MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamisi amemvua ujumbe wa Baraza la Umoja huo Taifa aliyekuwa mgombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Paul Makonda kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Taarifa kutoka ndani ya kikao cha baraza kuu la UVCCM zilizolifikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa Makonda alifukuzwa muda mfupi baada ya kufungulia kwa kikao hicho kinachoendelea mjini hapa.
Chanzo chetu kilieleza kuwa mara baada ya kuanza kikao hicho, Mwenyekiti alimwita Makonda na aliposimama alimweleza mbele ya wajumbe kuwa amemfuta ujumbe wa Baraza.
“Nimekuvua ujumbe kuanzia sasa kwani haiwezekani taarifa za chama ukazianika kwenye vyombo vya habari,” alilalamika mwenyekiti huyo.
Mapema asubuhi jana, Sadifa aliwaonya wajumbe kuwa asingekuwa na msalia mtume kwa watu ambao wanafanya shughuli za chama kinyume na matakwa kamili ikiwamo kuchanganya mapenzi na kazi za chama.
Alipotakiwa kuthibitisha kufukuzwa kwake Makonda alikiri kuwa alikuwa amefukuzwa na Mwenyekiti lakini akakataa kufafanua sakata hilo.
“Mimi ninachojua ni kuwa mwenye haki akionewa, mbingu husimama nyuma yake! Kama ni kufukuzuzwa ni kweli nimefukuzwa bila ya kujua sababu kamili,” alilalamika Makonda. Hata hivyo taarifa zilidokeza kuwa siku tatu kabla ya kikao hicho, alipigiwa simu na Mwenyekiti na kutakiwa ahudhurie kikao hicho.
Inaelezwa kuwa alipoingia kwenye kikao alifanya usajili kama wengine na kupewa posho pamoja na nyaraka za kikao hicho zinazofafanua juu ya ajenda.Taarifa za kuaminika zilieleza kuwa mara baada ya kupewa taarifa za kufukuzwa, mjumbe huyo alirudisha kwa hiyari yake makabrasha ya chama pamoja na posho zote kisha akaondoka eneo la mkutano.
Mkakati wa Sadifa kutumia madaraka yake kuwaadhibu wajumbe wenye tuhuma za kukiuka kanuni za UVCCM alianza kuzionyesha wazi wakati akifungua kikao cha Baraza hilo alipoonya mtu yeyote atakayekiuka maadili hatamwonea huruma.
Aliwaonya akisema hataona aibu kufanya hivyo hata kwa yule ambaye alikuwa akimfanyia ka mpeni zilizomwezesha kukalia kiti hicho.
“Sitavumilia upuuzi huo. Baada ya uchaguzi kupita mimi ni Mwenyekiti wa Vijana wote ndani ya chama changu wa Tanzania bila kujali kama walinichagua au hawakunichagua. Hivyo ninaomba tufanye kazi kwa kushirikiana kwa pamoja,” alisema Sadifa.
“Hata kama ulinipigia kampeni wakati wa uchaguzi mkuu ukifanya kosa nitakuwajibisha kama mtu mwingine yeyote na kamwe sitapendelea mtu eti kwa sababu tu alinipigia kampeni. Huu ni wakati wa kazi na wakati wa kazi tusicheke,” alionya.Mbali na hilo mwenyekiti huyo aliwatahadharisha viongozi wa jumuiya hiyo kujiepusha na vitendo vya kuchanganya kazi na mapenzi kwa madai kuwa vinazorotesha uwajibikaji ndani ya chama.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment