Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Wachezaji
Mpira wa Miguu Tanzania (SPUTANZA) na wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu
Tanzania (FRAT) uliochaguliwa wiki iliyopita.
Uongozi wa FRAT
ulichaguliwa Februari 13 mwaka huu mjini Morogoro wakati wa SPUTANZA
ulichaguliwa jana (Februari 17 mwaka huu) katika uchaguzi uliofanyika Kigamboni,
Dar es Salaam.
Waliochaguliwa kuongoza
SPUTANZA na hawakuwa na wapinzani ni Musa Kissoky (Mwenyekiti) na Said George
(Katibu Mkuu) wakati Ali Mayai aliwashinda Isaac Mwakatika na Hakim Byemba
katika nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
Kusianga Kiata na Charles
Mngodo walichaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya SPUTANZA. Katika
uchaguzi huo uliohudhuriwa na wapiga kura 17, Mhazini na nafasi moja ya mjumbe
wa Kamati ya Utendaji zitajazwa baadaye kutokana na kukosa
wagombea.
Kwa upande wa FRAT viongozi
waliochaguliwa ni Said Nassoro (Mwenyekiti), Charles Ndagala (Katibu Mkuu) na
Kamwanga Tambwe (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF).
Ushindi waliopata viongozi
waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo unaonesha jinsi wapiga kura walivyo na imani
kubwa kwao, na TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji
ya FRAT na SPUTANZA.
Uongozi huo mpya una
changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa
miguu kwa kuzingatia katiba zao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu
yao.
Pia tunatoa pongezi kwa
kamati za uchaguzi za FRAT na SPUTANZA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa
kuhakikisha uchaguzi umeendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama
wa TFF.
Post a Comment