Serikali inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa
hivi karibuni kumezuka kundi la Watu wadanganyifu ambao wamekuwa wakitumia
majina ya viongozi waandamizi wa serikali na Taasisi nyeti ikiwemo Usalama wa
Taifa kujipatia fedha kwa madai ya kutumwa na viongozi hao.
Watu hao wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa simu (SMS)
kwa maofisa mbalimbali wa wizara,mashirika ya umma na Idara za Serikali
zinazojitegemea kuomba pesa ili wawafanye mipango ya kupandishwa
vyeo.
Utapeli huo umekuwepo nchini kwa kipindi kirefu sasa ,
ambapo watu huwapigia simu viongozi wa Taasisi za fedha , Mifuko ya Taasisi za
Jamii na watu binafisi wakiomba fedha kwa madai ya kutumwa na viongozi
waandamizi Serikalini wakati si kweli.
Watu hao wamekuwa wakiwatapeli maofisa mbalimbali kuwa
wanaweza kuwafanyia mipango ya kupandishwa vyeo endapo watawapatia kiasi cha
fedha jambo ambalo halipo katika taratibu za utumishi wa umma.
Utumishi wa umma unazo taratibu zake za kuwapandisha
vyeo watumishi wake kulingana na sifa za kada zao na wala haiwezekani kwa
viongozi waandamizi kuwachangisha fedha kwa ajili ya kuwapandisha
vyeo.
Serikali inawataka wananchi kuwapuuza matapeli hao na
watoe taarifa katika vyombo vya dola na usalama mara wapatapo ujumbe wa aina
hiyo ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI (MAELEZO) DAR
ES SALAAM.
12.02.2013
Post a Comment