mwanamke?(hakueleza kama ni Bwana au Bibi Agape
Fue). Agape Fue ni nani hasa? Anaishi wapi?Je ni Mtanzania au sio Mtanzania
maana kikanuni wasio watanzania hawaruhusiwi kujihusisha na uchaguzi wa TFF
(rejea kifungu cha 9 cha kanuni za uchaguzi),pingamizi lake halikuambatana na
udhibitisha wa uraia. Kwa nini alichukua maamuzi haya? Sipati jibu.
Iweje mtu achukue maamuzi
mazito ya kumkatia mtu rufaa kisha uishie kusaini karatasi na kuwaachia wengine
wakusemee na usije hata kushuhudia kinachoendelea kama kweli una maslahi na
madai yako? Waandishi wa habari mnisaidie kupata majibu.
Ndugu zangu ,mtoa pingamizi
alidai haikuwa sahihi kupinga azimio la kubadili katiba ya TFF kwa njia ya
waraka.Naomba nisistize mambo matatu:
Wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF
wanawakilisha matakwa ya vyama vilivyowatuma kwenda kwenye mkutano mkuu wa
TFF,na ndio maana chama cha mpira cha mkoa wa Kagera (KRFA) kiliitisha kikao cha
kamati ya utendaji ili kamati iweze kutoa mwongozo kwa wajumbe wake kuhusu
nini kifanyike kuhusu waraka ulioletwa na TFF,hivyo maamuzi yaliyotolewa ya
kuukataa waraka huu yalikuwa ni maamuzi ya chama cha mpira mkoa wa Kagera na
wala hayakuwa ni maamuzi ya Jamal Malinzi,iweje malinzi niadhibiwe kwa maamuzi
haya,kwa nini usiadhibiwe mkoa mzima na mikoa yote iliyopinga waraka?hii ni haki
kweli? Siamini kama kuna mjumbe wa mkutano mkuu aliyekiuka maamuzi ya kamati
yake ya utendaji.
Katika mchakato wa kubadili
katiba kwa njia ya waraka kilichokuwa kinagomba sio maudhui (content) ya
mabadiliko ya Katiba bali utaratibu uliotumika kubadili Katiba. Swali la msingi
tulilojiuliza wajumbe wa kamati ya utendaji KRFA ni kwamba je kwa mujibu wa
Katiba ya TFF kifungu 22 na kifungu 30 wapi katiba inatamka kuwa inaweza
kubadilishwa kwa njia ya waraka? Mpaka leo hilo jibu hakuna,labda aliyeniwekea
pingamizi atusaidie kupata jibu la swali hili. Katiba ya TFF iko wazi kabisa
inatamka kuwa Katiba itabadilishwa kwa njia ya Mkutano Mkuu tu (General
Assembly).
Ni kweli FIFA iliagiza
yafanyike mabadiliko ya Katiba ya kuingiza kipendele cha ‘club licencing’ katika
Katiba ,lakini je FIFA katika agizo hilo ilisema Katiba ya TFF ivunjwe ili
kutimiza azma hiyo? Ikumbukwe kuwa mwaka 2004 FIFA iliagiza TFF iingize kwenye
Katiba kipengele cha Katibu Mkuu awe wa kuajiriwa badala ya kuchaguliwa,agizo
hili lilitekelezwa kwa kupitishwa na Mktano Mkuu wa TFF,iweje leo utaratibu huu
ukiukwe?
Hata majuzi CAF walipotaka
kubadili katiba ili Rais wa CAF atokane na wajumbe wa Kamati ya Utendaji jambo
hili lilitekelezwa kwa kuitisha mkutano mkuu wa dharura uliofanyika Seychelles
majuzi. Katiba ndio msingi mkuu wa uendeshajiwa TFF,nitaipigania siku zote.Huo
ndio utaratibu,si CAF si FIFA si Vyama vya mpira vya nchi,hakuna anayebadili
Katiba kwa njia ya waraka,kama kuna mwenye ushahidi aulete.
Kuengua jina langu eti kwa
kuwa nilipinga waraka wa kubadili Katiba sio uamuzi sahihi.
Kuhusu uzoefu wa miaka
mitano katika Uongozi:
Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi
mkuu wa TFF mwaka 2008 niligombea na jina langu lilikatwa na kamati ya uchaguzi
ya TFF.Nilikata rufaa katika Kamati ya Rufaa ya TFF na kushinda . Hukumu hii ni
halali hadi leo.Iweje leo hii miaka minne baadae Kamati hiyo hiyo ya rufaa
(kubadili majina ya wajumbe sio kubadili taasisi) inione sina uzoefu?.Si hilo tu
,hata katika kujaza fomu namba moja ya kugombea niliambatanisha vielelezo vyote
vya uzoefu wangu ikiwa ni pamoja na kudhibitisha kuwa katika kipindi cha miaka
mine iliyopita nimekuwa:
-Mjumbe wa Baraza la michezo
mkoa wa Dar es salaam.
-Mwenyekiti wa kamati ya
mashindano chama cha mpira mkoa wa Pwani COREFA.
-Mjumbe wa mkutano mkuu wa
mkoa wa Kagera
-Mwenyekiti wa chama cha mpira
mkoa wa Kagera
Hii ni pamoja na kuongoza
Yanga 2002-2005.
Hivi katika nafasi hizi za
uongozi ipi ni ya kuongoza ‘bonanza’? Nimedhalilishwa sana.
HITIMISHO
Vyombo vya habari kupitia
makala,tahariri na maoni ya wasikilizaji/wasomaji/watazamaji vimesifia sana
awamu mbili za uongozi wa Bwana Leodeger Tenga.Bwana Tenga amesifiwa kwa umahiri
wake wa kuleta utulivu katika sekta ya mpira wa miguu Tanzania.Amesifiwa kwa
kujenga taasisi imara ambayo mhimili wake mkuu ni sekretarieti makini na kamati
mbali mbali zilizo imara .Let him rise to the occasion,muda wa kuonyesha uongozi
imara ni huu,historia itamhukumu kwa jinsi gani atasimamia suala hili,haki sio
lazima itendeke lakini pia inatakiwa ionekane inatendeka.
Kamati ya utendaji ya TFF
inayo mamlaka ya kubatilisha maamuzi haya kwa maslahi ya mpira wa
Tanzania.Ninamshauri Rais wa TFF aitishe kikao cha dharura cha kamati ya
utendaji ili kijadili hali hii na kunirudishia haki yangu ya kugombea urais wa
TFF.
Nihitimishe kwa kuwaomba wadau
wa mpira wa miguu Tanzania wawe watulivu wakati tukisubiri kupata ufumbuzi wa
suala hili.
Mungu ibariki
Afrika,
Mungu ibariki
Tanzania.
Ahsanteni
sana,
JAMAL
MALINZI
S.L.P 10000 DAR ES
SALAAM
13/FEBRUARY/2013
Post a Comment