Walimu watatu wa Shule ya
Msingi Misingeni katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wamejeruhiwa sehemu mbalimbali
za miili yao kufuatia kushambuliwa na kundi la wazazi wenye watoto kwenye shule
hiyo.
Akizungumza na mwandishi,
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hilda Msita alisema wazazi hao walivamia shule
kupinga kitendo cha Mwalimu wa shule hiyo, Mathias Banzi kuwaadhibu watoto wao
kwa kuwachapa viboko kutokana na utovu wa nidhamu. Mwalimu Msita alisema baada
ya kutokea vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu kwa watoto hao, Mwalimu Banzi
aliwachapa viboko wanafunzi hao na ndipo mwanafunzi mmoja (Fadhili Mlibo)
alikimbia na kwenda kutoa taarifa kwa wazazi wake kuhusu jambo hilo.
Alisema kuwa baada ya kufika
nyumbani na kutoa taarifa kwa wazazi wake, Mama wa mwanafunzi huyo, Amina
Rashidi aliwaeleza wazazi wengine wenye watoto shuleni hapo na ndipo kundi la
wazazi zaidi ya 20 walivamia shule wakiwa na silaha za jadi na kuwajeruhi
walimu.
Mwalimu Mkuu wa shule huyo,
Hilda Msita aliwataja walimu waliojeruhiwa kwenye sakata hilo kuwa ni pamoja na
Mathias Banzi, Barnabas Matalisi na Sikujua Bunoge, ambao baada ya kipigo cha
wazazi hao walitibiwa katika hospitali ya mkoa Kigoma Maweni na
kuruhusiwa.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda
wa Polisi Mkoa Kigoma, Mohammed Kihenya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kwamba polisi inamshikilia Amina Rashidi mzazi wa mmoja wa watoto walioadhibiwa
katika sakata hilo. Kamanda Kihenya alisema kuwa pamoja na kumshikilia mzazi
huyo kwa kufanya vurugu mahala pa kazi na kujeruhi, pia inawatafuta watu wengine
ambao walihusika katika vurugu hizo.
Post a Comment