Na Edna
Bondo
WAKATI watanzania
wengi hawajasahau machungu ya kulizwa na kampuni ya kupanda na kuvuna mbegu ya
DECI, kumeibuka taasisi mpya ya fedha inayojitapa kutoa mikopo kwa njia ya
mtandao, huku ikitumia vibaya majina ya Rais Jakaya Kikwete na Barack Obama wa
Marekani.
Mbali ya taasisi
hiyo ya Tanzania Loans Society kutumia majina ya marais hao, imewahusisha pia
Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Ridhiwani Kikwete, ambapo inahofiwa kutapeli
mamilioni ya walalahoi.
Taarifa za taasisi
hiyo zinaonesha kuwa ilianza shughuli zake mwaka 2012, na kupata ufadhili wa
fedha kutoka kwa Rais Obama, ambapo inasimamiwa na Rais Kikwete, Waziri Mkuu
Pinda na mratibu mkuu ni Ridhiwani.
Watendaji wengine
ni Michael John ambaye namba yake ya simu ya mkononi ndiyo inayotumika kutuma
pesa za usajili.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa taasisi hiyo, imekuwa ikijitangaza
kutoa huduma ya mikopo na mawasiliano ya jinsi ya kupata mikopo hiyo, hufanyika
kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha wateja wa mikoani kupata mikopo hiyo
kirahisi bila usumbufu wa kuja makao makuu yao jijini Dar es
Salaam.
Baadhi ya wananchi
walioomba kupata mikopo hiyo, waliliambia gazeti hili kuwa, fomu za mikopo ya
taasisi hiyo hutolewa kwa sh 15,000 ambazo nazo hulipiwa kwa njia ya
mtandao.
Mmoja wa wateja wa
taasisi hiyo aliyedai kutapeliwa, Maywood Maganga alisema alionja machungu baada
ya kuingia kwenye tovuti yake na kukutana na maelekezo ya kumtaka ajaze fomu na
taarifa zake binafsi na kisha kutakiwa kutuma sh 15,000 kwenda kwenye namba 0656
73 64 16, iliyosajiliwa kwa jina la Michael John.
Maganga alisema
kuwa alifanya hivyo, na kusubiri majibu.
Kwa mujibu wa mkopo
huo wenye masharti nafuu, tena usio na riba, mteja hutakiwa kurejesha na kuanza
kukatwa baada ya miezi miwili tangu siku ya kupokea pesa hizo za
mkopo.
“Maelezo ya mkopo
huo yanaonesha kuwa una masharti nafuu sana na marejesho yake ni sh 60,000 kila
mwezi bila kujali kiasi ambacho mteja amekopa.
“Maelezo ya fomu
niliyojaza yalinionesha kwamba nitapata sh 300,000 kama zawadi kwa kukubali
kukopa na baada ya dakika 30, ningeingiziwa kiasi cha fedha za mkopo
nilizoomba,” alisema.
Kwa mujibu wa
Maganga, fomu alizozikuta kwenye tovuti ya taasisi hiyo, zilionesha mahala ofisi
ilipo, lakini alipofuatilia na kuuliza, alibaini kuwa taasisi hiyo haina ofisi
katika jengo la serikali la Utumishi wa Umma.
“Mwanzoni sikuwaza
kama taasisi hii itakuwa ya kitapeli, lakini baada ya siku mbili ya kutokutumiwa
pesa hiyo ndipo nilipogundua kwamba nimetapeliwa,” aliksema.
Maganga aliziomba
mamlaka husika kuingilia kati kwa kudhibiti utapeli huo, kwani Watanzania wengi
wameshalizwa kupitia taasisi hiyo inayotumia majina ya watu maarufu
kutapeli.
Aidha, maelezo ya
tovuti hiyo yanaeleza zaidi kuwa kwa kutambua ugumu wa maisha uliopo kwa
Watanzania na kukua kwa teknolojia kama nchi zingine zifanyavyo, taasisi hiyo
inatoa mikopo kwa njia hiyo ya mtandaao ili kuepuka usumbufu wa kuwafikia watu
walioko mikoani ili nao wanufaike.
Mbali ya hayo, pia
taarifa ya maelezo ya taasisi hiyo hiyo ilieleza kuwa kiwango cha chini cha
kupata mkopo ni sh 100,000 na ofisi zake zipo katika jengo la utumishi wa umma,
ghorofa ya tano chumba namba 30.
Ridhiwani hakuweza
kupatikana kuzungumzia taasisi hiyo, lakini katika taarifa aliyoituma hivi
karibuni kwenye ukurasa wake wa facebook, alikanusha yeye na viongozi wa
serikali akiwemo Rais Kikwete kuhusika na taasisi hiyo.
“Maisha ni
kuhangaika na kwamba inataka mtu anayefahamu njia sahihi kuweza kujua kuwa
nikitumia njia hii hali itakuwa sawa na pengine mambo yangu
yatanyooka.
“Hii inaweza kuwa
ndiyo maana halisi ya kuhangaika ufanikiwe, lakini tafsiri hii haiwezi kuwa
kutumia njia za kudhulumu, kukaba, kuiba au kufanya utapeli ili ufanikishe
malengo yako mabaya dhidi ya mtu au kikundi fulani cha watu," aliandika
Ridhiwani kwenye ukurasa wake wa facebook.
Kwa mujibu wa
Ridhiwani, hivi karibuni alipokea ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake ya
mkononi na barua pepe, ikihoji kuhusika kwake na kampuni hiyo.
Alisema mradi huo
unadaiwa kuanzia katika mikono ya Rais Obama kuja Tanzania kupitia Kikwete na
sasa yeye akishirikiana na Waziri Mkuu Pinda wanauendesha.
“Jambo hili si la
ukweli hata kidogo, na naomba kutumia nafasi hii kulikanusha kabisa mbele ya
umma wa Watanzania na wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wanafuatilia,”
ilisema taarifa hiyo ya Ridhiwani.
Vilevile taarifa ya
Ridhiwani ilitahadharisha umma wa Watanzania kuwa makini na mambo ya mitandao
ambayo hutumia jina lake kwa utapeli kwa lengo la kumchafua, lakini yeye na
viongozi wengine hawahusiki na Tanzania Loans Society.
Viongozi wa taasisi
hiyo hawakuweza kupatikana kwa njia yoyote ile kwani simu zao hazipokelewi na
hata katika ofisi wanazodai kuwapo, hawaonekani.Tanzania
Daima.
Post a Comment