Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akisoma
taarifa hiyo kwa vyombo vya habari mapema hii leo. Taarifa hiyo hiyo iliyodumu
kwa zaidi ya saa moja na nusu ilirushwa moja kwa moja (LIVE) na Radio Chemchem
FM ya Hapa mjini Sumbawanga.
NA
HAMZA TEMBA
OFISI YA MKUU WA MKOA
RUKWA
Feb
23
Elimu ni ufunguo wa maisha. Elimu ni
mwanga. Elimu ni dhamana. Elimu ni nuru. Hizi ni baadhi tu ya kauli mbiu ya
shule za msingi na sekondari zilioachwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere. Kauli mbiu hizi zilibeba ujumbe mzito wenye maana na
malengo ya elimu katika nchi yetu. Kwamba elimu impe mwanafunzi uwezo na ujuzi
wa kufikiria, kujitambua na kuutambua wajibu wake katika jamii na taifa na pia
kuwa mbunifu. Kwamba fikra na ubunifu utokanao na elimu uwe ni chachu ya kuleta
mwamko mpya wa kimapinduzi. Mapinduzi hayo yalenga kuwakomboa watanzania kutoka
katika minyororo ya maadui watatu wa maendeleo -- ujinga, umaskini na maradhi.
Azimio la Arusha lilesema wazi kwamba ni wajibu wa kila mtanzania kujielimisha
kwa kadri ya uwezo wake -- uwezo wake kiakili na si kifedha kwa
manufaa yake na watanzania wote.
Matokeo yake serikali ilifanya kila
jitihada kuwekeza katika vichwa vya watu ambao wengi wao sasa ndio wenye mamlaka
na nafasi mbalimbali za uongozi katika taifa letu. Kama si sera za Azimio la
Arusha zilizojaa misingi ya utu basi Ndugu Mizengo Pinda, mtoto wa mkulima
ambaye ni alama ya kazi iliyotukuka ya Mwalimu Nyerere ya elimu kwa wote,
tusingemjua. Na wengine wengi tu tusingewajua kwani ingekuwa vigumu sana kwao
kusoma. Fikiria vipaji na vipawa ambavyo tungevikosa kama si nia ya dhati na ya
kizalendo ya Mwalimu Nyerere ya kuongoza mapambano ya kumkomboa mtanzania.
Katika kutimiza azma ya elimu ni dhamana, Mwalimu aliandika sera ya Elimu ya
Kujitegemea. Lengo kuu likiwa ni kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kujitegemea
baada ya kumaliza shule.
Wahitimu wenye ujuzi si katika fizikia
au historia tu bali wenye uwezo kuendesha maisha yao kwa kuanzisha miradi ya
kilimo, ufugaji, ufundi, biashara n.k. Kupitia jeshi hili la wahitimu Tanzania
ilifanikiwa kufuta ujinga. Mwaka 1985 wakati Mwalimu anang’atuka watu waliokuwa
wanajua kusoma na kuandika walikuwa takribani aslimia 98. Leo hii wanaojua
kusoma na kuandika ni aslimia 69 tu. Miaka saba iliyopita wasiojua kusoma na
kuandika walikuwa ni aslimia 65. Tumeanguka. Na sasa aslimia 60 ya wahitimu wa
kidato nne wameshindwa. Taifa limefeli. Nini hatima ya Tanzania yenye kujaa
kizazi cha wajinga na masikini hoehae? Kabla ya kujibu swali hilo tujiulize kwa
nini tumefika hapa tulipo?
Chanzo
Kushuka kwa ubora wa elimu kumekuwepo
nchini kwa miaka 20 sasa. Chanzo kikuu cha kushuka huku ni sera za uliberali
mamboleo ambazo zinaendesha takribani kila sekta ndani ya nchi yetu. Sera hizi
zinazohubiriwa na IMF na Benki ya Dunia kimsingi zinaua ustawi na maendeleo ya
nchi yetu na watu wake. Utakumbuka kwamba katika jitihada za kupata mkopo kutoka
IMF Tanzania ilipewa masharti ya kupunguza wafanyakazi, kukata mishahara na
kukata matumizi katika sekta za kijamii za elimu na afya, kubinafsisha na kuuza
mashirika ya kwa bei bwerere karibu na chee na serikali kujiondoa katika
kusimamia uchumi. Kilimo kilitelekezwa na mashirika ya umma ya umma yalikufa
kifo cha kawaida. Kila kitu kiliachwa mikononi mwa soko huria ambalo limeuacha
umma wa wakulima na wafanyakazi ukilia. Matokeo yake tukaigeuza elimu kuwa
biashara huria. Serikali ikapunguza kuwekeza katika elimu. Gharama ya karo na
michango mingine ikaongezeka lakini huduma na ubora wa elimu ukawa unashuka kila
mwaka.
