Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo (Pichani) amewataka wakatoliki na watanzania kwa jumla kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo kumetokea kundi la watu wachache kutaka kuvunja amani  hapa nchini kwa kutumia udini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kardinali Pengo amesema moyo wa kisasi hautasaidia kitu chochote, kinyume chake utaleta maafa yaliyo makubwa zaidi na kutuingiza katika janga kubwa zaidi.
Ameongeza kuwa siku ya tarehe 20 kutakuwa na ibada katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph itakayoongozwa na Askofu Msaidizi kwa lengo la kumuombea marehemu Padri Evarist Mushi na kuliombea taifa ili watanzania tuendelee kuwa wamoja na tubaki katika amani tuliokwisha kuizoea.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amezungumza hayo baada ya kusoma waraka uliotolewa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu uliozungumzia mambo mengi ikiwemo kuwataja wakatoliki kama ‘makafiri’ na kuwa bado haijawa mwisho wa mapambano.