Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif akiangalia ramani ya Zanzibar jinsi Mkonga wa
Mawasiliano unavyoweza kuziunganisha taasisi za serikali kupitia mradi wa
e-government katika ofisi za kituo hicho Mazizini Zanzibar
Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho Zanzibar (Zan ID), Mohd Juma
Ame akionesha mfumo wa utayarishaji wa vitambulisho hivyo katika ofisi hizo
zilizoko Mazizini Zanzibar.Picha na Salmin Said,-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
--
--
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
ameelezea umuhimu wa kuwepo uadilifu katika mchakato mzima wa utoaji wa
vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi.
Amesema kitambulisho
hicho ni muhimu kwa maendeleo na usalama wa taifa, hivyo umakini na uadilifu
unahitajika kuhakikisha kuwa wanapewa wanaohusika.
Maalim Seif ameeleza
hayo leo wakati akiwa katika ziara maalum ya kutembelea ofisi za usajili na
kadi za utambulisho Zanzibar pamoja na kituo cha Serikali Mtandao e-government
kilichopo Mazizini.
Amesema kuna taarifa
kuwa wapo baadhi ya watu wasiokuwa raia wa Tanzania wamekuwa wakipatiwa
vitambulisho hivyo na kuwaacha wazanzibari wenye sifa, jambo ambalo ni hatari
kwa usalama wa nchi.
Hata hivyo ameelezea
kuridhishwa kwake na utendaji wa ofisi hiyo, na kuwataka kuongeza juhudi ili
kuhakikisha kuwa wanapata ujuzi wa kutosha katika kuendeleza kazi hiyo.
Amewahimiza wanasiasa
kuwashajiisha wafuasi wao kufuatilia vitambulisho vyao, ili kila mzanzibari
aliyetimiza masharti aweze kupata kitambulisho hicho ambacho kitamsaidia katika
harakati zake za maisha.
“Kitambulisho hiki
ndio maisha kwa sasa, bila ya kuwa nacho huwezi kufanya jambo lolote la
maendeleo, yaani hata ukitaka leseni ya udereva lazima uwe na kitambulisho,
seuze kusafiri, kuendelea na masomo au kutafuta ajira”, alifahamisha Maalim
Seif.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho Bw. Mohd Juma Ame amemuhakikishia Makamu wa
Kwanza wa Rais kuwa wanafanya kazi kwa utaalamu wa hali ya juu kuhakikisha kuwa
hakuna udanganyifu unaofanywa katika utoaji wa vitambulisho hivyo.
Amesifu ubora wa
vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, na kwamba vinatengenezwa kwa kutumia
teknolojia ya hali ya juu inayoweza kudhibiti taarifa za siri za muhusika
ambazo haziwezi kuonekana bila ya kutumia kifaa maalum, na hivyo kuweza
kudhibiti ubadhirifu.
Akizungumzia kuhusu
mtandao wa serikali, e-government Maalim Seif amesema mradi huo umeanza vizuri
na kutaka undelezwe kwa maslahi ya taifa.
Ameelezea matumaini
yake kuwa iwapo mpango huo utatumiwa vizuri unaweza kupunguza gharama za
uendeshaji wa serikali, kwa vile watendaji wataweza kuwasiliana, kufanya vikao
na kukubaliana kupitia njia hiyo ya mtandao.
Amewahimiza watendaji
wa ofisi hiyo kuandaa vipindi maalum vya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu
wa mfumo huo wa e-governmet, ili kuongeza uelewa na kuweza kuona faida za mfumo
huo.
Na
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Post a Comment