Shirika la utafiti wa anga la Marekani – NASA – linafuatilia kwa karibu sayari ndogo ambayo itapita karibu na dunia leo Ijumaa, ambayo shirika hilo limesema ndiyo ya mwanzo yenye ukubwa huo kuwahi kupita karibu kabisa na dunia.
Sayari hiyo iliyopewa jina la 2012 DA 14 na ambayo ina kipenyo cha mita 45, itapita kwa kasi katika umbali wa kilomita 27,000 kutoka uso wa dunia, saa nne na dakika ishirini na tatu usiku kwa saa za Afrika mashariki.
NASA imesema katika umbali huo, sayari hiyo haitaathiri satelaiti zinazoizunguka dunia na kuongeza kuwa hakuna haja ya kuwa na wasi wasi.
Watu katika nchi za Ulaya Mashariki, Australia na Asia wataweza kuiona sayari hiyo.
Wanasayansi wa NASA wanakadiria kuwa sayari ya ukubwa kama wa 2012 DA 14 hupita karibu na dunia kila baada ya miaka 40, na huigonga dunia kila baada ya miaka 1, 200.