Moja ya vazi la kanga lililobuniwa na Chichia. Picha
ya Urban Pulse
Moja ya Ubunifu wa Anna Luks. Picha na Urban
Pulse
Mheshimiwa Balozi Peter Kallaghe akiwa na mwanamuziki
Freddy Macha aliyetumbuiza shughuli hii na gitaa lake. Picha na Fred
Mchaki
Anna
Luks na Christine Mhando. Picha ya Urban Pulse
Moja ya ubunifu wa Jacquiline Kibacha uliohamasishwa
na jadi ya Wamasai. Picha ya F. Macha
Jacquiline
Kibacha akipokea tuzo ya mapambo iitwayo “Fashions Finest 2012” mjini London
mwezi Novemba mwaka jana. Picha na Simon Klyne
Jacquiline
Kibacha anayetumia jina la Heart 365. Picha na F. Macha
Marim Mungula, Baraka Baraka, Anna Luks, Wilkins Kiondo,
Chichia, Samson Soboye. Picha na Fred Mchaki.
---
Imeandikwa na Kuletwa hapa Hakingowi.com na Freddy Macha
Picha za Urban Pulse na F. Mchaki
Maonyesho maarufu ya mavazi –London Fashion Week-
yaliyoanza rasmi Ijumaa iliyopita mjini London yameiweka ramani ya Tanzania
duniani.
Shughuli hii muhimu kiuchumi na kisanaa inayoendelea
juma zima na kuhusisha vituo vya kitamaduni na balozi 27 ina lengo la kutangaza
vipaji vya wabunifu mavazi toka nchi zisizojulikana uwanja huu mahiri wa
kimataifa unaosifika takriban miaka 30 sasa.
“London Fashion Week” ni moja ya maonyesho manne
ulimwenguni yaliyoasisiwa rasmi kutukuza ubunifu, ufundi na biashara mwaka
1984. Huendeshwa sambamba miji ya New York, Milan na Paris kila mwezi Februari
na Septemba.
Watanzania tulioingia kwa dhamira ya “Swahili Flavour”
(Ladha ya Kiswahili) tumefadhiliwa na Ubalozi wa Tanzania London ukishirikiana
na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB). Watayarishaji wa shughuli hii ni shirika la
kitamaduni na elimu Uingereza- British Council lenye mahusiano ya kirafiki na
nchi 100 duniani.
“Maonyesho ya mavazi London ni fani ya hali ya juu na
kibiashara ambapo waume kwa wanawake huwa pamoja wakibadilishana mapambo na
visaidizi vyake,” anasema Julian Roberts, mbunifu mavazi wa British
Council.
Akiongea rasmi kwenye ufunguzi wa Ijumaa uliokuwa na
vinywaji baridi na muziki wa Kiswahili, mke wa Balozi Uingereza, Mama Joyce
Kallaghe aliwasifu wabunifu mavazi wetu na kuwakabirisha wageni mbalimbali
waliohudhuria “kuzitembelea mbuga nzuri za Kitanzania kama watafurahishwa na
mavazi na ladha yetu ya Kiswahili.”
Wabunifu na washoni hao watatu ni Christine Mhando (
“Chichia London”), Anna Lukindo ( “Anna Luks”) na Jacquleine Kibacha (“Heart
365”). Kibacha ambaye pia ni mtunzi wa mashairi huchanganya desturi za kijadi na
kisasa kwa shanga shanga, manyoya ya ndege na mapambo yaliyotokana na sanaa za
Wamasai. Miezi mitatu iliyopita kazi zake Kibacha zilipata tuzo maarufu la
“Fashions Finest 2012.”
Akifafanua fani yake, Christine “Chichia” Mhando
aliyehitimu chuo cha Usanii cha Kent mwaka 2002 alisema yeye huhamasisha vazi la
Kanga, misemo na maneno ya Kiswahili mathalan “Tongoza”, “Ala Kumbe!” na
“Zungumza” kama wajihi wa kazi hiyo. Anna Luks aliyefuzu shahada ya mwanzo (BA)
chuo cha Middlesex, alieleza azma yake ni kumwonyesha mwanamke wa Kitanzania
alivyo kupitia mitindo kama “dunia pana” , “kaba roho” na “baibui.” Anna Luks
huchanganya ushonaji wa mikono, kamba kamba na mavazi ya kisasa.
Naibu Balozi, Mheshimiwa Chabaka Kilumanga alisema
maonyesho haya ya kimataifa yatakua nafasi kubwa kwa Tanzania kujitangaza
kibiashara na ni sehemu mahsusi ya fahari ya utamaduni wetu.
Wahusika wengine waliochangia mafanikio ya shughuli ni
Mratibu Ubalozini, Bi Rose Kiondo; Afisa mwangalizi wa onyesho hilo, Samson
Soboye na Meneja wa dhana ya Swahili Flavour, Mike Puplampu.
Habari zilizopatikana jana zilisema kwamba wabunifu
mavazi wa Kitanzania wametajwa ndani ya kundi la washindi kumi bora. Ushindi huo
unathibitisha dhahiri uwezo wa sanaa na ubunifu wetu ndani ya hulka ya mavazi ya
kimataifa.
Tovuti: www.freddymacha.com
Post a Comment