LIGI Kuu ya Vodacom (VPL)
kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 23 mwaka huu) kwa
mechi tatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu yatakuwa
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Uwanja huo wa kisasa utakuwa
mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na makamu bingwa Azam. Ingawa Azam imecheza
mechi moja zaidi, lakini timu hizo zinatofautishwa kwa uwiano wa mabao ya
kufunga na kufungwa kwenye msimamo wa ligi huku kila moja ikiwa na pointi
36.
Pia vinara wa ufungaji kwenye
ligi kwa sasa wanatoka katika timu hizo mbili. Kipre Tchetche aliyepachika mabao
tisa hadi sasa ndiye anayeongoza akifuatiwa na Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye
mabao manane.
Iwapo timu yoyote itafanikiwa
kuondoka na pointi tatu katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Hashim
Abdallah wa Dar es Salaam, kasi ya mbio za kuwania ubingwa itaongezeka. Waamuzi
wasaidizi watakuwa Hamis Chang’walu wa Dar es Salaam na John Kanyenye kutoka
Mbeya wakati mezani atakuwepo Oden Mbaga.
Mechi nyingine za kesho ni
Mgambo Shooting dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga
wakati Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Jumapili (Februari 24 mwaka
huu), Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa katika hekaheka nyingine kwa Simba
chini ya Mfaransa Patrick Liewig kuikabili Mtibwa Sugar inayonolewa na nahodha
wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime.
FDL YAENDELEA KUSHIKA
KASI
Michuano ya Ligi Daraja la
Kwanza (FDL) inaendelea wikiendi hii kwa mechi kumi na moja katika viwanja
tofauti. Timu hizo zinapambana kutafuta hadhi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) msimu ujao 2013/2014.
Kesho (Februari 23 mwaka huu)
kundi A litakuwa na mechi moja itakayozikutanisha timu za Mkamba Rangers na JKT
Mlale itakayochezwa Uwanja wa Ruaha mkoani Morogoro.
Kundi B lenyewe litakuwa na
mechi mbili; Tessema itacheza na Ashanti United katika Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Dar es Salaam wakati Ndanda itaikaribisha Polisi Dar es Salaam kwenye
Uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara.
Raundi ya 12 ya ligi hiyo
kundi A itashuhudia timu zote nane zikiwa viwanjani; Pamba vs Mwadui (CCM
Kirumba), Polisi Tabora vs Polisi Mara (Ali Hassan Mwinyi), Polisi Dodoma vs
Morani (Jamhuri) na JKT Kanembwa vs Rhino Rangers (Lake
Tanganyika).
Jumapili (Februari 24 mwaka
huu) kundi A litakuwa na mechi kati ya Burkina Faso dhidi ya Kurugenzi
(Jamhuri), Majimaji vs Polisi Iringa (Majimaji) wakati kundi B ni Transit Camp
vs Villa Squad (Karume), na Green Warriors vs Moro United
(Mlandizi).
FIFA KUSIKILIZA MADAI YA
ASAMOAH DHIDI YA YANGA
Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA) limesema linapeleka rasmi madai ya mchezaji wa zamani wa
Yanga, Kenneth Asamoah kwenye chombo chake cha utatuzi wa migogoro (Dispute
Resolution Chamber) baada ya klabu hiyo kutojibu chochote.
Awali FIFA ilipokea
malalamiko ya Asamoah kuwa anaidai Yanga dola 5,000 za Marekani ambapo ilikuwa
ni sehemu ya malipo yake (signing fee) baada ya kujiunga na klabu
hiyo.
Desemba mwaka jana FIFA
iliiandikia barua Yanga kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
ikitaka maelezo yake kuhusu madai hayo ya Asamoah, lakini hadi sasa haijajibu
madai hayo.
Kwa mujibu wa FIFA, hatua ya
uchunguzi wa suala hilo umekamilika, na sasa linapelekwa rasmi katika chombo
chake cha utatuzi wa migogoro (Dispute Resolution Chamber) kwa ajili ya kufanya
uamuzi.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF)
Post a Comment