KIONGOZI wa
Kanisa Katoliki nchini Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ametabiriwa kuwa
anaweza kuchaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa kanisa hilo duniani anayejulikana kama
Baba Mtakatifu au Papa.
Kardinali Pengo
anatajwa kuweza kuchaguliwa kuwa Papa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo
nafasi yake ya ukardinali, inayomweka kwenye mazingira ya kuwa mmoja wa
watakaomchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki duniani, ambapo kwa mujibu wa
sheria za kanisa hilo yeyote mwenye cheo hicho, anaweza kuchaguliwa kuwa
Papa.
Wakizungumza
katika mahojiano na Mwananchi Jumapili, baadhi ya waumini wa kanisa hilo nchini,
wakiwamo walei, mapadri na maaskofu walimtabiria Kardinali Pengo kushika nafasi
hiyo ya juu katika Kanisa Katoliki.
Walisema kuwa
kuna sababu za msingi zinazowezesha Kardinali Pengo kutwaa nafasi hiyo kutokana
na uzoefu wake katika kazi mbalimbali pamoja na uongozi wa kanisa akishika
nafasi mbalimbali kitaifa na kimataifa.
Kwa sasa
Kardinali Pengo ni mjumbe pekee kutoka Afrika kwenye Kamati ya Uenezi wa Imani
Duniani, ambayo kwa jina la kilatini inajulikana kama Propaganda
Fidei.
Kamati hiyo
ambayo ina wajumbe tisa kutoka duniani kote ilikuwa ikiongozwa na Kardinali
Joseph Ratzinger, ambaye ndiye Papa anayestaafu kwa sasa.
Akizungumza na
gazeti hili jana aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Jimbo Kuu
la Dar es Salaam, Joseph Selasini alisema kuwa kila nchi duniani ina nafasi ya
kutoa Papa Tanzania pia ikiwemo.
Alisema kuwa
Kardinali Pengo anaweza kupata nafasi hiyo kwani sheria ya Kanisa Katoliki
inasema kuwa kardinali yeyote kutoka duniani kote ni moja ya watu watakaopigiwa
kura hivyo kuweza kuwa Papa.
Alisema: “Kwa
kawaida nafasi hiyo inawakutanisha makardinali wote duniani, Makao Makuu ya
Kanisa Katoliki mjini Roma. Hapo kila mmoja anakaa kwenye chumba chake na
kupigia kura jina analolijua yeye.”
Alisema kuwa
uchaguzi wa Papa hauna kampeni tofauti na uchaguzi wa kisiasa na kwamba Papa
anaweza kupatikana ikiwa mmoja wa makadinali atakuwa amepata theluthi mbili ya
kura zitakazopigwa na ikiwa tofauti na kiwango hicho cha kura uchaguzi unaweza
kurudiwa.
Akizungumzia
zaidi kuhusu nafasi ya Kardinali Pengo alisema kuwa anaweza akapata nafasi hiyo
kwani hata yeye ni mmoja ya washiriki wa nafasi hiyo mwenye uzoefu mkubwa wa
kuongoza kanisa.
“Yeye ni
Mwafrika pekee ambaye ni mjumbe wa wajumbe wa Kamati ya Uenezi wa Imani ya
Kanisa Katoliki hilo kati ya wajumbe tisa duniani,” alisema
Selasini
Endelea
hapa>> http://www.mwananchi.co.tz
Post a Comment