Kuongezeka kwa gharama za michango
kukawafanya wazazi waache kusomesha kwani hawana uwezo. Hali hii iko mpaka sasa.
Watoto wana akili. Shule za serikali zinawafukuza eti kwa sababu tu hawana karo
na michango ya madawati. Wanafunzi wanachangia kununua chaki achilia mbali
kwenda maabara. Huo ndio mfumo wa uchumi wa IMF wenye lengo la kuzalisha wajinga
na masikini wengi ili kujenga jamii yenye matabaka. Jamii ya watwana wengi na
mabwana wachache. Tanzania ya leo iko hivyo. Kama umezaliwa katika familia
masikini basi jua fika hutapata nafasi kuwa kama Ndugu Pinda. Haipo. Ndoto zenye
matumaini hazipo tena.
Kwa wale waliobahatika kusoma katika
shule za sekondari za serikali watakumbuka kuwa shule hizo zilisifika kwa
ufundishaji. Lakini mambo yalibadilika sana miaka ya 1990. Nakumbuka kuanzia
mwaka 1992 shule za serikali zilikuwa zikifungwa mapema kutokana na kutokuwa na
pesa za kununua chakula. Likizo ilikuwa ikianza mwishoni mwa mwezi Mei na kuisha
mwanzoni mwa Agosti. Likizo ikianza mwanzoni mwa mwezi Novemba na ikisha Januari
mwishoni. Kwa kawaida tulipaswa kufunga shule mwanzoni au katikati ya mwezi Juni
na kufungua mwanzoni au katikati ya mwezi Julai. Pia tulipaswa kufunga mwishoni
mwa mwezi Novemba na kufungua mwanzoni mwa mwezi Januari. Kwa hesabu ya haraka
tulikuwa tukipoteza miezi mitatu bila kusoma. Wazazi wenye pesa hawakubali
watoto wao wasome katika sekondari za serikali. Kwa nini? Jibu tunalo
sasa.
Mambo yalikwenda yanabadilika kila
uchao na hasa mitaala ya elimu ilifumuliwa. Nayo elimu ya watu wazima ikafa.
Baadaye ikaja fikra nzuri ya kujenga shule ya sekondari kila kata. Shule
zikajengwa kwa kasi lakini bila kuwepo kwa mikakati ya maana ya kuzalisha walimu
na uhakika wa vifaa vya kufundishia. Kimsingi shule za shule za kata ZINAKATA na
matokeo ya KUKATA tumeyaona. Wanafunzi wanaingia kwenye chumba cha mtihani
wanaandika namba na kutoka nje. Wengine wanakata kiu kwa matusi na hoja
kemukemu. Kama taifa tukubali lawama kwamba tumekitelekeza kizazi cha watoto
wetu na wadogo zetu.
Msongamano wa magari Dar es Salaam
unafaida moja kubwa sana ya kupima mambo yanavyonda ndani ya nchi yetu. Nikiwa
Dar es Salaam mwaka jana, ilikuwa ni siku ya jumatatu saa mbili asubuhi -- muda
wa watoto kuwa shule, mara nikaliona gari la waziri mwenye dhamana ya elimu
likiwa limesimama katika msongamano na limezungukwa na watoto ombaomba. Kioo
hakikukushushwa kuwauliza -- kulikoni, nendeni shule. Hawa watoto wako Dar es
Salaam, je, wale wanaoishi katika vijiji vya Nyanchenche, Nyamigota, Kakonko na
Chilimba, Chiroro, Chipango, Chipembe, Ikondo,
Muundi, Mang’onyi, Mwau na Minkoto hali yao kielimu ikoje?
Kwa hiyo kushindwa kwa wanafunzi wengi
hakutokani na mithani kuwa mgumu. Kumbe mitihani inatakiwa uweje sasa? Mwepesi?
Wala kushindwa hakutokani na mfumo wa usahihishaji mitihani. Wala kushindwa
hakutokani na sekta ya elimu kutokuwa chini ya ofisi ya Rais. Ofisi ya Rais
itakuwa na mangapi?
