Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akivuta
waya kuashiria kufyatua mtego wa kuwasha moto wa kuteketeza Silaha haramu,
wakati alipokuwa mgeni rasmi katika zoezi hilo la uteketezaji wa silaha haramu,
Lililofanyika katika Kambi ya Magereza jijini Dar es Salaam, leo Feb 16, 2013.
Kushoto kwake ni Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania, Simon Siro na wa
pili kulia kwake ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Perera Ame Silima na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kmataifa, Benard Membe.
Sehemu
ya Silaha hizo zikianza kuteketea kwa moto baada ya Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed
Gharib Bilal, kufyatua waya maalumu wa kuwasha moto huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi, baada ya kusimamia zaoezi
la uteketezaji wa Silaha haramu, lililofanyika Ukonga jijini Dar es Salaam, leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana
na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Simon Siro, wakati wakipita kukagua
sihala hizo haramu kabla ya kuanza kwa zoezi la uteketezaji wa silaha hizo
haramu lililofanyika Ukonga jijini Dar es Salaam, leo.
Silaha haramu zilizoteketezwa hii leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma
hotuba yake wakati wa zoezi la uteketezaji wa Silaha Haramu, lililofanyika
Ukonga Jijini Dar es Salaam leo.
Wimbo
wa Taifa, kabla ya kuanza kwa zoezi hilo.
*******************************************************
DKT. BILAL AWATAKA WANANCHI KUWAFICHUA WANAOMILIKI SILAHA HARAMU
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
ameongoza zoezi la uteketezaji silaha haramu na kuwataka wananchi
kushirikiana na serikali katika kuwafichua wanaomiliki silaha hizo
mapema kabla athari haijawa kubwa zaidi.
Akizungumza katika zoezi hilo la kuteketeza silaha haramu, ambalo limefanyika pamoja kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye viwanja vya Magereza, Ukonga Jijini Dar es salaam Dkt. Bilal alisema kila mwananchi ni mlinzi wa kwanza wa amani ya nchi yake na wanaomiliki silaha haramu ni wazi kuwa siyo raia wenye malengo mema na amani ya nchi zao.
“Naomba
kuchukua nafasi hii kuushukuru uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa kufanikisha zoezi hili ambalo linalenga kutukumbusha kuwa ili tuwe
na Jumuiya bora yenye kupiga hatua, hatuna budi kuhakikisha eneo letu
linabaki kuwa salama na kwamba wananchi wetu wanapata nafasi ya kufanya
kazi zao za kujiongezea kipato bila kuwa na hofu ya usalama wa maisha
yao,”
Alisema
ndani ya Jumuiya kumekuwa na migogoro mbalimbali sambamba na matukio ya
kihalifu ambayo mengi huchangiwa na uwepo wa silaha ndogo na kubwa
ambazo hazimilikiwi kihalali.
Alisema
takwimu zilizopo zinabainisha kuwepo kwa silaha haramu zipatazo 500,000
(laki tano) katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki hali ambayo
inaonesha kuwa kuna kazi kubwa ya kukabiliana na migogoro ya aina
mbalimbali ya uhalifu inayojitokeza katika jamii.
Alisema
kufuatia raia wasio waaminifu kumiliki silaha haramu kumekuwepo na
ongezeko la matukio ya kihalifu yanayotumia silaha na matukio mengi
katika ukanda wa Afrika Mashariki yanatokea katika maeno ya mipakani na
yale yanayohusisha muingiliano wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine,
matukio ya ujambazi, uvamizi na mengine ya aina hiyo.
Alisema
ongezeko la silaha haramu lina athari nyingi katika maisha na maendeleo
kwa ujumla na kutaja athari ya wazi kabisa inayotokana na ongezeko la
silaha hizo kuwa ni ile inayojitokeza katika sekta ya Utalii ambako watu
wameshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ujangili unaofanywa katika mbuga
za wanyama ambao unahatarisha kwa kiasi kikubwa mafanikio katika sekta
ya Utalii.
“Tusipowadhibiti
majangili mapema, siku wanyama wakipungua watahamia katika sekta
nyingine. Kazi hii itakuwa rahisi kama tukiifanya kama Jumuiya na sio
nchi moja moja,” alibainisha Makamu wa Rais.
Dkt.
Bilal alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kusaidia
Jumuiya ya Afrika Mashariki kukabiliana na tatizo la silaha haramu na
hasa Shirika la Maendeleo la Ujerumani GTZ ambalo limesaidia katika
kufanikisha zoezi hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Ujerumani nchini Klaus Brandes alisema Serikali
ya Ujerumani itaendelea kuisaidia Jumuiya katika kukabiliana na tatizo
la silaha haramu ili kuhakikisha eneo la ukanda wa Afrika Mashariki
linabaki kuwa na amani na salama.
Alielezea
kufurahishwa kwake na juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kutatua
migogoro kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
kwenye Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
Februari 16, 2013
Post a Comment