SAKATA
la wizi wa fedha katika akaunti za wateja wa benki, sasa limeingia katika sura
mpya baada ya Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Dk Gervas Mbasa (Chadema) naye
kuibuka na kudai kuwa ameibiwa Sh6 milioni kutoka kwenye akaunti
yake. Akizungumzia
wizi huo, mbunge huyo alisema fedha zake ziliibwa kwa nyakati tofauti kati ya
Desemba 20 mwaka jana na Januari 3, mwaka huu.
Alisema
kitendo hicho kilifanywa na mtu mmoja aliyempigia simu na mtu mmoja
aliyejitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Makao Makuu ya Kampuni ya Airtel na
kwamba alikuwa katika zoezi la kuhakiki namba zote za
zamani.
“Alinieleza kwamba kwa
niaba ya Airtel yupo katika zoezi la kuhakiki namba zote zilizosajiliwa zamani
na yangu ilikuwa ni ya miaka 10 na akaniuliza namba ya mwisho kuwasiliana na mtu
kupitia simu yangu. Nilimtajia namba ya mke wangu na baada ya maelezo hayo
aliniomba nisizime simu yangu wakati wakiwa wanashughulika na kuisajili na
kwamba muda wowote nitapatiwa maelekezo,” alieleza mbunge huyo.
Kilichotokea baada ya
muda ni kwamba simu yangu, haikuweza kufanya kazi, hatua hiyo iliyonilazimisha
kuwasiliana na watoa huduma wa kampuni hiyo huko jimboni ili kujua tatizo ni
nini, lakini kila aliyejaribu kuirejesha katika mawasiliano alinijibu kuwa
haiwezekani mpaka makao makuu,” alisema Mbasa.
“Kila wakala wa Airtel
niliyemfuata na kumweleza kuwa simu yangu haifanyi kazi, alipoingia kwenye
mtandao wao kwa ajili ya kuirejeshea mawasiliano alinijibu kuwa hiyo haiwezekani
mpaka makao makuu ya kampuni hiyo,” alisema.
Mbunge huyo alisema
majibu hayo yalimlazimisha kutulia bila mawasiliano hadi Januari mwaka huu
alipokwenda katika Makao Makuu ya Aritel na kufanikiwa kuirejeshea simu yake
mawasiliano.
Dk Mbasa alisema baadaye
aligundua kuwa wakati simu yake ikiwa imekosa mawasiliano watu hao walikuwa
wakishughulikia kuhamisha fedha zake kutoka katika akaunti
yake.
Alisema
Januari 6, mwaka huu alifanikiwa kwenda Tawi la Benki ya NMB la Mazengo ambapo
baada ya kuangalia salio katika akaunti yake, alibaini kuwapo kwa wizi huo na
baadaye aliwasiliana na maofisa wa benki hiyo ambao walimthibitishia kuwa
ameibiwa. Kwa
mujibu wa mbunge huyo, maofisa hao walimpatia fomu za kujaza, ili kusitisha
kutumia huduma ya `Sim Banking’ katika akaunti
yake.
Dk Mbasa alisema baadaye
aliwasiliana na meneja wa benki hiyo na kutakiwa kuandika maelezo ya wizi ikiwa
ni pamoja na kukabidhiwa kwa wataalamu wa masuala ya ufuatiliaji wa uhalifu kwa
njia ya mitandao.
Alisema baada ya
kuangalia katika mtandao, wataalamu hao walibaini kuwa fedha zake zilitolewa na
wahusika katika kipindi cha kati ya Desemba 20 mwaka jana na Januari 3, mwaka
huu.
“Kwa mujibu wa mtandao
wa Benki inaonyesha fedha zangu zilitolewa kwa kutumia huduma ya `Sim Banking’
ya NMB Mobile ambapo zilikuwa zikihamishwa kutoka katika akaunti yangu kwenda
`Pesa Faster Collection’ na kwa watu wengine wawili,”
alifafanua.
Alisema kutokana na
maelezo hayo ya NMB, alilazimika kufungua jalada katika Kitengo cha Polisi cha
Kupambana na Wizi kwa Njia ya mtandao lakini, hadi sasa hakuna lolote
lililofanyika.
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime alisema hana kumbukumbu kuhusu madai ya mbunge huyo kuibiwa na kuomba muda ili afuatilie kwa maofisa wake.
Meneja wa Kanda ya Ziwa
wa Kampuni ya Simu ya Mkononi Airtel, Ally Maswanya alisema hakuna zoezi la
uhakiki wa namba lililoendeshwa na kampuni yake na kwamba anavyotambua kuna watu
wahuni ambao wamekuwa wakijifanya kuwa ni maofisa wa kampuni na kisha
kuziingilia namba za wateja wao.
Chanzo -
Mwananchi
Post a Comment