Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akizindua kitabu cha Mwongozo wa Usanifu wa Barabara. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Saidi Amani na kushoto ni Eng. Joseph Nyamuhanga, Mkurugenzi wa Barabara katika Wizara ya Ujenzi.
Msajili wa Bodi ya Wabunifu na Wakadiriaji Majenzi, Arch. Jehad akipokea kitabu cha Mwongozo wa Usanifu wa Barabara kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) mara baada ya kuzinduliwa rasmi. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Saidi Amani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Herbert E. Mrango akipokea kitabu cha Mwongozo wa Usanifu wa Barabara kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, mara baada ya kuzinduliwa rasmi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Eliya Ntandu akipokea kitabu cha Mwongozo wa Usanifu wa Barabara kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) mara baada ya kuzinduliwa rasmi. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Saidi Amani.
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (wanne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Morogoro.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (Mb), leo amezindua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi ambalo linakutana kwa siku mbili mjini Morogoro. Wakati akiongea katika uzinduzi wa Baraza hilo linalojumuisha wajumbe kutoka katika taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Mheshimiwa Magufuli amewapongeza watendaji wakuu wa wizara na taasisi zake kwa namna wanavyosimamia utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi. “Mafanikio yanayoonekana kupatikana kwa upande wa wizara yetu ni matokeo ya usimamizi wenu mzuri” alielezea Waziri Magufuli na kuwataka kutorudi nyuma kwani hiyo ni dhamana waliyopewa na Taifa.
Akizungumzia changamoto zilizopo, Waziri Magufuli alisisitiza kukerwa kwa kuendelea kujitokeza vitendo vya rushwa katika vituo vya mizani na kwenye vivuko. Mhe. Magufuli amezipongeza hatua zilizokwisha kuchukuliwa na Mtendaji Mkuu wa Tanroads kwa kutangaza ajira za wafanyakazi wa vituo vya mizani na amemtaka kukamilisha mapema ajira za Wahandisi watakaosimamia vituo hivyo. “Hatua hizi tuzimechukua baada ya kubaini kuwa karibu asilimia themanini ya watendaji waliopo katika vituo vya mizani ni wala rushwa” alibainisha Mheshimiwa Waziri Magufuli.
Kwa upande mwingine Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) nao umepewa siku sitini ili kuanza zoezi la ukatishaji tiketi za elektoniki hasa katika kivuko cha Kuvukoni jijini Dar es Salaam. Waziri Magufuli alibainisha baadhi ya mbinu zinazotumiwa na watendaji wasio waaminifu katika vivuko hivyo, kuwa ni pamoja na kujichapishia tiketi kwa siri na wakati mwingine kutochana tiketi wanazozipokea kutoka kwa abiria kwa lengo la kuziuza tena.
Waziri Magufuli hata hivyo amepongeza zoezi la kukamata magari ya Serikali yanayotumia namba za binafsi kinyume na sheria. “Tayari hadi sasa jumla ya magari 1,830 tayari yamekamatwa na kusajiliwa kwa namba za Serikali” alifafanua Mheshimiwa Magufuli..
Wakati huo huo Waziri wa Magufuli pia amekizundua Kitabu cha Mwongozo wa Usanifu wa Barabara. Kitabu hicho kitatumiwa katika utekelezaji wa shughuli za ujenzi na matengenezo ya barabara hapa nchini.
Wakati akizindua kitabu hicho Mheshimiwa Waziri amewapongeza Mameneja wa Tanroads wa mikoa ya Dodoma na Morogoro kwa ubunifu ambao wameuonyesha kwa kutumia fedha wanazotengewa katika bajeti zao. Alielezea kufurahishwa na kazi za upanuzi wa barabara unaoendelea kuanzia eneo la Ihumwa hadi Dodoma Mjini ambao ni matokeo ya jitihada za watendaji wenyewe mkoani. Hapa Morogoro pia kazi hizi za upanizi wa barabara zimeelezwa kuanza kutekelezwa wakati ambapo mkoani Tabora tayari kuna zaidi ya kilometa sita za lami zimejengwa kwa kutumia fedha zilizotengwa katika bajeti ya mkoa. “Ninawaelekeza Mameneja wa Tanroads katika mikoa mingine nanyi muwe na ubunifu na sio kukaa bila ya kuchukua hatua zozote hata pale ambapo tayari kuna bajeti iliyopitishwa” alimalizia Mheshimiwa Magufuli.
Post a Comment