CHAMA cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimefuta wazo la kuendesha mdahalo kwa
wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF).
Mdahalo huo ulikuwa
ufanyike Februari 15, 2013 na tayari chama kilikuwa katika hatua nzuri ya
mazungumzo na wadhamini pamoja na kituo kimoja cha televisheni kwa ajili ya
kurusha 'live' tukio hilo, ambapo kesho ilikuwa tutangaze utaratibu mzima wa
mdahalo huo.
Katika mazungumzo ya leo na
uongozi wa kituo hicho ambao hautaki tukitangaze, tumekubaliana kufuta wazo la
mdahalo kwa sababu nafasi ya urais amebaki mgombea mmoja, hivyo mdahalo
hautakuwa na tija.
Dhamira ya awali ya kufanya
mdahalo ilikuwa kuwapa fursa wapiga kura wasikie vyema sera za wagombea urais na
Makamu wa Rais, ili wananchi wawasikilize wagombea hao na pia wapiga kura
wawatambue vizuri.
Hata hivyo TASWA itatafuta
utaratibu mwingine mzuri ambao utawezesha wagombea kuzungumza na waandishi wa
habari na kuulizwa maswali mbalimbali ambayo tunaamini kwa kiasi fulani
yatasaidia wapiga kura katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka
huu. TASWA inawatakia kila la kheri wagombea wote wa TFF
waliobakia.
TASWA imekuwa ikifanya
mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu kwenye uchaguzi wa TFF, ilifanya hivyo
mwaka 2001 na mwaka 2004 ingawa haukuwa wa live, ikafanya wa live mwaka 2008,
ambapo yote ilikuwa ya mafanikio makubwa.
Amir
Mhando
Katibu Mkuu
TASWA
12/02/2013
Post a Comment