Taarifa kwa Vyombo vya Habari
18 Februari, 2013
Sikika yampongeza Waziri Mwinyi kwa Kuwajibika
Sikika inapenda kumpongeza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi kwa
kuweka bayana na kukiri kwamba kuna uhaba mkubwa wa dawa muhimu za kutibu malaria,
maarufu kama dawa mseto (Alu) katika vituo vingi vya huduma za afya vya umma nchini.
Akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni, waziri Mwinyi alikiri kuwepo kwa uhaba
wa dawa hizo za kutibu malaria kama zilivyoripotiwa na mtandao wa Wizara hiyo kupitia
mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ‘SMS for Life.’ Dk. Mwinyi alinukuliwa akiwataka
watanzania kutokuwa na wasiwasi kwani suala hilo lilikuwa linashughulikiwa na kwamba
usambazaji wa Alu ulishaanza.
Tunampongeza kwa dhati waziri Mwinyi kwa kukiri uwepo wa tatizo hili na kuchukua hatua.
Sikika tunaamini kwamba hatua hiyo ni muhimu katika kukuza uwajibikaji na uwazi. Wiki
mbili zilizopita, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Regina Kikuli
na Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja walikanusha taarifa iliyotolewa na Sikika
kwamba kuna uhaba wa Alu kwa takribani asilimia 26, katika vituo vya huduma za afya nchini.
Taarifa hizo zilipakana kutoka kwenye mfumo huo huo wa Wizara (SMS for life).
Taarifa ya Kikuli pia ilikaririwa na vyombo vya habari ikiueleza umma kwamba kuna dawa
nyingine za malaria ambazo haziripotiwi kupitia SMS for life, jambo ambalo si kweli.
Sikika inaiomba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuharakisha usambazaji wa dawa hizi na
ilichukulie suala hili kama dharura kwani kuna baadhi ya vituo vya huduma vina uhaba mkubwa
wa Alu kwa takribani siku 300 sasa. Pia tunaishauri Wizara kubadili mfumo wa uagizaji wa
dawa kwa zahanati na vituo vya afya ambao huvilazimu vituo kuagiza dawa kila baada ya miezi
mitatu (robo mwaka), wakati usambazaji wake unachukua muda wa miezi miwili hadi mitatu.
Ni vyema vituo viwe vinaagiza dawa kila mwezi ili kupunguza tatizo la uhaba wa dawa muhimu
unaojitokeza mara kwa mara.
Ikumbukwe kwamba msimu wa mvua unakaribia kuanza katika maeneo mengi hapa nchini
na hivyo kuwepo kwa uwezekano wa kuongezeka kwa maambukizi ya malaria. Ugonjwa wa
malaria unaongoza kwa kusababisha vifo vingi nchini. Hivyo basi, uwepo wa dawa za ALu za
kutosha katika vituo vya huduma utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo hivyo.
Ni jambo la kushangaza kuona kuwa ALu zinakosekana katika vituo vingi hapa nchili wakati
kuna fedha za kutosha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo. Kwa kipindi
cha miaka 10 iliyopita, Tanzania ilipokea kiasi cha dola za Marekani 331,112,207 kutoka
Global Fund pekee, ambapo kiasi cha dola za Marekani 294,975,327 tayari zimeshatumika.
Ukiachilia mbali Global fund, malaria pia imekuwa ikifadhiliwa na Mfuko wa Ufadhili wa Rais
wa Marekani (PMI – USAID), Benki ya Dunia (World Bank) pamoja na wahisani wengine.
Yapo makampuni makubwa manne ambayo yameteuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO)
kwa ajili ya kuleta dawa hizo hapa nchi. Makampuni haya yanatambulika kimataifa kwa kuwa na
uwezo mkubwa wa kuzalisha na kusambaza dawa hizo kwa vipindi maalum. Tatizo tunaloliona
hapa ni Wizara yetu kushindwa kufanya makadirio na kuagiza dawa hizo kwa wakati.
Ni wakati sasa kwa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), Bohari ya Dawa ya Taifa
(MSD), Kitengo cha Dawa cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (PSS) na Waganga Wakuu
wa Wilaya (DMOs) kuchukua hatua madhubuti za kutatua tatizo la uhaba wa Alu. Suluhu ya
tatizo hili ni kwa wote wanaohusika kuwajibika kwa dhati ili kuokoa maisha ya watanzania.
Vilevile, tunaishauri serikali kupanua wigo wa matumizi ya mfumo wa ‘SMS for Life’ ili
kuongeza dawa zingine muhimu na vifaa tiba. Mfumo huu unasaidia sana kutoa taarifa zenye
ukweli na uhalisia na kuhusu uhaba wa dawa ili wizara ijipange kukabiliana na tatizo hilo
kwa kusambaza dawa zinazohitajika kwa wakati. Mfumo huu pia utasaidia kwa kiasi kikubwa
kuboresha uwazi na uwajibikaji katika usambazaji wa dawa, hatimaye kuboresha utoaji wa
huduma za afya nchini.
Kwa namna ya pekee, Sikika inavipongeza vyombo vya habari kwa juhudi zao za dhati katika
kuuhabarisha umma juu ya tatizo la uhaba wa Alu. Vyombo hivyo vilitanguliza zaidi maslahi
ya umma bila kujali matamko ya wazi ya baadhi ya viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii ya kuupindisha ukweli. Kwa mara nyingine tena, vyombo vya habari vimeweza kuonesha
uzalendo kwa kuweka maslahi ya taifa mbele.
Mr. Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz ,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz
Post a Comment