Kama nilivyosema hapo juu, nirudie
tena, kushindwa ni matokeo ya kukumbatia saaaaaana uliberali mamboleo ambao
lengo lake ni kuua mfumo wa ubunifu na fikra za watu wetu. Na kupitia hapo
kuwatumia wale wenye kuukubali uliberali mamboleo kujenga jamii ya kinyonyaji
kwa faida ya mabepari. Ni kutokana na hali hiyo mtoto wa masikini hasomi; walimu
wanakatishwa tamaa; ufisadi na rushwa kukithiri katika sekta ya elimu; mitaala
mibovu isiyowajengea wanafunzi uwezo wa kujitegemea baada ya kumaliza masomo; na
kubwa zaidi ni seerikali kutokuipa kipaumbele elimu. Tufahamu kuwa ni kanuni ya
mfumo wa kibepari kwamba ili uwatawale watu basi wafanye wengi wao wajinga, pili
wafanye wawe masikini. Ukiwapa elimu unawafumbua macho. Watahoji. Watadai haki
zao.
Nini
Kifanyike
Naamini tunaweza kuibadili hali hii na
kuifanya elimu Tanzania kuwa bora na si bora elimu kama ilivyo sasa. Yako
maswali mengi ya kujiuliza na miongoni mwayo ni: Je, hawa walioshindwa
tunawaweka wapi? Je, tuishie kuwaita waliofeli na kuwaacha wakiozea vijijini na
kuwa vibaka mijini? Ni ipi hatima ya maisha yao? Ni ipi hatma ya Tanzania katika
karne ya 21 yenye ushindani na mikakati ya wakoloni kurejesha ukoloni?
Maswahili haya yanajibiwa na hoja
kwamba taifa lolote duniani hujengwa na elimu na raslimali lilizoko katika taifa
hilo. Elimu ndio msingi wa maendeleo ya watu na ustawi wao. Elimu ndio msingi wa
demokrasia-shirikishi na uongozi bora. Elimu ndio msingi wa utafiti na ugunduzi
wenye manufaa kwa watu. Thamani ya elimu haina mfano wake. Wahenga walituusia
kuwa elimu ni bora kuliko mali. Mali unapozidi kuitumia ndivyo inavyokwisha ili
hali kwa mwenye elimu kadri anavyoitumia ndivyo anavyojiongezea maarifa na ujuzi
zaidi katika fani yake. Unapokuwa na utajiri wa mali unakuwa na jukumu la
kuilinda mali hiyo isipotee lakini elimu inamlinda mwenye nayo. Hapa nina maana
kwamba hatuwezi kujenga taifa lenye uchumi imara kwa machinga na biashara za
uchuuzi.
Tukumbuke kwamba wanazuoni na wale
wenye kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika taifa letu wote wasingekuwa na
nafasi walizonazo kama wasingekuwa na elimu. Mataifa makubwa kama Marekani,
Uingereza, Urusi, Japan, Ujerumani, China nk. yanafanya kila jitihada kusomesha
watu wake maana bila ya elimu yasingefika hapo yalipo. Umefika wakati sasa wa
kuirejea sera ya Mwalimu Nyerere ya Elimu ya Kujitegemea na kuifanya sera mama
ya elimu taifa letu. Sera hii ina mafunzo makubwa na ya maana sana hata sera ya
Umoja Mataifa ya elimu kwa ajili ya maendeleo-endelevu (Education for
Sustainable Development) haifikii ubora wake. Tuidurusu. Italisaidia taifa.
Pili, kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa umma wa wakulima na wafanyakazi wa
watanzania.
serikali ichukue hatua za makusudi za
kurekebisha mfumo wa elimu na mitaala. Tatu, zichukuliwe hatua za makusudi
kuhakikisha wale waliofeli wanapewa fursa ya kurudishwa shuleni ili wasome tena
-- wana akili na vipaji vizuri. Nne zifanyike jitihada za
kuzipatia vifaa vya kufundishia hasa masomo ys sayansi na kujenga mabweni katika
sekondari za kata ili kuwarahisishia maisha wanafunzi wanaoishi mbali na shule
hizo kwani wanaporudi makwao, wakiwa wamechoka, wanakutana na kazi za nyumbani
za kuteka maji, kusenya kuni na kupika. Watapata wapi muda wa kujisomea? Tano,
zijengwe maktaba katika maeneo karibu na shule za kata ili kuwapa fursa watoto
ya kujisomea. Sita, uwepo utaratibu wa kuwapikia wanafunzi chakula cha mchana.
Huwezi kushinda na njaa halafu ukasoma. Saba, ziongezwe jitihada za kusomesha
walimu wengi zaidi na kuwapa motisha inayotakiwa na mazingira mazuri ya kazi.
Nane, elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ufundi, ualimu, uhuguzi itolewe
bure. Uwezo tunao, sababu tunazo, NIA je?
Na Amani
Millanga
Post a Comment